Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-10 16:36:56    
Qingming, Siku ya kuanza kwa "kipindi angavu"

cri

Kwa mujibu wa mabadiliko ya hali ya hewa Wachina wamegawanya mwaka mzima kwa vipindi 24, na "kipindi kiangavu" ni moja kati ya vipindi hivyo.

"Vipindi 24" nchini China vimekukwepo kwa miaka zaidi ya 2000. Kupatikana kwa vipindi hivyo ni busara ya wahenga wa kale waliofanya uchunguzi wa muda mrefu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na unajimu, ni urithi mkubwa wa utamaduni wa China, na vipindi hivyo vinahusiana moja kwa moja na maisha ya Wachina. Kwa ufupi, vipindi hivyo vimepatikana kwa kugawa sawa sawa mwaka mzima kwa vipindi 24, na kwa ujumla hali ya hewa katika kipindi kimoja ni sawa, na siku ya kuanza kwa kipindi hicho, inapewa jina. Kwa kawaida Qingming yaani siku ya kuanza kwa "kipindi kiangavua" huwa kati ya tarehe 4, 5 au 6 Aprili. Mwaka huu siku hiyo ni tarehe 4 Aprili.

Kipindi hicho kwa Kichina kinaitwa Qingming, maana yake ni kuwa "mimea yote inachipuka na kila kitu kinakuwa safi na angavu". Katika kipindi hicho, mvua inaongezeka, na ni msimu wa shughuli za kilimo, Wachina huwa wanasema "mbegu zinatakiwa kupandwa kabla na baada ya Qingming" na "miti haitakiwi kupandwa baada ya Qingming".

Qingming inaonesha mabadiliko ya hali ya hewa, lakini pia ni aina moja ya utamaduni wa jadi nchini China, na utamaduni huo umeorodheshwa na serikali ya China katika urithi wa utamaduni wa jadi, maana Qingming ni siku ya kuwakumbuka marehemu.

Katika siku hiyo watu wa kabila la Wahan na baadhi ya makabila madogo huwa wanakwenda kusafisha makaburi. Katika sehemu fulani za vijijini wenyeji wana mila ya kuzika maiti, wanafanya tambiko mbele ya makaburi ya jamaa zao kwa pombe, keki na matunda, kuwasha udi, kufyeka magugu na kuongeza udongo kwenye makaburi, kisha wanapiga magoti na kumwaga pombe mbele ya makaburi. Kwa mujibu wa data za historia, katika siku hiyo sehemu nyingi nchini China mbingu huwa na mawingu mawingu au mvua za rasharasha huwa zinanyesha, hali hiyo inachangia huzuni za watu kwa marehemu. Mshairi mkubwa wa karne ya tisa Bw. Du Mu kwenye mashairi yake alieleza mazingira ya siku hiyo akisema "Siku ya Qingming mvua za rasharasha zinanyesha, watu waendao kusafisha makaburi wanahuzunika karibu kufa."

Hadi sasa, Wachina wanaendelea kuwa na mila hiyo ya kuwakumbuka marehemu katika siku hiyo. Kwa sababu katika sehemu nyingi mijini na vijijini maiti huchomwa, katika siku hiyo watu huenda kwenye sehemu ya makaburi kuweka maua kwa ajili ya jamaa waliokufa.

Siku hiyo licha ya kuwakumbusha watu wawakumbuke jamaa zao waliokufa pia ni siku ya kuanza kwa hali ya hewa kubadilika kuwa joto, majani na miti inaanza kuchipuka, kwa hiyo Wachina hutumia siku hiyo kutembelea nje ya miji kuangalia mandhari ya Spring. Kwa mujibu wa maandishi ya kihistoria, katika siku hiyo wahenga wa China walikuwa na mila ya kucheza bembea, mpira wa miguu na kurusha vishada. Mpira wa miguu waliocheza wahenga wa China ulikuwa ni mpira wa ngozi uliotunishwa kwa manyoya ya wanyama, mchezo huo ulienea nchini China miaka 2200 iliyopita. Mwaka 2004 mchezo huo ulikubaliwa na FIFA kuwa ni mwanzo wa mchezo wa soka duniani. Hadi sasa Wachina wanaendelea kuwa na mila ya kurusha vishada na kufanya matembezi nje ya miji, lakini wengi wao wanasafiri kwa magari yao binafsi badala ya kutembea.

Qingming yaani siku ya kuanza kwa "kipindi kiangavu" ni siku ya mabadiliko ya hali ya hewa, lakini pia ni siku yenye shughuli nyingi za jadi, licha ya kuwa ni siku ya kuwakumbuka marehemu pia ni siku ya kuburudika na mandhari ya Spring nje ya miji, hii ni hali pekee katika vipindi 24.