Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-12 20:22:11    
Mbio za mwenge wa michezo ya Olimpiki zakamilika kwa mafanikio mji wa Buenos Aires

cri

Tarehe 11 Aprili mbio za mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing zimekamilika kwa mafanikio huko Buenos Aires, mji mkuu wa Argentina. Mji huo ni mji wa 7 katika safari za mwenge huo nje ya China Bara, ambapo mwenge wa michezo ya Olimpiki ulikimbizwa kwa kupokezana na watu 80 kwa muda wa saa 2 na nusu.

Siku hiyo baridi kali ziliukumba mji huo, hata hivyo ukarimu wa wakazi wa huko haukuzuiliwa na upepo mkali, ambapo malaki ya watu walimiminikia barabarani kukaribisha mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing na mbio za mwenge huo zilikamilika kwa shangwe na furaha za watu.

Meya wa Buenos Aires Bw. Mauricio Macri alieleza kufurahia mafanikio ya mbio hizo. Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema "Mbio hizo zimefanyika kwa mafanikio, hili ni tamasha kubwa. Nina matumaini kuwa, walimwengu wanapata ufahamu mwingi zaidi kuhusu mji wetu kwa kupitia shughuli hizo za kukimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki, ninawaalika kutembelea Buenos Aires. Vile vile naona michezo ya Olimpiki ya Beijing itapata mafanikio makubwa zaidi katika historia ya michezo ya Olimpiki."

Mbio hizo za mwenge wa michezo ya Olimpiki zilianza kutoka ukumbi wa Lola Mora ulioko kwenye eneo la bandari, na kumalizika katika klabu ya mchezo wa farasi. Mchezaji maarufu wa Argentina wa mchezo wa mashua Bw. Carlos Espinola alikuwa wa kwanza kukimbiza mwenge huo, na Bi. Gabriela Sabatini aliyewahi kuwa nyota mchezaji wa tenis wa Argentina, alichaguliwa kuwa mtu wa mwisho wa kukimbiza mwenge huo. Mchezaji huyo maarufu wa tenis alisema "Jambo pekee la kuchaguliwa kuwa mkimbiza mwenge ni fahari kubwa kwangu, kwani hii ni mara yangu ya kwanza kupata fursa hiyo. Zaidi ya hayo nilichaguliwa kuwa mtu wa mwisho wa kukimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing nchini Argentina, hii ni sifa maalumu. Naona nina bahati kweli."

Usiku wa tarehe 11 kwa saa za Argentina, ndege maalumu iliyobeba moto mtakatifu wa michezo ya Olimpiki ya Beijing iliondoka Buenos Aires na kuelekea Dar es Salaam, Tanzania ambao ni mji pekee uliochaguliwa kukimbizwa mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing katika bara la Afrika. Na mbio za mwenge huo zitafanyika tarehe 13 mjini Dar es Salaam.

Kuhusu mbio hizo, meya wa Dar es Salaam Bw. Adam Kimbisa alisema, shughuli za kukimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki zitachangia maendeleo ya utamaduni na uchumi wa Tanzania. Wakazi wa mji wa Dar es Salaam wanaona fahari kubwa kutokana na mji huo kuchaguliwa kuwa mji pekee barani Afrika utakaokimbizwa mwenge wa michezo ya Olimpiki. Alisema hivi sasa maandalizi ya mbio hizo yamekamilika, watu wanasubiri kwa hamu ujio wa moto mtakatifu, na watafanya sherehe mbalimbali za kukaribisha mwenge huo.

Bw. Kimbisa aliongeza kuwa, mbio za mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing zinasaidia kuonesha picha nzuri ya Tanzania na mji wa Dar es Salaam. Alieleza matumaini yake kuwa, kutokana na shughuli hizo, Tanzania na Dar es Salaam zitaweza kuvutia watalii wengi na uwekezaji mwingi zaidi. Ndiyo maana shughuli hizo za kukimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing zitanufaisha China na Tanzania kwa pamoja.