Mikutano ya 17 ya mawaziri ya kamati ya sarafu na mambo ya fedha ya kimataifa na Benki ya Dunia ilifanyika kwa nyakati tofauti huko Washington tarehe 12 na 13, ili kujadili masuala ya bei za nafaka na mgogoro wa fedha duniani. Sababu zilizoyafanya mashirika ya fedha ya kimataifa kufuatilia suala la bei za nafaka za duniani, na kulihusisha suala hilo na suala la mgogoro wa mambo ya fedha ni kupanda kwa mfululizo kwa bei za nafaka duniani, ambapo nchi nyingi zinakabiliwa na hatari ya njaa.
Bei za nafaka duniani zilianza kupanda kutoka mwaka 2002, isipokuwa zimekuwa zinapanda kwa haraka zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia zinaonesha kuwa, bei za nafaka zilipanda kwa 83% katika miaka 3 iliyopita, hususan bei ya ngano, ambayo ilipanda kwa 181%. Licha ya kupanda kwa bei za nafaka, akiba ya nafaka duniani inapungua, suala la usalama wa chakula limekuwa tatizo kubwa. Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa limekadiria kuwa, akiba ya nafaka ya duniani imepungua hadi kiwango cha chini zaidi tokea mwaka 1980. Kupanda kwa kiwango kikubwa kwa bei za nafaka, si kama tu kutazidisha gharama za maisha ya watu wa kawaida, bali pia kutaathiri utulivu wa jamii katika baadhi ya nchi.
Katika miezi michache iliyopita, kupanda kwa bei za nafaka kulisababisha ghasia katika nchi za Misri, Cameroon, Cote d'Ivoire, Ethiopia, Madagascar, Philippines na Indonesia. Nchini Haiti, ambako wanategemea kuagiza chakula kutoka nchi za nje, kupanda kwa bei za chakula kulisababisha ghasia za kimabavu zilizodumu kwa zaidi ya wiki moja, na hatimaye zilisababisha kuanguka kwa serikali. Mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha la kimataifa Bw. Dominique Strauss-Kahn kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 12 mwezi Aprili, alitoa onyo kuhusu mgogoro kuhusu nafaka na athari zinazoweza kuletwa kwa uchumi na siasa, alisema hali hii ya kupanda kwa bei za nafaka ikiendelea hivyo, italeta matokeo ya kutisha, na watu laki kadhaa duniani watakabiliwa na tishio la njaa. Historia imedhihirisha kuwa njaa mara kwa mara inasababisha kutokea kwa vita.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Bw. Robert Zoellick alisema, katika nchi nyingi zinazoendelea, maghala yanayotumiwa na watu maskini kununua chakula inafikia kiwango cha juu cha 75% ya pato lao, kupanda kwa bei za chakula ni pigo kubwa kwa maisha ya watu maskini. Bei kubwa za nafaka zinafanya baadhi ya nchi maskini zikabiliwe na hatari ya njaa, na huenda zitasababisha kutokea kwa msukosuko wa kijamii katika baadhi ya nchi. Mgogoro wa upungufu wa chakula utaweza kuharibu kabisa mafanikio iliyoyapata jumuiya ya kimataifa katika jitihada za kuwasaidia watu maskini.
Kuhusu hali mbaya ya nchi ya Haiti, Benki ya Dunia tarehe 12 ilitangaza kutoa mkopo wa dola milioni 10 kwa nchi hiyo, kuunga mkono mradi wa usalama wa jamii wa serikali ya Haiti, ikiwa ni pamoja na kutoa chakula kwa shule na kuongeza nafasi za kazi. Aidha Bw. Zoellick alitoa mpango wa chakula wa dunia ili kutatua mgogoro wa nafaka. Kutokana na mpango huo, Bw. Zoellick amezihimiza nchi mbalimbali kutoa mchango wa dola za kimarekani zaidi ya milioni 500 kwa shirika la mpango wa chakula duniani ili kutatua mgogoro wa chakula uliopo hivi sasa. Benki ya Dunia nayo itaongeza mikopo kwa karibu maradufu kwa sekta za kilimo za nchi za Afrika, ambayo inakaribia dola za kimarekani milioni 800.
Baadhi ya wataalamu wanasema, sababu nyingine kubwa inayosababisha kupanda kwa bei za nafaka ni kuwa nchi zilizoendelea zimepunguza misaada ya nafaka kwa nchi zinazoendelea, ambapo zinahimiza kuzalisha nishati kwa kutumia nafaka. Vyombo vya habari vinaona kuwa, nchi zilizoendelea zinapaswa kubeba jukumu la kuongeza misaada ya nafaka kwa nchi zinazoendelea.
|