Rais Mwai Kibaki wa Kenya tarehe 13 huko Nairobi alitangaza kuwa, serikali ya mseto ya nchi hiyo inayoundwa na chama cha PNU kinachoongozwa naye, na chama cha upinzani ODM kinachoongozwa na Bw. Raila Odinga imeanzishwa rasmi, na Bw. Oding ameteuliwa kuwa waziri mkuu wa serikali. Matokeo hayo yameondoa hali ya mvutano nchini humo kuhusu kuundwa kwa serikali ya mseto. Hadi sasa mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Kenya uliodumu kwa zaidi ya miezi mitatu umemalizika. Wachambuzi wanaeleza kuwa, ingawa kuundwa kwa serikali ya mseto kunaonesha kuwa Kenya imepiga hatua kubwa katika njia ya kuelekea kwenye amani, lakini serikali mpya bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, na Kenya bado inahitaji muda wa kutimiza amani, ustawi na utulivu halisi.
Kwenye serikali ya mseto, waziri mkuu Bw. Odinga anashughulikia usimamizi na uratibu wa mambo ya idara mbalimbali kwenye baraza la mawaziri. Bw. Uhuru Kenyatta aliyeteuliwa na chama cha PNU na Bw. Musalia Mudavadi aliyeteuliwa na chama cha ODM wamechaguliwa kuwa manaibu mawaziri wakuu. Wanachama wa vyama hivyo viwili wanashika nyadhifa nyingine za uwaziri kutokana na kanuni ya mgawanyo wa madaraka kwa usawa. Tarehe 13 Rais Kibaki alisema kuundwa kwa serikali ya mseto kunatokana na majadiliano ya pande mbalimbali, pia kumezingatia vya kutosha uwiano wa kikanda na changamoto zinazoikabili nchi hiyo. Pia aliahidi kuwa serikali ya mseto itafanya juhudi zote, ili kuihimiza Kenya ipate maendeleo kwa kuelekea upande wa amani, umoja na utulivu, na kuhimiza mawaziri wote wasaidie Kenya ipate utulivu mapema.
Gazeti kubwa nchini Kenya Daily Nation tarehe 14 lilitoa maelezo likisema, ingawa serikali ya mseto imeanzishwa, lakini bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Suala la kwanza linaloikabili nchi hiyo ni kuwa kama serikali hiyo itakuwa na umoja, na kushughulikia vizuri mambo ya nchi. Ingawa chama cha tawala na chama cha upinzani vimefikia makubaliano kuhusu mgawanyo wa madaraka, na kupunguza kwa muda hali ya mvutano kati yao, lakini kutokana na kuwa vyama vyote hivyo viwili vinashika madaraka ya idara muhimu kwenye serikali, kuna uwezekano kuwa kutakuwepo hali ya kuzuiana na kususiana kati yao.
Suala la uchumi ni changamoto nyingine inayoikabili serikali hiyo. Mgogoro wa uchaguzi wa rais umeleta pigo kubwa kwa uchumi nchini Kenya, na makadirio ya ongezeko la uchumi wa nchi hiyo kwa mwaka huu limepungua hadi asilimia 4.5 kutoka asilimia 6.9. Shughuli za utalii ambazo ni nguzo ya uchumi wa nchi hiyo pia zilikumbwa na athari mbaya, na zimepata hasara ya dola za kimarekani zaidi ya bilioni moja. Mgogoro huo vilevile uliathiri uuzaji nje wa chai na kahawa. Aidha kutokana na kupanda juu kwa kiasi kikubwa kwa bei ya chakula kwenye soko la kimataifa, bei ya vitu nchini Kenya pia inapanda, na zaidi ya nusu ya watu wenye matatizo makubwa ya kiuchumi wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa maisha, na hali ya mfumuko wa bei inazidi kuwa mbaya, na thamani ya fedha za Kenya inazidi kushuka. Ndiyo maana kutatua masuala ya uchumi na maisha ya wananchi ni changamoto kubwa inayoikabili serikali ya mseto ya Kenya.
Hivi sasa serikali ya Kenya inachukua hatua za kupanga maisha ya wakulima waliokimbia makazi yao kutokana na mgogoro wa uchaguzi mkuu, na kuwapatia mbegu na mbolea ili kuwasaidia warejee nyumbani kwao mapema, na kuanza maisha ya kawaida. Serikali ya Kenya pia imeanzisha Idara inayoshughulikia maendeleo ya sehemu ya kaskazini ya Kenya na sehemu nyingine zenye ukame, ili kuhimiza maendeleo kwenye sehemu hizo zilizopuuzwa zamani, na kuinua kiwango cha maisha ya watu wa huko. Serikali ya mseto pia inataka kuhimiza wananchi kuongeza imani yao kwa serikali kwa kutumia sera ya kuwanufaisha wananchi. Watu wanafuatilia kama sera hizo zitafanya kazi au la.
|