Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-17 16:53:44    
Majumba ya makumbusho nchini China yafunguliwa kwa watazamaji bila malipo

cri

Nchini China majumba ya makumbusho yamefunguliwa bure kwa umma badala ya kutoza kiingilio kama ilivyokuwa hapo kabla. Hii ni hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Utamaduni ya China hivi karibuni ili kunufaisha umma. Hadi kufikia tarehe mosi Aprili majumba 600 ya makumbusho yamefunguliwa bure na mwaka kesho idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia 1,400. Serikali katika ngazi mbalimbali zimetenga fedha nyingi ili kuyasaidia majumba hayo kutokana na kufunguliwa bure kwa umma.

Hapo kabla baadhi ya majumba ya makumbusho yalikuwa yanaruhusu wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari pamoja na baadhi ya wazee kuingia bila malipo. Mwezi Machi mwaka 2007 mji wa Shenzhen uliopo kusini mwa China, ulikuwa wa kwanza kuruhusu watu kuingia bure kwenye majumba yote ya makumbusho mjini humo, na tarehe 6 Novemba mwaka huo mkoa wa Hubei uliopo katikati ya China pia ulitangaza kuruhusu watu kuingia bure kwenye jumba la makumbusho la mkoa huo. Ndani ya jumba hilo kuna vitu vya kale zaidi ya laki mbili, kati ya vitu hivyo kuna kengele za muziki za kale na upanga uliotumiwa na mfalme Gou Jian wa Dola la Yue lililokuwepo miaka zaidi ya 400 K.K. nchini China. Hatua ya kuruhusu watu kuingia bure kwenye majumba ya makumbusho inaufurahisha umma. Kwenye jumba la makumbusho la mkoa wa Hubei mwandishi wa habari alizungumza na Bw. Zhang Wu aliyekuwa ameambatana na mtoto wake. Bw. Zhang Wu alisema,

"Hapo kabla kiingilio cha jumba hilo kilikuwa Yuan 30, sasa ni bure, tumekuwa na haki sawa na wenye uwezo wa kiuchumi kunufaika na utamaduni wa taifa, nafurahi sana."

Ili kukidhi mahitaji ya umma kunufaika na maliasili ya utamaduni, serikali kuu na serikali za mitaa zilitenga fedha nyingi ili kuhakikisha majumba hayo yanafunguliwa bure kwa umma. Naibu waziri wa utamaduni wa China Bw. Zhou Heping alisema,

"Serikali kuu imetenga Yuan bilioni 1.2 kuyawezesha majumba ya makumbusho nchini China yaruhusu watu kuingia bure kwa nyakati tofauti, na serikali za mitaa pia zilichukua hatua nyingi ili kuboresha huduma zao."

Ili majumba ya makumbusho yaweze kuruhusu watu kuingia bila malipo serikali ya Hubei imetenga Yuan milioni 30 kila mwaka ili kufidia gharama za uendeshaji wa majumba hayo, na serikali ya Beijing pia imetenga Yuan zaidi ya milioni 100 ili kuhakikisha watu wanaweza kutembelea majumba ya makumbusho bila malipo.

Kwa mujibu wa mpango wa serikali ya China, katika mwaka huu na mwaka kesho watu wataweza kuingia kwenye majumba yote ya makumbusho nchini China bila malipo. Naibu mkuu wa Idara Kuu ya Vitu vya Kale ya China Bw. Zhang Bai alisema, kutokana na kuwa watu wanaweza kuingia kwenye majumba ya makumbusho bila malipo huduma za majumba hayo zinatakiwa ziwe bora zaidi kwa sababu watazamaji wamekuwa wengi, na usimamizi wa shughuli na usalama wa majumba hayo pia unatakiwa kuimarishwa zaidi."

Kuanzia tarehe 28 Machi majumba ya makumbusho 29 yaliyo chini ya serikali ya Beijing yalianza kuruhusu watu kuingia bila malipo. Mkuu wa Idara ya Vitu vya Kale ya Beijing Bw. Kong Fangzhi alisema, kutokana na watazamaji kuongezeka kwa kasi kuna haja ya kuwa na mpango wa kukwepa matatizo yanayoweza kutokea. Alisema,

"Kutokana na kuongezeka kwa watazamaji kwa wingi, mazingira ya majumbani yanaweza kuwa mabaya, na pili kutokana na kuwepo kwa watazamaji wengi usalama wao na usalama wa vitu vya kale pia unatia wasiwasi, kwa hiyo tumechukua hatua za kutaka makundi ya watazamaji yalete maombi ili yapangiwe siku za kutembelea, na wasimamizi na walinzi lazima wawepo kwenye majumba ya makumbusho."

Kabla ya kuchukua hatua ya kuruhusu watu kuingia kwenye majumba ya makumbusho bila malipo, Idara ya Vitu vya Kale ya Beijing iliwahi kuwafundisha wafanyakazi wa majumba hayo na imeweka matakwa kuhusu mapokezi, huduma, maelezo na hatua za dharura. Na Majumba yote yametangaza simu za kuomba kupangiwa muda wa kutembelea, watazamaji wanatakiwa kutembelea majumba hayo kwa mujibu wa siku walizopangiwa.

Kwenye Jumba la Makumbusho la Mji Mkuu Beijing mwandishi wa habari alizungumza na mwanafunzi kutoka Uingereza Andrew Paadacides aliyefanya ziara kwenye jumba hilo akiwa na rafiki yake, alikuja siku yake aliyopangiwa kabla. Alisema,

"Naona vizuri sana, hapa zana ni za kisasa na kuna vitu vingi vya kale. Mbele ya kila kitu kuna kibao cha maelezo ya Kiingereza, watu kutoka nchi za Ulaya na sehemu nyingine wanaweza kufahamu utamaduni wa China."

Baada ya majumba ya makumbusho kuruhusu watu kuingia bila malipo, mashirika mengi ya utalii yamepanga ratiba ya kutembelea majumba hayo. Mwongoza watalii wa Sirika la Utalii la Takpo la Hong Kong Bw. Li Guanying alisema, watalii wao wengi ni wanafunzi, kabla ya kuja hapa Beijing shule zao ziliwashauri wanafunzi hao watembelee majumba ya makumbusho, na mpaka sasa wamemaliza kutembelea majumba matatu na wanafurahi. Alisema,

"Niliwaambia kwamba kutembelea majumba ya makumbusho ni kama kutembelea maktaba, muda wa saa mbili tu hautoshi kuangalia kila kitu kilichopo, kwa hiyo wachague kuangalia vitu vinavyowavutia. Huko Hong Kong hakuna majumba makubwa ya makumbusho. Watoto wa kizazi kipya hawafahamu sana historia ya China, wana hamu ya kuifahamu."

Naibu mkuu wa Jumba la Makumbusho la Mji Mkuu Beijing Bw. Han Yong alisema baada ya kufanya uchambuzi kuhusu watazamaji wa Beijing wakafahamu kwamba baadhi ya watazamaji ni wataalamu na wengine ni watazamaji wa kawaida. Sasa majumba hayo yanaruhusu watu kuingia bila malipo, licha ya kuhakikisha usalama, ni lazima kuboresha huduma. Bw. Han Yong alisema,

"Baada ya umma kuruhusiwa kuingia kwenye majumba ya makumbusho bila malipo, namna ya kuwavutia zaidi watazamaji wa kawaida ni suala la kuzingatiwa, yaani tutafanyaje baada ya kipindi fulani watazamaji wakipungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo tunapaswa kuboresha huduma, kuinua kiwango cha maonesho na kufanya shughuli mbalimbali za kuwavutia. Kama mara kwa mara tunabadilisha maonesho na kutangaza shughuli zetu za aina mpya watu wataendelea kuja kwa wingi."

Katika kipindi cha michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, watalii na wanamichezo kutoka nchi za nje hakika watakuwa wengi na watatembelea majumba ya makumbusho kwa madhumuni ya kufahamu utamaduni wa China. Mkuu wa Idara ya Vitu vya Kale ya Beijing Bw. Kong Fanzhi alisema wamejiandaa kuwapokea. Alisema,

"Hatuna wasiwasi kuwa hata watazamaji wa nchini na wa nchi za nje wakitembelea majumba ya makumbusho kwa pamoja, kwa sababu tuna zana za usalama na muhimu zaidi ni kuwa watu hao ni watu wenye mwenendo mzuri."

Kwa mujibu wa takwimu zisizokamilika kutoka Idara ya Taifa ya Vitu vya Kale, baada ya kufungua majumba ya makumbusho idadi ya watazamaji imeongezeka mara tano kuliko hapo kabla. Kuruhusu watu kuingia bila malipo kwenye majumba hayo kumewaletea wananchi uhondo wa utamaduni. Lakini kwenye baadhi ya sehemu majumba ya makumbusho yalikumbwa na tatizo la idadi ya watazamaji kuongezeka hata mara kumi. Kutokana na hewa chafu na joto ndani ya majumba mazingira ya kuhifadhi vitu vya kale yakawa mabaya. Kutokana na hali hiyo majumba hayo yamechukua hatua za kudhibiti idadi ya watazamaji kwa siku ili kuhakikisha usalama wa vitu vya kale.

Idhaa ya kiswahili 2008-04-17