Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-17 20:27:20    
Mwelekeo wa nishati ya viumbe utakuwaje?

cri

Ofisa maalumu wa haki ya lishe bora wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jean Ziegler, hivi karibuni alitoa kauli ambayo inafanya suala la nishati ya viumbe kufuatiliwa na watu wengi. Alisema kuendeleza uzalishaji wa petroli ya ethanol ni "uhalifu kwa binadamu", hata alitoa wito wa kutaka Umoja wa Ulaya uache lengo la kuinua kiwango cha matumizi ya petroli ya ethanol hadi 10% ifikapo mwaka 2020. Wakati huo huo, Ufaransa pia ilitoa pendekezo la kuweka kizuizi kwa uagizaji wa ethanol, ikiona kuwa nishati ya ethanol ni chanzo cha kuongezeka kwa bei za nafaka. Brazil, ambayo ni nchi iliyotangulia duniani kuendeleza nishati ya viumbe, haikubaliani na kauli hiyo. Waziri wa kilimo wa Brazil alipozungumzia kauli ya Bw. Jean Ziegler alisema, Brazil imeendeleza nishati ya viumbe kwa miaka 30, lakini bei za nafaka nchini Brazil hazikupanda hata kidogo kutokana na jambo hilo.

Toka zamani Brazil ina upungufu mkubwa wa raslimali za mafuta ya asili ya petroli, ili iweze kujitosheleza kwa nishati, serikali ya Brazil imeharakisha utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza nishati mbadala, hususan nishati ya ethanol. Hivi sasa karibu magari yote ya nchini Brazil yanaweza kutumia nishati ya alcohol, toka mwezi Julai mwaka uliopita, serikali ya Brazil ilitangaza kuongeza kiwango cha matumizi ya alcohol hadi 25% kutoka 2% hadi 5% ya matumizi ya petroli iliyotangazwa mwaka 1931.

Katika hali ya kupanda kwa kiasi kikubwa kwa bei ya petroli na kuongezeka joto kwa dunia, uendelezaji wa nishati ya viumbe unachukuliwa kuwa ni mpango mzuri wa kupunguza wasiwasi wa upungufu wa nishati duniani na kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini baadhi ya watu wanapinga, wakisema, nishati ya viumbe siyo ya "kijani" sana kama inavyodhaniwa, katika uzalishaji wa nishati ya viumbe, mazao ya mahindi na miwa, ambayo ni mali-ghafi yake, yanahitaji ardhi kubwa, wakati mwingine misitu inakatwa ili kupata mashamba mengi zaidi, hatua, ambayo inaharibu aina nyingi za viumbe, tena wakati wa kufyeka mashamba na kuchoma moto misitu, hewa nyingi ya carbon dioxide inatolewa. Wakosoaji pia walisema, nishati ya viumbe ni kama kunyang'anya nafaka kutoka mezani mwa watu na kuziweka katika matanki ya magari, na kusababisha njaa na umaskini. Kiongozi wa zamani wa Cuba, Bw. Castro alishutumu vikali, kutosheleza mahitaji ya magari kwa miwa mingi, jambo hilo huenda litasababisha upungufu mkubwa wa nafaka duniani, na watu kukumbwa na maafa ya njaa.

Pamoja na kupanda kwa bei za nafaka duniani, nishati ya viumbe inazidi kuwa shabaha inayoshambuliwa. Watu wengi wanasema, mazao mengi ya kilimo yakiwemo mahindi yanatumiwa kuzalisha nishati, jambo hilo limesababisha upungufu wa nafaka na kupanda kwa kiasi kikubwa kwa bei za nafaka. Kuna watu wengine wanaounga mkono uzalishaji wa nishati ya viumbe, mkuu wa Benki ya Dunia, Bw. Robert Zoellick amesema, nishati ya viumbe ya nchini Brazil haikusababisha kupanda kwa bei za nafaka. Watu wa sekta mbalimbali za nchini Brazil wanaamini kuwa nishati ya viumbe ni njia yenye ufanisi ya kupunguza wasiwasi wa upungufu wa nishati na kuboresha mazingira. Bei kubwa za nafaka za hivi sasa zimesababishwa na ongezeko la mahitaji ya nafaka ya duniani.

Ni kweli kuwa uzalishaji wa nishati ya viumbe una matatizo mengi, na yanapaswa kuzingatiwa. Hivi sasa kuna malumbano kuhusu athari zinazoletwa na nishati ya viumbe kwa mazingira ya utoshelezaji wa matumizi ya nafaka, lakini ni mwafaka kwa nchi zote zivumbue nishati mpya kutokana na hali yake halisi, nishati ya viumbe huenda ni moja tu ya njia mbadala ya nishati ya petroli.