Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-21 14:59:23    
Mtaa mmoja wenye mikahawa inayouza aina mbalimbali za chakula kitamu

cri
Mkoa wa Qinghai uko kwenye sehemu ya kaskazini magharibi ya China, na unajulikana kutokana na kuwa na mandhari nzuri ya maumbile. Leo tunawafahamisha kuhusu mtaa mmoja wenye mikahawa inayouza aina mbalimbali za chakula kitamu, ulioko katika mji wa Xining, mji mkuu wa mkoa wa Qinghai, pamoja na utamaduni wa chakula wa uwanda wa juu.

Mtaa huo uko kwenye sehemu ya mashariki ya mji wa Xining, kwenye kando mbili za mtaa huo mdogo wenye upana wa mita 10, vimejengwa vibanda vingi vya chuma vilivyofunikwa kwa maturubai meupe, ingawa vibanda hivyo vinaonekana ni vya kawaida, lakini vinauza karibu aina zote za chakula chepesi chenye umaalumu wa mkoa wa Qinghai. Kila siku jioni, mtaa huo hujaa wateja wanaokuja kula chakula cha kipekee cha uwanda wa juu wa Qinghai.

Katika mkoa wa Qinghai, wanaume kwa wanawake, na wazee kwa watoto wote wanapenda sana kula aina ya chakula cha Niangpi, ambacho ni chakula chenye umaalumu mkubwa wa Qinghai. Chakula cha Niangpi kimegawanyika katika aina mbili kutokana na rangi zake, hivyo kuna Niangpi nyeupe na Niangpi nyeusi, Niangpi inatengenezwa kwa unga wa ngano, na kuchanganywa aina kadhaa za viungo vya vitoweo. Kijana wa kabila la wahui anayeuza Niangpi kwenye mtaa huo wa chakula, Bw. Mu Hai alisema, kwa kawaida, Niangpi inatengenezwa kwa mvuke.

"Baada ya Niangpi kuivishwa kwa mvuke, inabanguliwa kwenye sahani kubwa, baada ya Niangpi kupoa, inakatwa kama mikanda miembamba mirefu, kisha inatiwa siki, mafuta yenye pilipili, mustard, leek na vitungu saumu vilivyopondwa, chakula hicho ingawa ni kikali, lakini ni baridi kidogo na chenye ladha nzuri."

Bw. Mu Hai alisema, kuna njia mbili za kutengeneza Niangpi. Niangpi iliyotengenezwa kwa kukaangwa, ni yenye rangi ya manjano na mwanga, Niangpi ya aina hiyo inapasuka-pasuka wakati inapotafunwa; Niangpi iliyotengenezwa kwa mvuke ni nene kidogo, ingawa aina hizi mbili za Niangpi zina rangi na kuonekana tofauti, lakini ladha zake karibu ni za namna moja. Ingawa Niangpi ni chakula chepesi, lakini pia kinaweza kutumiwa kama chakula kikuu cha kuondoa njaa, tena kinaweza kutumiwa kama kitoweo. Niangpi inaweza kutumiwa katika majira yote ya mwaka.

Tambi zinazopikwa pamoja na utumbo wa kondoo ni chakula kingine chepesi chenye umaalumu wa mji wa Xining. Chakula hiki ni chenye utumbo mwingi wa kondoo ukichanganywa na tambi kidogo zilizochemshwa. Chakula hicho hutengenezwa kwanza kwa kusafisha utumbo wa kondoo, halafu kutia vitungu vya kijani, vipande vya tangawizi iliyokatwakatwa, zanthoxylum, chumvi na unga wa viazi, kisha kufunga midomo ya utumbo kwa nyuzi, na kuchemshwa katika maji moto. Baada ya hapo vinatiwa vipande vidogo vya karoti, vitungu vya kijani na vitungu saumu katika sufuria inayochemsha utumbo wa kondoo. Wakati wa kula, utumbo wa kondoo na tambi zilizochemshwa vinatiwa kwenye supu ya utumbo. Tambi zenye utumbo zilizotiwa kwenye supu, ni yenye rangi ya manjano mepesi, bei yake ni rahisi lakini ni tamu sana.

Kwenye kibanda kinachouza tambi zenye utumbo, wateja hujaa, ambao wanasimama wakichukua bakuli kubwa mikononi. Mtalii kutoka mji wa Tianjin, Bw. Zhao Hailiang alikuwa akisifu sana tambi zilizotiwa katika bakuli kubwa alilokuwa amelishika mkononi. Alisema,

"Nilifika Xining siku tatu zilizopita, kila siku ninakuja kula tambi hizo, tena kila mara ninakula mabakuli mawili ya tambi. Nimetembelea sehemu nyingi za nchini, lakini sikuwahi kula tambi tamu kama za hapa. Sijui walitia viungo gani katika supu, tambi ni tamu sana baada ya kutiwa katika supu ya utumbo. Utumbo pia ni mtamu sana, mimi sikuona kama utumbo una mafuta mengi, ninajua nikirudi nyumbani sitapata tena chakula hicho, hii inanisikitisha."

Licha ya Niangpi na tambi za matumbo, mkoani Qinghai kuna aina nyingine ya chakula chepesi, ambacho ni maarufu kuliko aina zote nyingine, chakula hicho ni nyama ya kondoo inayoitwa 'shouzhua yangrou'. Nyama ya kondoo wa mkoa wa Qinghai ni maarufu sana kutokana na kuwa na ladha nzuri, hivyo inapendwa sana na watu wengi. Wakazi wa makabila mbalimbali wa mkoani Qinghai, wawe wa makabila ya wahui, wahan au wamongolia, wote wanachukulia 'shouzhua yangrou' kuwa ni chakula kizuri zaidi cha kukirimu wageni. Katika miaka ya hivi karibuni, pamoja na maendeleo ya utalii ya mkoani Qinghai, chakula hicho kinachukuliwa kuwa moja ya vitoweo maarufu vya Qinghai katika mahoteli makubwa na mikahawa ya huko.

Wakazi wa mji wa Xining wanajali sana viungo vinavyotumiwa katika mapishi ya nyama ya kondoo. Kabla ya kula nyama ya kondoo, huwa wanakunywa kikombe kimoja cha chai ya "lao cha". Chai ya "lao cha" inapikwa kwa kutumia chai ya mchele kutoka mkoa wa Yunnan, na kuchangwa na chumvi na zanthoxylum, chai ya aina hiyo inasaidia kuyeyusha chakula na kuondoa ladha ya mafuta mengi. Pili, wakati wa kula nyama ya kondoo, ni vizuri kula vitungu saumu ya huo vya rangi ya zambarau. Ili kula vizuri 'shouzhua yangrou' inatakiwa kuongeza mchanganyiko wa pilipili wa huko. Kiungo hicho siyo pilipili peke yake, bali ni mchanganiko wa pilipili, vitungu saumu vilivyopondwa, zanthoxylum, vipande vidogo vidogo vya tangawizi, mafuta ya saladi na unga wa matunda ya nyasi (grass fruit).

Baada ya kula 'shouzhua yangrou', yaani kula nyama ya kondoo kwa mikono unaweza kujaribu mtindi wa Qinghai. Mwanamke mmoja wa kabila la wahui aliyekuwa anauza mtindi, ambaye alivaa baibui, huku akiwahudumia wateja wake, mtindi mweupe uliotiwa katika mabakuli na kufunikwa kwa kifuniko kikubwa cha kioo, ulikuwa unapendeza sana.

Mtindi ni chakula maalumu kilichotengenezwa kwa maziwa kwenye uwanda wa juu wa Qinghai. Katika sehemu za kilimo na ufugaji mifugo, wakazi wana desturi ya kula mtindi, hususan wakazi wa kabila la wahui, wanatengeneza mtindi kwa kutumia maziwa ya ng'ombe, na kutia matone kadhaa ya mafuta ya mboga (Vegetable oil). Mwendeshaji wa duka moja la mtindi, Bi. Ma Lihua alisema,

"mtindi una vitamini nyingi zaidi kuliko maziwa. Mtindi ni chakula kinachofanya kazi za aina mbili za chakula na kuimarisha afya. Mtindi unaouzwa katika sehemu nyingine siyo safi kama wa hapa kwetu, mtindi wetu ni mbichi unaotengenezwa kila siku, wala siyo kama ule unaotiwa kwenye makopo ukichanganywa na vitu vingine vya kikemikali."

Idhaa ya kiswahili 2008-04-21