Mkutano wa Baraza la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa umefunguliwa tarehe 20 huko Accra, mji mkuu wa Ghana. Ufunguzi wa mkutano huo wa siku 6 umehudhuriwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon, rais John Kufuor wa Ghana, rais Luiz Lula da Silva wa Brazil na wajumbe kutoka nchi wanachama 192 wa baraza hilo.
Ajenda kuu ya mkutano huo ni "nafasi na changamoto zinazoletwa na utandawazi wa uchumi duniani", hata hivyo kutokana na hali ilivyo sasa ya kupanda kwa kiasi kikubwa kwa bei za chakula duniani, jinsi ya kuhakikisha usalama wa nafaka na kudhibiti bei za chakula limekuwa ni suala linalofuatiliwa sana kwenye mkutano huo. Katika hotuba za Bw. Ban Ki-Moon, rais John Kufuor na rais Lula da Silva, wote walitaja masuala ya chakula na kilimo. Na Bw. Ban Ki-Moon alisisitiza kuwa, suala la chakula linapaswa kutatuliwa mara moja, na yeye atateua kundi la wataalamu ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha miezi 6 iliyopita, bei za mazao muhimu ya kilimo ikiwemo ngano na mahindi zilipanda kwa asilimia 50, huku bei ya mchele ilipanda sana na kuweka rekodi mpya. Kupanda kwa bei za chakula si kama tu kumeathiri vibaya maisha ya watu duniani, bali pia kumeanza kusababisha kutokea kwa maandamano na vurugu nchini Misri, Haiti, Cote D'ivoire na Burkina Faso. Kuna dalili kwamba, iwapo suala la kupanda kwa bei za chakula litashindwa kutatuliwa upasavyo, maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi nyingi yataathirika, hata utulivu wa kisiasa. Wajumbe wanaohudhuria mkutano huo walitaja sababu kuu zilizosababisha kupanda kwa bei za chakula duniani kuwa ni pamoja na, mabadiliko ya hali ya hewa, kupanda kwa bei za nishati na uzalishaji wa nishati ya viumbe kwa kutumia nafaka. Mbali na hayo mambo mengine pia yamechangia kutokea kwa msukosuko wa nafaka, mambo hayo ni pamoja na utandawazi wa viwanda katika nchi za kilimo, pengo linalopanuka katika sekta ya kilimo kati ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea, na kupungua kwa misaada ya kilimo duniani.
Kwenye mkutano huo Bw. Ban Ki-Moon alisema ni lazima hatua za dharura zichukuliwe ili kuhakikisha chakula kinapatikana bila matatizo, na hatua ya kwanza ni kuongeza misaada ya kibinadamu. Kwa kutekeleza mpango wa Umoja wa Mataifa, kutakuwa na uwezekano wa kukidhi mahitaji ya kimsingi ya chakula kwa watu wapatao milioni 73 kutoka nchi 80, lakini kutokana na kupanda kwa bei za chakula, inapaswa kuzidi kugharamia dola za kimarekani bilioni 75 ili kutimiza lengo hilo. Bw. Ban Ki-Moon alisema kwa mtizamo wa mbali, jambo muhimu zaidi katika ufumbuzi wa suala la chakula ni kuimarika kwa uzalishaji wa kilimo.
Lakini uzalishaji wa kilimo pia unaathiriwa na upungufu wa fedha, na hali hii ni mbaya zaidi katika nchi zilizo nyuma kimaendeleo. Hivi sasa katika nchi maskini zilizoko kusini mwa Sahara, ni asilimia 1 tu ya misaada ya kimataifa inatumika katika uzalishaji wa chakula. Siku moja kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo, katibu mkuu wa Baraza la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa Bw. Supachai Panitchpakdi alitoa wito kwa serikali za nchi mbalimbali zizidi kutenga fedha kwa ajili ya sekta ya kilimo, na alizihimiza nchi zilizoendelea ziongeze misaada ya kilimo kwa nchi maskini.
Rais Lula da Silva wa Brazil kwenye mkutano huo alizihimiza nchi zilizoendelea zitoe teknolojia za kilimo kwa nchi zinazoendelea. Na wajumbe wengi wa mkutano huo walikubaliana kuwa, inafaa baraza hilo, benki ya dunia na mfuko wa fedha duniani zianzishe utaratibu wa kuhakikisha chakula kinatolewa vya kutosha kwa nchi zinazohitaji chakula.
|