Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-22 11:10:41    
Meneja mkuu wa kampuni ya magari ya FAW-VW kutoka Ujerumani Bw. Dieter Maschgan

cri

   

Kampuni ya FAW-VW ni kampuni kubwa ya utengenezaji wa magari yenye mitaji ya kiwanda cha FAW cha China, kiwanda cha Volkswagen na kiwanda cha Audi cha Ujerumani. Mwaka 2005 Bw. Maschgan alikuja kufanya kazi nchini China kwa mara ya nne, akiwa ni mwakilishi wa kampuni ya Volkswagen ya Ujerumani na meneja mkuu wa upande wa Ujerumani wa kampuni ya magari ya FAW-VW. Kwenye kiwanda cha magari cha kampuni ya FAW-VW mjini Changchu, mwandishi wetu wa habari alikutana na meneja mwandamizi wa kampuni ya magari ya FAW-VW kutoka Ujerumani Bw. Dieter Maschgan. Bw. Maschgan alisema,

"Jina langu ni Dieter Maschgan, nina umri wa miaka 52, na nina watoto wawili. Katika miaka 27 iliyopita, nilianza kufanya kazi katika kampuni ya Volkswagen, na nimefanya kazi nchini China kwa miaka 12."

Bw. Maschgan alisema alizaliwa mjini Berlin, na anapenda magari tangu akiwa mtoto. Wakati wenzake walipokuwa wanacheza, yeye alipenda kusoma magazeti yanayohusu magari. Siku zote alifanya juhudi ili kutimiza lengo lake. Mwaka 1980 alianza kufanya kazi kwenye kiwanda cha magari cha Volkswagen, na mwaka 1988 alikuja China akiwa ni mwakilishi wa kampuni ya Volkswagen. Alisema,

"kwa mara ya kwanza nilikuja China mwaka 1988, na nilifanya kazi katika kiwanda cha magari cha Shanghai-VW kwa miaka mitatu. Wakati huo ulikuwa muda mfupi baada ya kiongozi wa China Bw. Deng Xiaoping kutoa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, hivyo kazi zote zilikuwa kwenye hatua ya awali, na kazi mjini Shanghai zilikuwa chache."

Baadaye Bw. Maschgan alifanya kazi nchini China mara nyingi, na alifanya kazi mjini Changchun kwa muda mrefu. Alipozungumzia mabadiliko yaliyotokea mjini humo katika miaka ya hivi karibuni, alisema,

"Mabadiliko makubwa yametokea mjini Changchun katika miaka ya karibuni, eneo la maendeleo ya uchumi la hapa limepata maendeleo ya kasi, na majengo mpya yamejengwa. Viwanda vimeendelezwa mjini humo, na vitaendelea kupata maendeleo.

Licha ya maendeleo makubwa ya viwanda, kuhusu michezo ya 6 ya majira ya baridi ya Asia iliyofanyika mwaka jana na maonesho ya bidhaa ya Asia ya Kaskazini Mashariki yanayofanyika kila mwaka mjini humo, Bw. Maschgan alisema,

"Shughuli hizo zimeonesha kuwa si kama tu mji wa Changchun unapiga hatua kubwa katika maendeleo ya viwanda, bali pia umekuwa mji mashuhuri wa utalii duniani. Wakati michezo ya majira ya baridi ya Asia ilipofanyika, nilitambua kuwa utaratibu wa barabarani na madukani ni mzuri, wageni wengi walikaa mahotelini, hivyo naona kuwa mji huo umekuwa mji mashuhuri duniani."

Kama ilivyo kwa wageni wengine, Bw. Maschgan alikabiliwa na matatizo mengi kutokana na tatizo la lugha. Marafiki na wenzake wa China walimpatia msaada, ambao walimfanya ajione kuwa kama yuko nyumbani. Ili kumsaidia Bw. Maschgan kufanya kazi kwa mafanikio, kampuni ya FAW-VW ilimpatia mtafsiri ili aweze kushughulikia teknolojia na kazi ya kupanga wafanyakazi bila ya matatizo. Bw. Maschgan alisema,

"Ninapofanya kazi katika kampuni ya FAW-VW, najiona kama niko nyumbani. Watu wengi wananisaidia ili kuondoa matatizo ya lugha. Nikisaidiwa na watu wengine, nimefanikiwa kutatua matatizo yaliyosababishwa na tofauti ya utamaduni na njia ya kufikiri kati Wajerumani na Wachina. Najiona kama niko nyumbani."

Akiwa ni meneja mwandamizi wa ofisi ya mpango ya kampuni hiyo, Bw. Maschgan ana maoni ya kipekee kuhusu kazi ya kupanga wafanyakazi. Kutokana na kuwa kampuni hiyo ina mitaji kutoka viwanda mbalimbali, kusawazisha kazi za wafanyakazi wa China na wafanyakazi wa nchi za nje ni suala linalofikiriwa na Bw. Maschgan siku zote. Alisema,

"China ilianza kujifunza teknolojia mbalimbali na kupata maendeleo baada ya kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango katika miaka ya 70 karne iliyopita. Upande wa Ujerumani unaweza kutoa teknolojia za kisasa, lakini moyo wa kufanya kazi kwa makini walio nao wafanyakazi wa China ni muhimu zaidi."

Kampuni ya FAW-VW ilipoanzishwa mwaka 1992, iliweza kutengeneza magari elfu 8 tu kwa mwaka, na wafanyakazi walikuwa wachache sana. Hadi mwaka 2007 kampuni hiyo ilikuwa na uwezo wa kutengeneza magari karibu laki 4.9 kwa mwaka. Bw. Maschgan alisema hayo ni maendeleo makubwa, ambayo yalipatikana kutokana na juhudi za wasimamizi wa Ujerumani na Wachina. Wafanyakazi wa kampuni hiyo wanajifunza na kujiendeleza kwenye kazi zao. Bw. Maschgan alisema mkakati wa kuwaandalia wataalamu ni kazi muhimu ya maendeleo ya kampuni yake, ambao haulengi kuandaa mtu mashuhuri kama mchezaji Yao Ming, bali unalenga kuandaa timu yenye wataalamu hodari wa magari. Alisema,

"Mwaka 2007 tuliajiri wanafunzi wengi waliohitimu kutoka vyuo vikuu, lakini hawakuwa na uzoefu wa kazi. Hivyo tutawapatia mafunzo mbalimbali ili wajue njia ya kufanya kazi na kuinua uwezo halisi. Hii ni kazi yetu muhimu katika mwaka 2008. Na katika siku za usoni, tutatafiti magari ya aina mpya, hivyo tunatakiwa kuwasaidia wafanyakazi wetu wawe na ujuzi kuhusu mambo ya magari."

Mwaka 1996, kampuni ya FAW-VW ilitoa kauli mbiu ya "kutoa kipaumbele kwa sifa ya bidhaa" kati ya makampuni mbalimbali ya magari. Baada ya miaka zaidi ya kumi, kampuni hiyo imepata maendeleo katika mauzo ya magari, teknolojia na usimamizi. Hivi sasa "kutoa kipaumbele kwa sifa ya bidhaa" kumekuwa utamaduni wa kampuni hiyo. Bw. Maschgan alipozungumzia maendeleo ya kampuni hiyo katika siku za usoni, alisema,

"Nina matumaini kuwa kampuni ya FAW ya China, kampuni ya Volkswagen na kampuni ya Audi zitaendelea kushirikiana. Tangu kampuni ya FAW-VW iundwe mwaka 1992, makampuni hayo matatu yalishirikiana kwenye shughuli mbalimbali. Mwanzoni yalishughulikia utengenezaji wa magari na injini, baadaye yalishughulikia utengenzaji wa gia boksi, na baadaye kampuni ya Volkswagen na kampuni ya kwanza ya magari ya China yalianzisha viwanda vya injini huko Dalai. Hivi sasa tunajaribu kufanya utafiti ili kutengeneza magari ya aina mpya kwa ushirikiano kati ya makampuni hayo mawili, na tunajaribu kuuza bidhaa mpya kabla ya michezo ya Olimpiki ya Beijing."