Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-22 18:16:23    
Kutatua masuala ya nishati kutasaidia maendeleo endelevu duniani

cri

Baraza la nishati la kimataifa lilifunguliwa tarehe 20 huko Rome, nchini Italia, ambapo wawakilishi wa serikali za nchi zaidi ya 70, maofisa wa mashirika ya kimataifa na viongozi wa makampuni makubwa ya nishati walihudhuria baraza hilo. Na masuala ya usalama wa nishati na mabadiliko ya hali ya hewa yalizungumzwa zaidi kwenye baraza hilo.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya kiuchumi na ya kijamii Bw. Sha Zukang, alihudhuria baraza hilo akimwakilisha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kwenye baraza hilo, Bw. Sha Zukang alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema 

"Suala la nishati na suala la mabadiliko ya hali ya hewa, yote ni sehemu ya suala la maendeleo endelevu. Suala la nishati ni muhimu sana katika kutimiza malengo ya milenia, na jinsi ya kushughulikia suala hilo kunahusiana moja kwa moja na kama malengo ya milenia yatatimizwa au la."

Lengo la kwanza kwenye malengo ya milenia yaliyotolewa mwaka 2000 kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa ni kuondokana na hali mbaya ya umaskini na njaa. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, baadhi ya nchi zimeanza kutumia nishati ya kiumbe badala ya mafuta. Baadhi ya mashirika ya kimataifa na wataalamu wanaona, hatua hiyo ni sababu muhimu ya kupanda juu kwa bei za chakula kwa hivi sasa. Kuhusu maoni hayo, Bw. Sha Zukang alisema

"Nchi kadhaa duniani zimefanya vizuri katika utafiti, uzalishaji na matumizi ya nishati ya kiumbe, ambayo kusema kweli inasaidia kupunguza tatizo la nishati. Hata hivyo tukiangalia hali ya dunia nzima, tunaona uzalishaji wa nishati ya kiumbe unahitaji maji, ardhi na nguvu kazi. Kwa hiyo nakubali kuwa nishati ya kiumbe ni njia moja ya kuondoa upungufu wa nishati, lakini pia inaleta athari mbaya katika uzalishaji wa nafaka, pamoja na maendeleo endelevu ya mazingira na jamii. Zaidi ya hayo kwa namna moja au nyingine, inachangia kufanya msukosuko wa chakula uwe mbaya zaidi."

Ofisa huyo amesisitiza kuwa, majadiliano kuhusu nishati ya kiumbe bado yanaendelea, lakini kanuni ni kuwa lazima matumizi ya nishati ya kiumbe yasaidie kutimizwa kwa malengo ya milenia. Na kuhusu utatuzi wa suala la mabadiliko ya hali ya hewa, Bw. Sha Zukang alieleza kanuni mbili zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa. Alisema

"Ni lazima suala la mabadiliko ya hali ya hewa lishughulikiwe kwa kufuata kanuni ya "kubeba wajibu tofauti kwa pamoja" iliyokubalika kwenye jumuiya ya kimataifa. Yaani suala hilo linahusiana na maslahi ya binadamu, tuna maslahi ya pamoja kwenye suala hilo, kwa hiyo nchi zote, nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea zinapaswa kutoa mchango, na kuchukua wajibu tofauti, kwani hali halisi ni kwamba, nchi mbalimbali zina uwezo tofauti, kwa hiyo zinatakiwa kuchukua wajibu na majukumu tofauti."

Bw. Sha Zukang alitaja kanuni nyingine ni kushughulikia suala la mabadiliko ya hali ya hewa kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu. Alisema

"Maendeleo endelevu yanazihusu nchi zote, hususan nchi zinazoendelea, ambazo zinakabiliwa na kazi muhimu ya kuondokana na umaskini, kuwalisha wananchi, kupunguza magonjwa, kuwasomesha watoto, kuwapa wananchi huduma za afya na makazi, na masuala hayo yanahusiana na maisha. Ni muhimu zaidi kwa nchi zinazoendelea kupata maendeleo."