Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-22 20:42:22    
Barua 0422

cri

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai United Arab Emirates ametuandikia barau akisema, akiwa ni kizazi cha Baba Mtanzania na Mama Mu-oman ni fahari yake kubwa kuona kwamba mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Mwaka huu ya mjini Beijing China umeweza kupokelewa na kukimbizwa kwa shangwe, vigerere, furaha na nderemo kubwa katika taifa lake la Tanzania na taifa la mama yake yaani Oman katikati ya mwezi April mwaka huu.

Anasema yeye binafsi anajivunia mno kuona kwamba Tanzania na Oman zimeonesha uungaji mkono wao mkubwa kwa Jamhuri ya Watu wa China katika kufanikisha mbio za mwenge huo kabla ya ufunguzi wa tamasha kubwa kabisa la Michezo ya Olimpiki mjini Beijing ifikapo tarehe 8 August mwaka huu. Bila shaka kwa maoni yake binafsi, huu ni ushahidi kwa walimwengu juu ya kushindwa kwa baadhi ya makundi ya watu wachache wanaojaribu kutaka kuipaka matope michezo hiyo kwa kuchochea mandamano na fujo zisizokuwa za lazima juu ya swala la kisiasa Mkoani Tibet.

Anasema Watanzania na Wa-omani wote wako pamoja bega kwa bega na ndugu wa Jamhuri ya Watu wa China ili kuhakikisha Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka huu inaweza kufanikiwa vyema na kuwaunganisha walimwengu wote kwa ujumla chini ya kauli mbiu "Dunia moja, ndoto moja ".

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Mbarouk Msabah kwa barua yake ya kueleza maoni kuhusu mbio za kukimbiza kwa kupokezana mwenge wa Michezo ya Olimpiki huko Dar es Salaam Tanania na nchini Oman. Kweli kutokana na habari zilizoripotiwa kuhusu mbio hizo huko huko Dar es Salaam na nchini Oman wachina wengi wameona hisia za dhati za urafiki walizonazo watu wa Afrika kwa wananchi wa China, ambao wanachukua Michezo ya Olimpiki ya Beijing kuwa ni Michezo yao wenyewe, wanafurahia na kupokezana kwa shagwe mwenge wa Michezo ya Olimpiki, hali ambayo imetutia moyo sana.

Msikilizaji wetu Laurent Mweli wa sanduku la posta 7 Tarime Mara nchini Tanzania ametuletea barua akisema, hali halisi ya Michezo ya Olimpiki inaelezeka wazi, kwani michezo hii inawezesha nchi mbalimbali kushiriki pamoja katika michezo ya Olimpiki, hivyo michezo ya Olimpiki ni muhimu sana. Michezo hii ya Olimpiki imekuwa ikifuata historia yake na michezo ya haki, hivyo imekuwa ikihitaji ufanisi mkubwa na uwezo wa kifedha ili iweze kufanikiwa.Msikilizaji wetu huyu anatoa pongezi kwa waandaji michezo ya Olimpiki iliyopita na pia anatoa pongezi nyingi kwa mji wa Beijing kwa kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki kwa mwaka huu wa 2008. Pia anasema anategemea kuwa michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka huu itakuwa tofauti na michezo iliyopita na itakuwa na msisimko wa aina yake, kwani anaamini kuwa watu wa China wako mstari wa mbele kushirikiana katika kuimarisha amani na usalama wakati wa michezo ya Olimpiki.

Bw.Laurent pia anasema ni matumaini yake kuwa viwanja na majumba ya kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya beijing yako safi na tayari kwa ajili ya mashindano, kwa hakika michezo ya Olimpiki ya Beijing itaimarisha upendo na mshikamano baina ya mataifa mbalimbali. Ushauri wake ni kuwa waandaji wa michezo hii wazidi kuiboresha zaidi ili michezo hii iweze kupendwa duniani zaidi kama vile mashindano ya kombe la dunia ya mpira wa miguu. Mwisho anaitakia Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa uandaaji mwema wa vipindi na matangazo, na anaipongeza sana kwa kuwapa nafasi wasikilizaji nafasi ya kuchangia maoni na kushiriki kwenye chemsha bongo.

Tunamshukuru kwa dhati Bw. Laurent Mweli kwa barua yake ya kueleza maoni yake kwa maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, tunafurahia usikivu wake mzuri kwa matangazo yetu, hivi sasa Michezo ya Olimpiki ya Beijing inatukaribia siku hadi siku, tunaposikia maneno yote ya wasikilizaji wetu kwa kuunga mkono Michezo ya Olimpiki ya Beijing tunafurahi kweli. Asante sana.

Msikilizaji wetu Peris Lily Shipenzi anayetunziwa barua zake na Mbarak Mohamed Abucheri, S.L.P. 792 Kakamega nchini kenya anaanza barua yake kwa kutoa salamu nyingi kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya radio China Kimataifa, ni matumaini yake kuwa wote ni wazima na tunaendelea kuchapa kazi ya kuwahudumia wasikilizaji kwa vipindi vizuri vinavyoelimisha, kufahamisha na kuburudisha

Msikilizaji wetu huyo anaendelea kusema kuwa yeye ni buheri wa afya akiendelea na shughuli za ujenzi wa taifa bila kusahau kuitegea sikio Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa. Anasema anapenda kuchukua nafasi hii adimu kutoa shukrani zake na pongezi kwa uongozi wa Radio China kimataifa na watangazaji wote kwa kazi nzuri na anawatakia wote kila la kheri na baraka katika mwaka huu wa 2008.

Vilevile anapenda kufahamisha kuwa amebadilisha anuani yake ya posta na kwa sasa anatumia anuani aliyotutajia hapo mwanzo, Hivyo anaiomba idhaa ya kiswahili ya CRI iwasiliane naye kupitia anuani hiyo hapo juu. Pia anachukua nafasi kuomba atumiwe majarida ya China Today na China pictorial, kalenda ya mwaka 2008 na zawadi mbalimbali ili aweze kufahamu na kujifunza mambo na tamaduni mbalimbali za China. Anapenda pia tusisahau kumtumia kadi za salamu ili aweze kuwasiliana na wasikilizaji wenzake duniani kupitia kipindi cha salamu zenu. Mwisho anaomba kuwasilimu Mama Jesca Meta, Dada Phoebe Muwala, Dada Miriam Akatro na Shemeji Zebedayo Muwala wote hao wakiwa Kakamega kaskazini, Mtoto Rufaida Mbarak akiwa Kakamega Kusini, na anawataka wote washirikiane kupitia redio China Kimataifa

Msikilizaji wetu Philip Machuki wa kijiji cha Nyankware, S.L.P 676 Kisii nchini Kenya anaanza barua yake kwa kutoa salaam nyingi kutoka kwake akitaraji kuwa wafanyakzi wote wa Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ni wazima. Awali ya yote anaomba msamaha kwa kutoandika barua kwa muda mrefu sasa, haikuwa nia yake bali ni kutokana na na shughuli za kila siku. Ila pia anafurahi sana kupokea barua kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa iliyokuwa na zawadi mbalimbali, na juu ya zawadi hizo kulikuwa na jarida alipendalo la China Today, anatoa shukuruani nyingi sana kwa Radio China Kimataifa.

Bw. Machuki anaendelea kusema kuwa anafurahishwa sana na idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kuwakumbuka wasikilizaji wake na mara kwa mara na kuwatumia majarida, zawadi na kubwa zaidi kusoma barua na salamu zao hewani kila siku.Yeye ni mmoja wa wasikilizaji wa vituo vingi vya kimataifa, lakini idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ndio hutoa muda zaidi kwa wasikilizaji wake kutoa maoni yao na kutuma salamu kwa ndugu na marafiki zao, pia anatoa pongezi kwa zawadi mbalimbali na hasa zinazotokana na chemsha bongo, ingawa yeye binafsi hajawahi kushinda kwenye chemsha bongo, lakini hataacha kuiskiliza radio china kimataifa kwani anafahamu vyema kwamba siku moja atapata fursa ya kuitembelea China ama kutunikiwa zawadi maalum. Anapenda kumpongeza Mama Cheni kwa ziara yake aliyoifanya Kisii na ni matumaini yake kuwa amegundua kuwa hakuna sehemu yoyote ile ambayo ina wasikilizaji wengi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa kama Kisii. Anamalizia barua yake kwa kutoa shukrani kumuomba Mungu aendelee kuibariki Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru sana kwa Bw. Philip Machuki kwa barua yake ya kueleza maoni yake juu ya Radio China Kimataifa na vipindi vyake. Kweli tumeona kuwa kutokana na juhudi zao zisizolegalega, wasikilizaji wetu huko Kisii Kenya wamekuwa wengi zaidi, ambao kila mara wametuletea barua kutoa maoni na mapendekezo yao kwa matangazo yetu. Tunafurahi sana bado wanakumbuka ziara yetu huko Kisii, ni matumaini yetu kuwa, tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu ili kuchangia uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Kenya na kati ya China na Afrika.

Msikilizaji wetu Yaaqub Saidi Idambira anayetunziwa barua zake na msikiti wa Jamia kakamega, S.L.P 124 Kakamega nchini Kenya, anaanza barua yake kwa kutoa mkono wa salamu na baraka kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, ni matumaini yake wote ni wazima tukiendelea kuchapa kazi ya kuwahudumia wasikilizaji kwa matangazo na vipindi vya moja kwa moja toka Radio China Kiamtaifa. Anasema yeye ni buheri wa afya akiendelea na shughuliza ujenzi wa taifa bila kusahau kutegea sikio matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China.

Anasema anachukua fursa hii kutoa pongezi kwa serikali ya Jamhuri ya watu wa China kupitia idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa wakati huu wanapoadhimisha ushirikiano kati ya taifa la China na Bara la Afrika katika nyanja ya bishara na uchumi, utaamduni, na michezo, afya na elimu. Serikali ya China imetekeleza ahadi na inaendelea kutekeleza kwa kutoa mkono wa ushirikiano katika kujenga viwanja vya michezo katika mataifa mbalibmali barani Afrika na kuwatuma wafanyabiashara wa China kuzuru bara la Afrika, ili kuwapa wafanyabiashara wa barani Afrika hamasa na mbinu za kufaulu katika biashara na vilevile kubadilishana mawazo katika mbinu za kuimarisha na kuboresha biashara.

Pia anasema anafurahia ujenzi wa barabara na miundo mbinu mingine ili kuboreha na kurahisisha urafiki katika bara zima la Afrika. Ni matumaini yake na ya wengine kuwa, China kama nchi yenye kujali mataifa ya bara la Afrika itaendelea na kudumisha ushirikiano wa kutoa misaada kwa mataifa maskini barani Afrika ili kujimudu kimaendeleo. Na pia anasema katika mwaka wa 2008, ana matumaini kwamba mataifa ya Afrika mashariki yaani Kenya, Uganda na Tanzania pia yatafikiriwa na kuzingatiwa hasa katika ujenzi wa viwanda, shule, hospitali na miundo mbinu yaani barabara, viwanja vya michezo na vya ndege. Pia ni matumaini yake kuwa uongozi wa Radio China Kimataifa utaendelea na juhudi za kuboresha matangazo na vipindi kwa ushriikiano na mashirika mbalimbali ya habari ya utangazaji barani Afrika kujenga vituo vya Radio China Kimataifa katika mataifa ya bara la Afrika.

Tunawashukuru wasikilizaji wote waliotutumia barua, ni matumaini yetu kuwa wataendelea kusikiliza kwa makini matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo kwa vipindi vyetu ili tuviandae vizuri zaidi.