Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-24 18:52:36    
Moja ya mbinu 36, Kujifanya mjinga

cri

"Kujifanya mjinga" ni moja ya mbinu 36 za kivita, maana yake ni kujifanya kutoelewa mambo yenyewe, lakini kwa kweli unaelewa kila kitu.

Kwenye kitabu cha kale cha China kiitwacho "Yijing" mbinu hiyo inaelezwa kwamba "bora ujidai huelewi kuliko kujidai unafahamu mambo na kutenda kwa pupa."

Mbinu hiyo kwenye kitabu cha "Mbinu 36 za Kivita" inaelezwa kwamba, hata kama una uwezo wa kutosha, haifai kuonesha uwezo wako hadharani, bali unapaswa uonekane kama mnyonge ili kuwapumbaza maadui na kuwafanya wawe wajeuri, kisha kuwapa pigo la kasi bila wao kudiriki lolote. Cha muhimu katika matumizi ya mbuni hiyo ni "kujidai" ili kuwapumbaza maadui.

Mbinu ya "kujifanya mjinga" inatumiwa sana na wanasiasa. Wakati hali inapokuwa mbaya ujidai kama mjinga na kufanya mambo yasiyo ya maana, huku unaficha uwezo na nia yako ya kisiasa, ili maadui wasiwe na tahadhari, na wakati mzuri unapowadia timiza nia yako ya kisiasa.

Ifuatayo ni hadithi iliyotokea katika historia ya China:

Karne ya tatu K.K. China ilikuwa katika kipindi ambacho madola mengi yalikuwa yanapigana. Jemadari Cao Cao na Liu Bei wote walikuwa wanataka kutawala madola yote, lakini nguvu ya Liu Bei ilikuwa dhaifu na hakufua dafu kupambana na Cao Cao, zaidi ya hayo alikuwa chini ya uangalizi wa Cao Cao. Ili kuficha nia yake alijidai anamheshimu na kumsikiliza sana Cao Cao.

Siku moja Cao Cao alimwalika Liu Bei kwenye chakula. Cao Cao alimwuliza Liu Bei, "Unaona ni nani aliye shujaa duniani?" Liu Bei alitaja watu kadhaa, lakini wote walibezwa na Cao Cao. Kwa ghafla Cao Cao alisema, "Katika dunia hii shujaa ni mimi na wewe tu!" Liu Bei aliposikia aliyosema alishtuka hata vijiti vya kulia vikamponyoka mkononi. Liu Bei alidhani pengine Cao Cao aligundua nia yake ya kisiasa, kama hivyo ndivyo basi siku za uhai wake zilikuwa zinahesabika. Bahati nzuri wakati huo radi kali ilipiga, Liu Bei alimwambia Cao Cao kuwa alishitushwa na radi. Cao Cao alipoona jinsi Liu Bei alivyokuwa mhofu alicheka akidhani mtu huyo ni mwoga hata anaogopa radi, atawezaje kufanikiwa mambo ya taifa? Kwa hiyo akapuuza tahadhari dhidi yake. Baadaye Liu Bei alijinasua kutoka kwenye udhibiti wa Cao Cao na kujiunga na jemadari mwingine Sun Quan na kupambana kwa pamoja dhidi ya Cao Cao, mwishowe alianzisha utawala wake na kusababisha hali ya kuwepo kwa madola matatu yaliyolingana kwa nguvu katika historia ya China.

"Kujifanya mjinga" ikiwa mbinu ya kuwapumbaza maadui pia inatumika katika mashindano ya biashara. Wafanyabiashara wanatumia mbinu hiyo kwa kuficha nia yao, wanajifanya wajinga wakati wanafahamu, au wanajifanya werevu wakificha ujinga wao. Wakati fulani mambo ambayo wanaweza kuyatenda wanasema hawawezi, ili kulazimisha wapinzani walegeze masharti na kujipatia manufaa katika mapatano ya kibiashara. Wakati fulani wanafahamu hali ilivyo lakini wanajidai kuwa hawafahamu lolote, ili kuwadanganya wapinzani wao. Ili kukwepa kutegwa na mbinu hiyo wahusika wanapaswa kufafanua vilivyo hali ya pande zote wala sio kufanya uamuzi kwa mujibu wa jinsi mpinzani wako anavyoonekana au maneno anayosema. Hii ni sababu kwa nini kitabu cha mbinu za kivita mara nyingi kinasema "Fahamu hali yako mwenyewe na fahamu hali ya adui wako, ndipo unapoweza kushinda mapambano yote".