Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-24 19:51:46    
Mabadiliko ya vyombo vya usafiri nchini China

cri

Mkutano wa bunge la umma la China ulifanyika kuanzia tarehe 5 hadi 18 mwezi Machi. Wakati wa mkutano huo, mwandishi wetu wa habari aliwahoji wajumbe Waislam waliohudhuria mkutano huo. Baada ya China kufanya mageuzi na kufungua mlango kwa miaka 30, vyombo vya kusafiri nchini China vinabadilika siku hadi siku.

"Miaka 30 iliyopita tulitembea kwa miguu tu, hata hatukuwa na baiskeli, baadaye hali ilikuwa nzuri zaidi, tulikuwa na baiskeli."

Mjumbe Su Guanglin, ambaye ni imam wa msikiti mjini Lanzhou, alipozungumzia hali isiyokuwa rahisi wakati huo alicheka. Alisema wakati huo kama waliweza kuwa na baiskeli, walikuwa wanaridhika sana. Baada ya kufanya mageuzi na kufungua mlango mwaka 1978, uchumi uliendelezwa, na baiskeli zilianza kuenezwa, kuanzia hapo, China ilikuwa "nchi maarufu wa baiskeli" duniani. Ingawa wakati huo nauli ya basi haikuwa kubwa, lakini sio watu wote waliweza kumudu. Bw. Su Guanglin akikumbusha alisema,

"Wakati huo nauli ya basi ilikuwa ndogo, lakini mapato yetu hayakufikia kiwango cha kumudu gharama hizo mbali na chakula na nguo, hivyo hatukupanda mabasi."

Kuanzia miaka ya 80 hadi miaka 90, vyombo vingine ya usafiri yaani pikipiki, viliingia katika maisha ya watu. Mjumbe wa kabila la Wakirgizi, kutoka mkoa wa Xinjiang Bibi Maria Mati alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, wakati huo kupanda pikipiki kulikuwa jambo la fahari. Bibi Maria alisema pikipiki aliyopanda wakati huo bado ilikuwa inatumia mafuta ya dizeli, baadaye pikipiki nyingi zimekuwa zinatumia nishati ya umeme, ambazo zinahifadhi mazingira. Katika miaka ya 70 na 80 ya karne iliyopita nchini China, kupanda magarimoshi na ndege kulikuwa sio jambo la kawaida kama sasa. Mjumbe wa kabila la Wahui wa mkoa wa Ningxia Bw. Bai Shangcheng akizungumzia mara yake ya kwanza kupanda garimoshi, alisema,

"Mara yangu ya kwanza niliposafiri kwa garimoshi ilikuwa katika mwaka 1979, nilijisikia vizuri. Wakati huo umbali wa mji wa Lanzhou kutoka maskani yangu ulikuwa kilomita 600 tu, lakini ilinichukua muda wa usiku mzima. Sasa mara za kusafiri garimoshi zimapungua, ninaendesha gari kwenye barabara ya mwendo kasi, inanichukua saa 4 hadi 5 tu."

Kadiri mageuzi na ufunguaji mlango yanavyoendelea, na kutokana na maendeleo ya uchumi wa China, ndivyo vyombo vya usafiri pia vimekuwa na mabadiliko mapya siku hadi siku. Baada ya kuingia mwishoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90, magari binafsi pia yalianza kuwa mengi. Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 90, magari yaliingia katika familia za watu wa kawaida. China hatua kwa hatua imekuwa "nchi ya magari" kutoka "nchi ya baiskeli". Mjumbe wa kabila wa Wahui kutoka mkoa wa Shandong Bw. Wan Qiusheng alisema,

"Zamani watu walipanda baiskeli, karibu hakukuwa na pikipiki, lakini sasa hata nimebadili magari mara kadhaa."

Bw. Wan Qiusheng ni mfano mzuri wa kuanzisha kampuni yake kwa mafanikio kutokana na mageuzi na ufunguaji mlango. Akizungumzia hali yake ya hivi leo, alisema,

"Siwezi kuanzisha kampuni yangu mwenyewe kama kusingekuwa na mageuzi na ufunguaji mlango."

Baada ya mageuzi na ufunguaji mlango, Waislam kama Bw. Wan Qiusheng wanaoanzisha shughuli zao na kutajirika ni wengi. Kutokana na maendeleo ya uchumi wa nchi na urahisi wa mawasiliano, pamoja na kuongezeka kwa mapato yao, Waislam wanaotaka kwenda Mecca kuhiji ili kutimiza matumaini yao wanaongezeka zaidi siku hadi siku. Hija ya moja ya nguzo 5 za dini za Kiislam, hivyo Waislam wote wanataka kwenda Mecca wakiwa hai. Baada ya China kufufua kazi ya kutuma ujumbe wa kwenda kuhija mwaka 1979, kila mwaka Waislam wa China wanaweza kwenda Mecca kuhiji, na idadi ya watu hao imekuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka. Bw. Su Guanglin alisema, mwaka jana idadi ya Waislam mkoani Gansu waliojiandikisha kwenda kuhiji ilifikia zaidi ya 10,000, na mwaka 2006 alifanikisha nia yake ya kwenda kuhiji huko Mecca. Lakini zamani kuhiji kulikuwa sio jambo rahisi. Alisema,

"Zamani tulikuwa hatuwezi kufikiria kwenda kuhiji, kwani ilikuwa inachukua muda mrefu, ilichukua muda wa mwaka mmoja na zaidi, kwa kuwa mawasiliano hayakuwa rahisi. Zamani tukitaka kuhiji tulipaswa kufunga safari yetu kutoka Beijing, hatukuweza kuanza safari mjini Lanzhou. Niliwahi kutoa mwito katika mikutano mingi kupunguza mzigo kwa Waislam, yaani gharama ya kwenda Beijing. Baada ya kujadiliwa, serikali inakidhi matumaini yangu, sasa tunaweza kufunga safari kutoka Lanzhou, ni rahisi sana."

Maendeleo na mabadiliko ya vyombo vya mawasiliano yanatoa urahisi mwingi kwa watu. Sasa kupanda magarimoshi au kupanda ndege kusafiri ni jambo la kawaida. Hasa maendeleo ya mtandao wa mawasiliano mijini yanarahisisha maisha ya watu. Mjumbe wa Beijing wa kabila la Wahui Bibi Wang Xiaoke alisema,

"Mawasiliano ya sasa yamekuwa rahisi zaidi, hasa kupitia njia ya subway ni rahisi, naona kuwa serikali imeboresha sana kazi ya upande huo. Zamani serikali ilitaka kutoa urahisi kwa watu kusafiri, sasa inazingatia zaidi namna ya kutatua tatizo la msongamano wa barabarani. Kwa sababu ya maendeleo ya uchumi, ongezeko la magari ni la kasi kuliko ongezeko la miundo mbinu ya mawasiliano, hivyo ripoti ya kazi za serikali ya kila mwaka inatilia maanani utengaji wa fedha katika mawasiliano ya umma. Aidha, mwaka jana serikali ya mji wa Beijing ilipunguza bei ya tikiti za mawasiliano ya umma, na kutumia kadi ya IC, na kuwahimiza wakazi kutumia mawasiliano ya umma. Hatua hizo zinapunguza shinikizo la mawasiliano."

Bibi Wang Xiaoke alisema, kadiri uchumi wa China unavyoendelezwa, ndivyo idadi ya magari binafsi inavyoendelea kuongezeka. Lakini michezo ya Olimpiki itafunguliwa hapa Beijing katika siku chache zijazo, alieleza matumaini yake kuwa, wakati huo wakazi wa Beijing wataacha kuendesha magari yao binafsi kadiri wawezavyo na kutumia mawasiliano ya umma, ili kuweka mazingira mazuri ya mawasiliano, vilevile kuweka mazingira mazuri ya usafiri kwa wageni kutoka nchi mbalimbali duniani.