Sherehe ya ukaguzi wa gwaride ya kuadhimisha miaka 16 ya ushindi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Urusi ilifanyika tarehe 27 mwezi huu huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. Wakati watu wa nchi hiyo walipokuwa wanasherehekea siku hiyo, kundi la Taliban lilizusha mashambulizi na kusababisha vifo vya watu wanne akiwemo mbunge mmoja, lakini rais Hamid Karzai wa nchi hiyo alinusurika.
Asubuhi ya siku hiyo, rais Karzai na wanasiasa wa nchi hiyo walihudhuria sherehe hiyo. Wakati rais Karzai alipokuwa anaanza kutoa hotuba ya ufunguzi wa sherehe hiyo, watu wenye silaha wa Taliban walirusha maroketi kadhaa dhidi ya sehemu ilipofanyika sherehe hiyo na kupambana na jeshi la serikali, mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu wanne, akiwemo mbunge mmoja na watu wengine 7 kujeruhiwa. Baadaye msemaji wa kundi la Taliban Bw. Zabiullah Mujaheed alitangaza kuwajibika na tukio hilo, na kusema wanachama 6 wa Taliban walikuwa wamevaa fulana zenye mabomu na walifanya shambulizi hilo kwa kutumia bunduki na maroketi, shabaha ya shambulizi hilo ilikuwa ni rais Karzai wa nchi hiyo, watu watatu kati ya hao waliuawa katika mapambano hayo.
Kutokana na kuwa rais Karzai aliondoka kwenye sehemu hiyo kwa wakati, hakujeruhiwa katika shambulizi hilo. Tangu rais Karzai alipoingia madarakani, amechukuliwa kuwa moja ya shabaha za Taliban, kabla ya hapo alinusurika mara tatu kuuawa. Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Karzai kushambuliwa na kundi la Taliban katika mji mkuu wa nchi hiyo. Baada ya kutokea kwa tukio hilo, rais Karzai alitoa hotuba kulaani mashambulizi hayo, alisema kundi la Taliban kuzusha mashambulizi kwenye shughuli za maadhimisho ya miaka 16 ya ushindi wa vita dhidi ya uvamizi wa Urusi kumeharibu sikukuu muhimu ya nchi na wananchi wa Afghanistan. Habari zinasema, rais Karzai ametoa amri ya kufanya uchunguzi kamili kuhusu tukio hilo. Hivi sasa kikosi cha usalama cha nchi hiyo kimewakamata watu kadhaa waliohusika na shambulizi hilo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon siku hiyo alitoa taarifa akilaani vikali tukio hilo. Taarifa hiyo inasisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono wananchi wa Afghanistan wasukume mbele mchakato wa ukarabati chini ya uongozi wa serikali halali, na katibu mkuu wa jumuiya ya NATO Bw. Jaap de Hoop Scheffer siku hiyo pia alitoa taarifa kulaani shambulizi hilo. Taarifa hiyo inasema jumuiya ya NATO itaendelea kuisaidia serikali ya Afghanistan na wananchi wake katika kulinda usalama na demokrasia.
Mwaka huu hali ya usalama nchini Afghanistan imezidi kuwa mbaya. Mashambulizi mbalimbali yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 450. Kundi la Taliban tarehe 25 mwezi Machi lilitangaza kuanzisha mashambulizi ya majira ya Spring dhidi ya jeshi la serikali ya nchi hiyo na majeshi ya nchi za nje nchini humo. Vyombo vya habari vinaona kuwa mashambulizi hayo yatazusha wimbi jipya la mabavu nchini humo.
Wakati huo huo rais Karzai wa nchi hiyo tarehe 25 mwezi huu alilaani vikali baadhi ya vitendo vya Marekani na Uingereza katika vita vya Afghanistan, na kuona kuwa kuwakamata wanachama wa Taliban na wafuasi wao hakusaidii hata kidogo kwenye mapambano dhidi ya ugaidi. Rais Karzai aliitaka Marekani iache mapema vitendo hivyo na kutilia maanani zaidi shughuli za ukarabati wa nchi hiyo. Wachambuzi wanaona kuwa hii imeonesha nia ya rais Karzai kutaka kuboresha uhusiano kati yake na kundi la Taliban na kuondoa hali ya wasiwasi ya muda mrefu kati ya serikali ya nchi hiyo na kundi la Taliban. Lakini kutokana na hali ya hivi sasa, juhudi hizo hazikufanikiwa kuzuia mashambulizi ya Taliban, na hali ya wasiwasi kati ya pande hizo mbili itaendelea kuwepo.
|