Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-28 19:38:45    
China yakarabati kasri la Potala ili kuhifadhi utamaduni wa Tibet

cri

Kasri la Potala lililoko katikati ya Lhasa mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Tibet lina historia ya zaidi ya miaka 1,300, na ni majengo ya kale ya kasri yaliyojengwa kwenye uwanda wa juu zaidi na kuhifadhiwa vizuri zaidi duniani. Kuna hadithi nzuri kuhusu kasri hilo. Mnamo karne ya 7, ili kumwoa binti wa mfalme wa enzi ya Tang, mfalme wa Tibet aliamuru kasri hilo lijengwe. Kasri la Potala lilijengwa kando ya mlima, na sasa lina eneo la mita za mraba zaidi ya laki 4, jengo kuu la kasri hilo lenye ghorofa 13 lilijengwa kwa mawe na mbao, paa lake limeezekwa kwa vigae vya shaba vilivyopakwa rani ya dhahabu. Kasri hilo linaonesha vizuri usanii wa ujenzi wa majengo ya kale ya kabila la Watibet.

Kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kimaumbile na kasoro ya miundo yake yenyewe, kasri la Potala lililojengwa miaka mingi iliyopita lilikuwa katika hali mbaya, msingi wa majengo yake ulianguka na kuharibika, na ukuta wake ulikuwa na ufa na kuanza kuporomoka, mbali na hayo, nguzo za kasri hilo pia zilikumbwa na hali ya hatari kutokana na wadudu wanaokula mbao. Ili kuhifadhi kasri hilo, tangu miaka ya 50 ya karne iliyopita, hasa katika miaka 20 iliyopita China ilifanya kazi nyingi za kulikarabati.

Tokea mwaka 1959, licha ya kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kawaida kwa kasri la Potala, mwaka 1989 na mwaka 2002 kwa mara mbili serikali ya China ilitenga fedha nyingine nyingi kwa ajili ya utarabati mkubwa kwa kasri hilo. Mkurugenzi wa idara ya uendeshaji wa kasri la Potala Bw. Qamba Kelzang alisema,

"Kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1994, kwa mara ya kwanza serikali kuu ya China ilitenga yuan milioni 53 kwa ajili ya kazi za kuliimarisha kasri la Potala ili kuondoa hali ya hatari ya majengo hayo. Mwaka 2002 serikali ya China ilitenga yuan milioni 170 ili kukarabati kasri hilo kwa mara ya pili, na kazi za ukarabati wa mara hiyo sasa bado inaendelea."

Imefahamika kuwa kazi za ukarabati wa mara ya pili zinahusu sehemu tano, yaani kuimarisha msingi wa majengo, kuboresha mazingira ya sehemu karibu na kasri hilo, kuboresha mifumo ya maji, umeme na usalama, ufuatiliaji na usimamizi wa majengo kwa teknolojia ya kisasa na kurudisha hali ya asili ya picha za ukutani. Mzee Jam Yang ni fundi wa kampuni ya uchoraji wa majengo ya sanaa ya kale ya mji wa Lhasa, Tibet, na tangu miaka ya 80 ya karne iliyopita alianza kujiunga na kazi za kukarabati kasri la Potala, alisema,

"Niliwahi kushiriki kwenye kazi za ukarabati wa mabaki muhimu ya utamaduni mkoani Tibet likiwemo kasri la Potala, mabaki hayo yana thamani kubwa kwa China na hata dunia, na serikali ya China imetenga pesa nyingi ikwa ajili ya kuihifadhi. vikiwa vitu vya mabaki ya kale, kazi za ukarabati wake ni tofauti sana na zile za vitu vya kawaida. Kila tunapofanya kazi hizo, tunakusanya maoni ya pande mbalimbali, ili kuzifanya vizuri."

Mtaalamu mmoja aliyeshiriki kwenye kazi za ukarabati wa kasri la Potala alijulisha kuwa, idara kuu ya vitu vya mabaki ya kale ya China na idara zinazohusika za Tibet zinatuma vikundi vya wataalamu wa sekta mbalimbali yakiwemo majengo ya kale, jiolojia na maji kufanya utafiti kwenye majengo yote ya kasri la Potala, ili kutathmini njia za kulikarabati kasri hilo.

Bw. So Nam ambaye ni mwamini wa dini ya kibudha ya kitibet alijionea mabadiliko ya mara pili ya kasri la Potala, alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni, serikali yetu ilitenga pesa nyingi kwa ajili ya kuhifadhi na kukarabati mahekalu muhimu mkoani Tibet likiwemo kasri la Potala na hekalu la Sakya. Hatua hizo zimehifadhi vizuri mabaki ya utamaduni wa Tibet, na sisi watu waamini wa dini ya kibudha tunafurahi sana."

Katika mara ya pili ya kulikarabati kasri la Potala, pesa nyingi zilizotengwa na serikali zilitumiwa katika kufanya kazi ya kurudisha hali ya asili ya picha za ukutani za mita za mraba 2,100 ndani ya kasri hilo. Hivi sasa kazi hiyo imekamilika, picha hizo zinadumisha sura zao za awali. Mkuu wa idara ya uendeshaji wa kasri la Potala Bw. Qamba Kelzang alisema,

"Kanuni yetu ni kuvikarabati vitu vya kale kuwa vitu vya kale, rangi tulizotumia kwenye kurudisha hali ya awaili ya picha za ukutani ni za madini, rangi hizo hazitatoweka daima."

Kazi za ukarabati wa kasri la Potala sasa zimekamilika kwa asilimia 70, na zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu. Wakati huo huo kazi za ukarabati pia zinafanyika kwenye mahekalu ya Norbu Lingka na Sakya ambayo pia ni mabaki maarufu ya majengo ya dini ya kibudha ya kitibet. Naibu mwenyekiti wa kamati ya serikali ya mkoa unaojiendesha wa Tibet Bw. Padma Tsinle alisema,

"Kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2005, China imetenga yuan milioni 330 ili kuhifadhi kasri la Potala na mahekalu ya Norbu Lingka na Sakya. Aidha kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2010, China itatenga yuan kati ya milioni 700 na 800 katika kazi za kuyakarabati mahekalu. Madhumuni ya hatua hizo ni kuhifadhi mabaki ya utamaduni, pia ni kuhifadhi dini."

Tibet ni mkoa wenye mabaki mengi ya utamaduni nchini China. Katika zaidi ya 20 iliyopita, serikali kuu ya China na serikali ya mkoa huo kwa jumla zimetenga yuan bilioni moja kwa ajili ya kuhifadhi mahekalu na sehemu nyingi 1,400 za dini ya kibudha. Kutokana na mpango kuanzia mwaka huu, serikali ya China itatenga yuan nyingine karibu milioni 600, ili kuyakarabati majengo 22 ya mabaki ya utamaduni na mahekalu mkoani Tibet.