Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-29 21:04:17    
Barua 0429

cri

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga nchini Tanzania kwenye barua yake anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya ksiwahili ya radio China Kimataifa hatujambo, na yeye ni mzima sana na anaendelea kuitegea sikio radio yake aipendayo, Radio China Kimataifa, Anapenda kutumia fursa hii kuwapa pole marafaiki zake wa jamhuri ya watu wa China na wasio wachina kwa kukumbwa na theluji nyingi iliyotokea wakati wa majira ya baridi mwezi wa kwanza kuanzia talehe 10. Lakini pia msikilizaji wetu huyu anauliza, idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa iliwatangazia wasikilizaji wake kuwa mwaka jana ingeanza kurusha matangazo yake kwenye mawaimbi ya FM kupitia shirika la utangazaji Tanzania TBC pamoja na sauti ya Tanzania Zanzibar lakini mpaka sasa haijafanyika, kwa nini? Pili Jarida la daraja la urafiki mbona mpaka sasa hivi bado kimya, kuna nini mbona wasikilizaji hawajatumiwa?

Mwisho anaomba kitengo kinachohusika na maswali ya chemsha bongo kuwatumia makala ya chemsha bongo kabla ya makala hiyo kutangazwa, kwani makala hiyo ya chemsha bongo huchelewa sana kuwafikia. Kwa mfano makala ya maswali ya chemsha bongo inayohusu michezo ya Olimpiki ya Beijing hadi 30 mwezi wa kwanza 2008 bado haijamfikia. Anamalizia barua kwa kuwatakia wafanyakazi wote na wasikilizaji wa Radio China Kimataifa kazi njema.

Msikilizaji wetu Issa Rashid Ally wa S.L.P 208 Tabora nchini Tanzania anaanza barua yake kwa kusema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa ni buheri wa afya, na pia anawapa pole wafanyakazi wote kwa majukumu ya kila siku. Anasema anaendelea lengo hasa la barua yake ni kumtafutafuta rafiki kati ya wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Yeye ana umri wa miaka ishirini na tatu, na rafiki amtakaye ni wa umrri wake au usiozidi miaka 32, hana ubaguzi wa jinsia, rafiki anaweza kuwa mwanaume au mwanamke. Pia anapenda kuishauri idhaa ya kiswahili ya CRI kuanzisha kipindi cha papo kwa papo ambacho msikilizaji anaweza kuuliza na kujibiwa. Anamalizia kwa kusema kwamba yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tano na kwa yoyote yoyote kati ya wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya CRI atakayependa kuwa rafiki yake amtumie picha yake na yeye atamtumia ya kwake.

Msikilizaji wetu Julias Tocta Ng'oja wa Kanisa katoliki Reha, S.L.P 129 Tarakea Rombo Kilimanjaro nchini Tanzania anaanza barua yake kwa kuwasalimu wafanyakazi wote wa CRI. Anasema yeye ana machche ambayo anapenda kuuliza, kwanza anataka kujua atafanya nini kwa sababu posta ya huko kwao inakataa bahasha alizonazo na analazamika kusafiri kwenda nchi jirani kuzituma, pili anasema baada ya matokeo ya Chemsha bongo kutolewa wasikilizaji wa vijijini wamekufa moyo kwani wameona wasikilizaji wanaotumia mtandao ndio walioshinda, tatu anasema anafuraha kwa sababu anaipata CRI kwa njia nzuri kabisa kupitia KBC kwa yeye anaishi mita 200 kutoka mpakani, pia anaipata kupitia masafa mafupi.

Bwana Tocta Ng'oja pia anasema anasikitika sana kuona Marekani inamwunga mkono Dalai Lama anayejifanya kudai uhuru wa Tibet hali Tibet ipo ndani ya China, anasema vipindi vya CRI vinaendelea kumuelimisha na kumfahamisha zaidi kuhusu suala hilo. Pia anshukuru kwa sababu anaendelea kuburudika na kufahamu mengi zaidi anaposikiliza vipindi vinavyozungumzia makabila madogomadogo ya China na vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa mbalimbaliya China. Anamaliza kwa kuwatakia kazi njema mashabiki wote wa CRI wanaosali katika kanisa katoliki la Reha, na anawaomba waendelee na moyo wao wa kuchapa kazi kwa bidii.

Wasikilizaji wapendwa ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya Posta hazipokei bahasha zilizolipiwa tunazowatumia, tunasikitishwa sana na hali hiyo, lakini kadiri siku zinavyoendelea ndivyo tunatarajia kuwa hali hiyo itabadilika. Kuhusu juhudi za matangazo yetu kuanza kusikika nchi Tanzania, bado zinaendelea. Kama mnavyojua kumekuwa na mabadiliko mengi kubadilisha kutoka Radio Tanzania, kwenda Taasisi ya Utangazaji na sasa TBC, mabadiliko hayo yamefanya baadhi ya mambo yaende polepole. Na malalamiko kuhusu uchaguzi wa washindi wa chemsha bongo, tunapenda mfahamu kuwa wasikilizaji wetu wote ni sawa, bila kujali wanasikiliza matangazo yetu kupitia FM, internet au masafa mafupi, bila kujali wanawasiliana nasi kwa njia ya posta au kwa e mail. Si wote waliopata ushindi walitumia barua pepe, wengi walituma barua kwa njia ya posta, kwa hiyo tunaomba wasikilizaji wetu msijisikie kubaguliwa, kwetu umuhimu wenu uko sawa kabisa.

Msikilizaji wetu mwingine Bw Korry Joseph Begga wa shule ya msingi Nyansurura, S.L.P 300 Musoma, Mara nchini Tanzania, ametuandikia barua akisema yeye ni kijana wa kiume wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 22 na kwa sasa yupo kidato cha sita. Anapenda kujiunga na idhaa ya kiswahili ya radio China Kimataifa ili aweze kuchangia mawazo mbalimbali ili kuboresha idhaa hii ya kiswahili ya CRI.Anamalizia kwa kusema kuwa atashukuru sana kama ombi lake litakubaliwa, na anawatakia wafanyakazi wote kazi njema na Mungu awabariki sana.

Karibu sana Bw Korry kwenye usikilizaji wa matangazo yetu, tunakupokea kwa mikono miwili uwe huru kutoa maoni na mapendekezo yako kwa matangazo yetu.

Bw Geoffrey Asuza Modaki wa S.L.P 49 kakamega nchini Kenya anaanza barua yake kwa kutusalimu na watangazaji na wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Bw Joseph anashukuru sana kupata barua tuliyomwandikia wiki chache zilizopita. Anasema anapenda kutujulisha kuwa anafurahia sana vipindi vya CRI hasa habari, maelezo baada ya habari, kipindi cha salamu zenu na jifunze kichina na vipindi vingine vinavyohusu utamaduni wa China. Anamalizia barua yake kwa kuishukuru sana kwa kumkumbuka na anaomba pia kama anaweza kutumiwa kofia yenye maandishi ya CRI pamoja na fulana.

Tunawashukuru wasikilizaji wote waliotuletea barua na kutoa maoni na mapendekezo kwa matangazo yetu, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kuwa nasi katika kuboresha vipindi vyetu na kudumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.