Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-30 16:41:19    
Umoja wa Mataifa watoa hatua nyingi mfululizo kukabiliana na msukosuko wa nafaka

cri

Mkutano ulioshirikisha viongozi wa mashirika 27 yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa na kuendeshwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon umepata mafanikio makubwa baada ya kufanya mashauriano kwa siku moja. Asubuhi tarehe 29 Bw. Ban Ki-moon alitangaza hatua nyingi mfululizo za kukabiliana na msukosuko wa nafaka uliotokea hivi karibuni duniani. Mkutano huo ulifanyika kwa siku mbili huko Bern Uswisi, lakini siku ya pili asubuhi wakati mkutano ulipokuwa unaendelea Bw. Ban Ki-moon alifanya mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kwamba mkutano umefanya maamuzi mengi.

"Tumefanya maamuzi kwa umakini, maamuzi hayo yakiwa ni pamoja na hatua zitakazotekelezwa katika kipindi kifupi, kipindi kirefu kiasi na kipindi kirefu."

Mkutano huo ulifanyika kutokana na shinikizo kubwa la hatari. Katika miezi kadhaa iliyopita msukosuko wa nafaka ulitokea na kuzusha vurugu katika nchi kumi kadhaa barani Afrika, Asia na sehemu ya Bahari ya Caribbean, zaidi ya hayo bei ya nafaka inaendelea kupanda kwa kasi. Wakati huu wa hatari, nchi nyingi zina matumaini kuwa Umoja wa Mataifa utajitokeza na kuwa kama mwokozi. Bw. Ban Ki-moon alisema, Umoja wa Mataifa unaona kuwa kwanza kabisa ni lazima tuhakikishe watu wenye janga la njaa wanapata chakula. Alisema,

"Suala la kwanza linalotakiwa kutatuliwa ni kuhakikisha watu wenye njaa wanapatiwa chakula, kwa hiyo Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutaka jumuyia ya kimataifa, na kwanza kabisa nchi zilizoendelea zitoe msaada wa fedha dola za Marekani milioni 755."

Bw. Ban Ki-moon aliongeza kuwa, kama msaada huo hauwezi kupatikana mara moja, "janga la njaa lisiloweza kukadirika, utapiamlo na vurugu za kijamii zitazuka." Hali ni ya hatari sana. Kuhusu wito wa Bw. Ban Ki-moon mkurugenzi wa Benki ya Dunia Bw. Robert Zoellick alisema, huu ni wakati kwa wadhamini wa kimataifa kufanya mambo kwa vitendo. Alisema,

"Kwa mujibu wa takwimu, katika miaka miwili iliyopita, watu zaidi ya milioni mia moja wametumbukia kwenye umaskini kutokana na bei ya nafaka kupanda. Hali hiyo haikusababishwa na maafa ya kimaumbile, lakini hali hiyo pia ni sawa na maafa. Wadhamini wa kimataifa wanapaswa kuitikia wito huo na kutosheleza mahitaji ya dharura ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP kwa kuchagia dola za Marekani milioni 755."

Hivi karibuni baadhi ya nchi zimechukua hatua za kusimamisha au kupunguza nafaka zinazouzwa nchi za nje. Bw. Ban Ki-moon anaona kuwa nchi hizo zinapaswa kurekebisha hatua zao kwa kutumia mbinu za bei na sera, wala sio kudhibiti uuzaji wa nafaka kwa nchi za nje. Bw. Robert Zoellick pia alisema Benki ya Dunia inapenda kuzisaidia baadhi ya nchi kifedha, lakini haifai kuchukua za kudhibiti uuzaji wa nafaka kwa nchi za nje. Alisema

"Tunahimiza nchi hizo ziache hatua za kusimamisha uuzaji wa nafaka kwa nchi za nje, kwa sababu kufanya hivyo kutapandisha bei ya nafaka na kuziongezea baadhi ya nchi tatizo la chakula."

Licha ya hatua za msaada katika kipindi kifupi, hatua zitakatotekelezwa katika kipindi kirefu kiasi ni kuzifanya nchi zilizo nyuma kiuchumi ziinue uwezo wa uzalishaji wa kilimo. Kwenye mkutano huo kimsingi imeamuliwa kutoa pembejeo zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 kwa wakulima milioni 200 wa nchi zilizo nyuma kiuchumi ikiwa ni pamoja na mbegu, na Benki ya Dunia itaongeza mikopo kwa nchi za Afrika. Bw. Ban Ki-moon alisema, haifai tena kutumia njia ya zamani ya kutoa msaada wa nafaka moja kwa moja, bali kuna haja ya kuwahamasisha wakulima walime. Alisema, "Suala jingine linalotakiwa kutatuliwa ni kuzalisha nafaka kwa ajili ya siku za mbele. Wakati bei ya nafaka inapopanda wakulima wa nchi zinazoendelea wamepunguza uzalishaji wa kilimo kwa sababu wanapungukiwa pembejeo na nishati. Ni lazima tufanye juhudi kadiri tuwezavyo kuwahamasisha wakulima waimarishe uzalishaji wao na kuhakikisha kuwa mwaka kesho hakutakuwa na upungufu wa nafaka."

Mkurugezi mkuu wa FAO Bw. Jacques Diouf alisema hatua hizo "ni kama mvua katika siku za kiangazi", kwa sababu hata wakulima hao wanataka kulima pia wanashindwa kumudu bei ya sasa ya mbegu na nishati.