Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe imewaalika wagombea wote wa urais au wawakilishi wao wasimamie kazi ya kuhesabu upya kura za uchaguzi wa urais iliyoanza tarehe 29 Aprili. Hatua hiyo huenda itaweza kuondoa hali ya mvutano ya hivi sasa.
Tarehe 29 Machi watu wa Zimbabwe walipiga kura kumchagua rais, wabunge na madiwani, hii ilikuwa mara ya kwanza kwa uchaguzi huo kufanyika kwa pamoja nchini Zimbabwe. Kundi la chama cha MDC linaloongozwa na Bw. Morgan Tsvangirai lilikishinda chama tawala cha Zanu-PF, na kupata viti vingi zaidi bungeni. Lakini matokeo ya uchaguzi wa urais yalichelewa kutangazwa, hali ambayo ililalamikiwa sana na kundi la Tsvangirai. Katika juhudi za kutafuta uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa, katibu mkuu wa chama cha MDC Bw. Tendai Biti alikwenda kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, akiliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lifuatilie msukosuko wa kisiasa nchini Zimbabwe, na kutuma mjumbe maalumu kwenda Zimbabwe kufanya uchunguzi. Lakini kwenye upigaji kura uliofanyika baadaye kwenye mkutano wa baraza la usalama, pendekezo hilo lilikataliwa na nchi nyingi wanachama wa baraza hilo, ambazo zinaona kuwa msukosuko wa kisiasa wa Zimbabwe unapaswa kutatuliwa ndani ya kanda yake.
Kazi ya kuhesabu upya kura za uchaguzi wa urais wa Zimbabwe inatazamiwa kufanyika kwa wiki moja. Na kabla ya hapo, tume ya uchaguzi ya Zimbabwe tarehe 19 Aprili ilikuwa imemaliza kuhesabu upya kura za majimbo 23. Matokeo hayo yanaonesha kuwa, hakuna tofauti kubwa kati ya matokeo hayo mapya na yale yaliyotangazwa hapo zamani, kwamba chama cha upinzani cha MDC kimepata viti vingi zaidi kuliko chama tawala cha Zanu-PF, na hadhi ya chama cha MDC kuwa chama chenye viti vingi bungeni haikuathirika.
Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe itatangaza matokeo rasmi baada ya matokeo hayo kuthibitishwa na pande mbalimbali. Kama hakuna mgombea yeyote atakayepata zaidi ya asilimia 51 ya kura, basi upigaji kura wa duru la pili utafanyika kati ya wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi. Ingawa kiongozi wa chama cha MDC Bw. Morgan Tsvangirai alijitangaza kuwa ameshinda kwenye uchaguzi wa rais, lakini chama cha Zanu-PF na wachambuzi wengine wanaona kuwa, inawezekana Bw. Tsvangirai alipata kura zinazolingana na zile za rais wa sasa Bw. Robert Mugabe, kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika kwa duru la pili la upigaji kura. Na kama kutakuwa na haja ya kufanyika kwa duru la pili, basi upigaji kura utafanyika ndani ya siku 21 baada ya matokeo ya kuhesabu upya kura kutangazwa.
Hali ya mvutano nchini Zimbabwe iliyosababishwa na uchaguzi wa rais imefuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Jumuiya ya SADC tarehe 12 Aprili ilifanya mkutano wa wakuu wa dharura wa kujadili msukosuko huo, lakini rais Mugabe hakushiriki kutatua msukosuko huo na ufumbuzi wa msukosuko ulishindwa kupatikana.
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambayo ni nchi jirani muhimu ya Zimbabwe aliwahi kusema hadharani mara kadhaa kuwa, hakuna msukosuko wa kibinadamu nchini Zimbabwe, na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuheshimu na kuwa na imani na tume ya uchaguzi ya Zimbabwe. Afrika Kusini ilikuwa nchi mwenyekiti wa zamu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili, ambapo ilikuwa inakataa maombi kadhaa ya kuitisha vikao maalumu kujadili hali ya Zimbabwe. Hata hivyo naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Lynn Pascoe tarehe 29 Aprili alisema, katibu mkuu Bw. Ban Ki-Moon ana nia ya kufanya usuluhishi kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika na Jumuiya ya SADC, na hajaondoa uwezekano wa kutuma mjumbe maalumu au tume ya uchunguzi nchini Zimbabwe.
|