Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-01 20:32:49    
China yaanzisha ghala la damu kwa ajili ya michezo ya Olimpiki

cri

Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Beijing mwezi Agosti mwaka huu ni tamasha kubwa la michezo duniani ambalo hufanyika kila baada ya miaka minne, ambapo wanamichezo na watalii kutoka nchi na sehemu mbalimbali watakutana hapa Beijing. Ili kukabiliana na ajali yoyote itakayoweza kutokea, China imeanza kuanzisha ghala la damu.

Kama tunavyofahamu damu ya binadamu inagawanyika kwenye makundi ya A, B, AB na O. Lakini kutokana na utafiti wa kina zaidi kuhusu damu ya binadamu, kuna kundi la damu liitwalo RH-. Watu wa Asia wenye damu ya kundi hilo ni wachache, lakini wengi wa watu makabila kadhaa madogomadogo nchini China na wazungu wana damu ya kundi hilo.

Naibu mkurugenzi wa Kituo cha damu cha Chama cha msalaba mwekundu cha Beijing Bi. Shi Weiwei alisema "Asilimia ndogo ya watu wa China wana damu kundi la RH-, na kwa kila waasia elfu moja, ni watu watatu tu wana damu ya kundi hilo, huku miongoni watu wa makabila madogomadogo ya China, kwa mfano kabila la Wauygur, watu wenye damu ya kundi la RH- wanachukua asilimia 5 hivi, na miongoni mwa wazungu wa Ulaya na Marekani, ni asilimia 15 hivi."

Ofisa wa kituo hicho Bw. Zhu Ruiliang alieleza kuwa, kuweka akiba nyingi ya damu kundi la RH- kunalenga kukabiliana na ajali yoyote itakayoweza kutokea, kwa mfano hali ya kujeruhiwa kwa wachezaji. Alisema  "Iwapo tukimkuta mgonjwa mwenye damu ya kundi hilo, tutapaswa kuongezea mgonjwa damu, hususan wakati mgonjwa akipata majeraha makubwa, tutahitaji damu nyingi."

Ili kulimbikiza damu ya kutosha ya kundi la RH- kwa ajili ya michezo ya Olimpiki, Kituo cha damu cha Chama cha msalaba mwekundu cha Beijing kilianza kufanya maandalizi tangu mwishoni mwa mwaka 2006. Naibu mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Shi Weiwei alieleza kuwa, mwaka 2006 kituo hicho kilitoa wito kwa jamii wa kuchangia damu ya kundi la RH-.

Bw. Wang Jisong ni miongoni mwa watu walioitikia wito huo. Alisema anafahamu kuwa ana damu ya kundi la RH-, ambayo ni adimu nchini China, na ni vigumu kupatikana zaidi kuliko damu ya makundi mengine. Kwa hiyo tangu mwaka 2006 bwana huyo amekuwa akichangia damu kwa mara kadhaa. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa,  "Nataka kutoa mchango kwa jamii kwa kadiri ya uwezo wangu, kwani ni watu wachache sana wana damu ya kundi hilo adimu."

Kwenye shughuli za kuwakutanisha wakazi wa Beijing wenye damu ya kundi la RH-, Bw. Wang na wenzake zaidi ya 1,300 walisema kama wageni watakaokuja Beijing kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki wakihitaji huduma ya kuongezewa damu, wao watatoa damu bila kusitasita.

Mbali na watu wa China, wageni wengi wanaoishi nchini China pia wamejitolea kuchangia damu ya kundi la RH-.

Bw. Nasser Hussain kutoka Saudi Arabia ni mwalimu katika shule moja hapa Beijing. Alipopata habari kuwa damu hiyo inahitajika sana kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, alijitolea kutoa damu kwenye Kituo cha damu cha Chama cha msalaba mwekundu cha Beijing. Alimwambia mwandishi wa habari kuwa, walimu wenzake wenye damu ya aina hiyo wote wamewahi kujitolea kutoa damu kwenye kituo hicho, alisema hii ni njia mwafaka kwao kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki na kuonesha uungaji mkono wao kwa michezo hiyo.

 "Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo naweza kuonesha upendo na moyo wangu wa dhati kwa watu wanaohitaji msaada, hususan wachezaji watakaoshindana kwenye michezo ya Olimpiki."

Naibu mkurugenzi wa kituo hicho cha damu Bi. Shi Weiwei alieleza kuwa, hivi sasa ghala hilo limehifadhi mililita laki 1.5 za damu ya kundi la RH-, kiwango hicho kitaongezeka hadi kufikia mililita laki 2 wakati michezo ya Olimpiki ya Beijing itakapofunguliwa.

Mjini Qingdao, ambao ni miongoni mwa miji 6 inayoshirikiana na Beijing kuandaa michezo ya Olimpiki, kundi la watu wanaojitolea kuchangia damu ya kundi la RH- limeanzishwa. Mkurugenzi wa Kituo cha damu cha mji wa Qingdao Bw. Chen Tonghua alisema  "Ili kuhakikisha mashindano ya mashua yanafanyika kwa mafanikio, hapa mjini Qingdao watu wanaojitolea zaidi ya 200 wenye damu ya kundi la RH- wameanzisha kundi moja, ambao wanaitikia wito wa kuchangia damu mara wanapohitajika, hali hiyo inaleta huduma za uhakika za kupatikana kwa damu."

Mbali na hayo Kituo cha damu cha Qingdao kinaandaa harakati mbalimbali za kuwashirikisha watu wengi zaidi wenye damu ya kundi hilo adimu. Imefahamika kuwa kabla ya mashindano ya mashua ya kukagua maandalizi ya michezo ya Olimpiki yatakapofanyika mwezi Mei mjini Qingdao, ghala la damu la mji huo litakuwa limelimbikiza mililita elfu 8 za damu ya kundi la RH-.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-01