Wizara ya ulinzi ya Russia tarehe mosi Mei ilitangaza kuwa, Russia imeongeza kutuma wanajeshi wa kulinda amani Abkhazia nchini Georgia, na wanajeshi hao walikuwa wamefika kwenye sehemu hiyo. Siku hiyo Georgia ilitoa malalamiko kwa balozi wa Russia nchini Georgia, na kuonesha kuwa hali ya wasiwasi imezuka tena kati ya nchi hizo mbili.
Tarehe 29 Aprili Russia ilitangaza kuongeza wanajeshi wake wa kulinda amani huko Abkhazia hadi elfu 3, ikisema hatua hiyo hailengi kudhibiti sehemu hiyo bali ni kwa ajili ya kulinda maslahi ya kimsingi ya wakazi wa huko. Russia pia iliishutumu Georgia kwa kupeleka silaha, nishati, chakula na zana za kijeshi kwenye bonde la Kodori la Abkhazia, na kukusanya wanajeshi wake na kufanya maandalizi kwa ajili ya operesheni ya kijeshi. Waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergey Lavrov aliishutumu Georgia kwa kujaribu kutatua kwa nguvu masuala ya Abkhazia na Ossetia Kusini.
Katika muda mrefu uliopita Russia na Georgia zimekuwa zikipambana katika masuala ya Abkhazia na Ossetia Kusini. Abkhazia ni Jamhuri inayojitawala nchini Georgia, ilijitangazia uhuru mwaka 1992 na kupambana na serikali kuu ya Georgia. Mapambano hayo yalipomalizika mwaka 1993, ujumbe wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa uliingia na kukaa kwenye sehemu hiyo, na Russia pia ilituma kikosi cha kulinda amani kukaa kwenye sehemu hiyo. Ossetia Kusini ni jimbo moja nchini Georgia, ambalo linapakana na Ossetia Kaskazini. Baada ya kusambaratika kwa Urusi ya zamani, Ossetia Kusini ilianza kuipinga serikali kuu ya Goergia.
Mwaka 1992 pande nne za Russia, Georgia, Ossetia Kusini na Ossetia Kaskazini ziliunda kamati ya mseto ya kusimamisha mapambano, na pande tatu za Russia, Georgia na Ossetia Kusini zilianzisha kikosi cha kulinda amani katika sehemu zenye mapambano. Russia haijatambua uhuru wa Abkhazia na Ossetia Kusini, lakini sehemu hizo mbili zinaungwa mkono na Russia katika mambo ya kiuchumi na kidiplomasia. Ndiyo maana masuala hayo yamekuwa yakisumbua mara kwa mara uhusiano kati ya Russia na Georgia.
Wachambuzi wanadhihirisha kuwa, kuzuka tena kwa hali ya wasiwasi kati ya Russia na Georgia hivi karibuni kunahusiana na tukio la kujitangaza uhuru kwa Kosovo mwezi Februari mwaka huu. Baada ya tukio hilo, kulikuwa na habari kuwa, Russia itatambua uhuru wa Ossetia Kusini na Abkhazia kama hatua ya kulipiza kisasi kwa nchi za Ulaya na Marekani ambazo zinaunga mkono uhuru wa Kosovo. Mwezi Machi mwaka huu, Russia iliweka vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi wa urais wa Russia katika sehemu hizo mbili bila kuiarifu Georgia, hatua hiyo ilikuwa changamoto dhidi ya mamlaka ya Georgia, na kuleta hali ya wasiwasi katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambao ulikuwa umeanza kuboreshwa.
Masuala ya Abkhazia na Ossetia Kusini yanahusiana na mamlaka ya Georgia na ukamilifu wa ardhi wa nchi hiyo, kwa uhakika Georgia itafanya kila iwezalo kulinda maslahi yake nyeti. Na kwa upande wa Russia, ni vigumu kwake kuziacha sehemu hizo mbili kutokana na sababu za kihisia. Kwa hiyo masuala hayo yamebadilika kuwa tatizo sugu katika uhusiano kati ya Russia na Georgia. Mbali na hayo nchi hizo mbili zina mikwaruzano mingine katika masuala ya Georgia kujiunga na jumuiya ya NATO na Russia kujiunga na shirika la biashara duniani WTO. Ingawa hivi karibuni uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa umeboreshwa kiasi, hata hivyo kutokana na kuwepo kwa uhasama mkubwa sana, hali ya wasiwasi inaweza kurudi hata kama tukio lolote dogo likitokea.
|