Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-05 20:23:24    
Jumba la makumbusho la Hanyangling

cri

Kwenye sehemu ya kaskazini ya mji wa Xian, mji mkuu wa mkoa wa Shanxi, kuna makaburi mengi ya wafalme wa enzi ya kale ya Han ya Magharibi, kati ya makaburi hayo makaburi ya Hanyangling yamekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1,200. Hivi sasa kwenye makaburi ya Hanyangling ya enzi ya Han, limejengwa jumba la makumbusho, ambalo ni jumba la kwanza la kisasa lililojengwa chini ya ardhi nchini China. Ukiingia kwenye makaburi ya Hanyangling, unaweza kuona uwanja mkubwa wenye majani na miti mingi, kaburi kubwa la mfalme na kaburi kubwa la mke wa mfalme yanatazamana kwa mbali.

 

Eneo la makaburi ya Hangyangling ni kiasi cha kilomita 20 za mraba. Enzi ya mfalme ya Han ya Magharibi ya kale ni enzi ya pili ya kifalme ya nchini China, katika enzi hiyo kulikuwa na wafalme 11. Mtoa maelezo kwenye jumba la makumbusho la Hangyangling, Bi. Zhang Bei alituambia kuwa makaburi ya Hanyangling yalijengwa kwa ajili ya Liu Qi, yaani mfalme Jing wa nne wa enzi ya Han ya Magharibi. Bi Zhang Bei alisema,

"Makaburi ya Hanyangling yalijengwa katika mwaka wa nne baada ya Liu Qi kurithi ufalme, mfalme Jing alifariki baada ya miaka 12 kupita, ujenzi wa makaburi ulisimamiwa na Liu Che, mtoto wa mfalme Jing na mke wa mfalme kwa pamoja, na ujenzi wa makaburi uliendelea kwa miaka 28."

Kwenye eneo la makaburi ya Hangyangling kuna makaburi karibu elfu moja yaliyojengwa baada ya kifo cha mfalme Jing, hivi sasa makaburi 190 kati ya hayo yamefukuliwa. Kwa kufuata njia inayokwenda chini ya ardhi, mashimo mengi yaliyofukiwa sanamu za watumishi yanaonekana mbele. Huu ni ukumbi wa maonesho ya vitu vilivyofukiwa nje ya shimo la jeneza la mfalme, na ni wenye kivutio kikubwa zaidi kwenye makaburi ya Yangyangling. Bi. Zhang Bei anawaongoza watalii kuangalia maonesho kwa kupitia vioo vilivyowekwa kwenye ujia, huku akisema mashimo yaliyofukiwa vitu yote ni mashimo ya mstatili yaliyochimbwa kutoka upande wa mashariki kwenda upande wa magharibi, kila shimo lina kina cha mita 3 na upana wa mita 2.4, na kila shimo lina sanamu nyingi za udongo wa ufinyanzi. Bi Zhang Bei alisema,

"Sanamu zilitengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi, kisha ziliwekwa mbavu za mbao, mavazi ya sanamu hizo yalitengenezwa kwa vitambaa vya hariri, pamba, kitani na ngozi, sanamu hizo zinafanana na za aina mbalimbali kwa ajili ya mfalme Jing katika dunia nyingine."

Bi. Zhang Bei alisema jeshi hilo la sanamu zilizozikwa wakati mfalme Jing alipofariki, ni kundi kubwa la sanamu zilizozikwa pamoja na maiti ya mfalme baada ya sanamu za farasi na askari za Qinshihuang, mfalme wa kwanza wa enzi ya Qin. Tofauti na sanamu za mfalme Qinshihuang zenye sura za ukakamavu, sura za sanamu zilizofukuliwa kwenye makaburi ya Hanyangling zina sura ya uchangamfu na furaha.

Naibu mkurugenzi wa jumba la makumbusho la Hangyangling, Bw. Yan Xinzhi alisema, hii inahusiana na hali halisi ya wakati ule iliyokuwa ni jamii yenye masikilizano. Nchi hiyo ilikuwa na neema na utulivu. Kwa hiyo mafundi walipofinyanga sanamu waliweka hisia zao katika nyuso za sanamu wakati walipozitengeneza. Bw. Yan Xinzhi alisema:

 

"Sanamu hizo ni tofauti na sanamu zile za askari na farasi za enzi ya Qin, sisi tunaweza kufahamu vizuri zaidi kuhusu utamaduni wa kale wa China, sanamu za enzi ya Qin zinaonesha ukakamavu, lakini sanamu za Yangling ya enzi ya Han zinaonesha upole."

Haya, lakini sanamu hizo zilitengenezwa wapi? Katika uchunguzi kuhusu mabaki ya mji wa Changan wa enzi ya Han karibu na makaburi ya Hanyangling, zilifukuliwa sampuli nyingi za kutengenezea sanamu za mfinyanzi, hii inadhihirisha kuwa baada ya sanamu hizo kutengenezwa katika mji wa Changan, zilipelekwa kwenye makaburi ya Hanyangling na kuzikwa huko.

Utengenezaji wa sanamu za mfinyanzi za makaburi ya Hanyangling ilikuwa ni kazi kubwa. Mtoa maelezo kwenye jumba la makumbusho la Hanyangling, Bi. Zhang Bei alisema,

"Kazi za utengenezaji ilikuwa ni pamoja na kuchukua udongo wa mfinyanzi, kukanda udongo uliotiwa maji, kufinyanga sanamu, kuchoma moto, kutia rangi sanamu, na kuzivalisha nguo. Udongo uliochukuliwa ni udongo safi wa mfinyanzi, hakuwa laini sana na wala haukuwa mgumu sana, sampuli za kutengenezea sanamu hizo ni za sehemu nne za kichwa, mwili, mapaja na miguu, kisha sehemu hizo nne za sanamu ziliunganishwa pamoja, pua na masikio ya sanamu pia zilitengenezwa kwa sampuli, kisha ziliunganishwa kwenye kichwa cha sanamu, baada ya hapo, fundi alichonga michoro ya kuonesha hisia za sanamu kwenye uso wake ili mradi kila sanamu iwe na uso wake tofauti na wa sanamu nyingine, mwishoni aliivalisha mavazi tofauti kwa kulingana na hadhi yake."

Mbali na sanamu, pia zilifukuliwa vitu vingine kwenye makaburi ya Hanyangling vikiwa ni pamoja na vyombo vinavyotumiwa na watu katika maisha, silaha, vitambaa na nafaka. Kutokana na vitu vilivyofukuliwa na utaratibu wa mazishi wa kale, tunaweza kusema kuwa huko vilizikwa vitu vingi vya kiutamaduni, ambavyo ni hazina yenye thamani kubwa. Uzalishaji mali katika enzi ya Han uliendelea sana, vitu vingi visivyofahamika vilivyozikwa vitaonesha vilivyo hali halisi ya ustawi ya enzi ya Han ya zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Bi. Zhang Bei alisema,

"Handaki hilo la chini lenye urefu wa mita 94 ni refu zaidi kati ya mahandaki kumi yanayoweza kutembelewa na watu, handaki hilo linafika hadi kwenye eneo hili linalotukabili, tunaweza kuona mistari mitatu ya maghala yaliyotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi, yale kwenye mstari wa kushoto kabisa bado hayajafunguliwa, yale ya mistari miwili mingine yamefunguliwa na yamevunjika, tunaweza kuona nafaka zilizomwagika zikiwemo uwele, mtama, shayiri na ngano."

Vitu vilivyozikwa kwenye mashimo nje kwenye makaburi ya Hangyangling ni vingi na vya aina nyingi sana, na vinawavutia watu. Vitu vilivyokwishafukuliwa kwenye makaburi ya Hanyangling vingi zaidi ni kutoka kwenye mashimo mengine ya vitu vilivyozikwa wakati mfalme Jing alipofariki dunia, endapo vitu vyote vilivyozikwa vitafukuliwa, kwa uchache kabisa itachkua muda wa miaka 150. Watafiti wa mabaki ya kiutamaduni ya kale walipofukua vitu kwenye sehemu hiyo, walijitahidi kuhifadhi sura ya mazingira ya makaburi ya Hanyangling, na kutojenga majengo yoyote juu ya ardhi, na walijenga jumba la makumbusho chini ya ardhi. Bi Zhang Bei alisema,

 

"Mashimo yote yenye vitu vilivyozikwa kwenye jumba la makumbusho la chini ya ardhi yamehifadhiwa kwa vioo, hali joto ya sehemu ya ndani ya mashimo hayo yanayotenganishwa kwa vioo ni nyuzi 23 au 24 hivi, unyevunyevu wake unadhibitiwa kati ya 95% hadi 99%, lakini unyevunyevu wa nje ni 50% tu."

Wakati tunapoangalia makaburi ya Hanyangling kwa mitazamo mbalimbali na kwa karibu kwenye ujia uliotenganishwa kwa vioo, tunaweza kuhisi maisha kwenye kasri ya mfalme wa enzi ya Han ya Magharibi, tena tunaweza kufahamu kazi za kufukua mabaki ya kale na ufufuaji wa vitu vya kiutamaduni vya zamani.