Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-06 19:29:23    
Kimbunga chasababisha hasara kubwa nchini Myanmar

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Myanmar tarehe 5 alipozungumza na wanadiplomasia alisema, kimbunga cha kitropiki kilichokumba Myanmar kimesababisha vifo vya watu wasiopungua elfu 15, na idadi hiyo pengine itaongezeka kadiri shughuli za uokoaji zinavyoendelea.

Kimbunga hicho kilichopewa jina la Nargis hapo mwanzo kilikuwa kinaelekea Bangladesh, lakini tarehe pili kilipofika kwenye Ghuba ya Bengal ghafla kiligeukia Myanmar. Kimbunga hicho pamoja na mvua kali kiliingia kwenye ardhi ya Myanmar kutoka kwenye delta ya mto Irrawaddy kilomita 220 kutoka Rangoon, kisha kikazikumba delta za Rangroon na Irrawaddy. Kasi ya kimbunga hicho ilikuwa kilomita 190 hadi 240 kwa saa. Mkoani Irrawaddy tu watu waliokufa na kujeruhiwa walifika elfu 11.

Kimbunga hicho kiliharibu majengo mengi na kusababisha watu wengi kupoteza makazi, kwenye kisiwa cha Hai Gyi mkoani Irrawaddy watu laki moja wamepoteza makazi, na kimbuga hicho kimesababisha umeme, maji na mawasiliano ya habari kukatika, na sasa upungufu wa maji ya kunywa ni mkubwa. Serikali ya Myanmar imeorodhesha sehemu ya Rangroon, mkoa wa Pegu, jimbo la Mon na Jimbo la Karen kuwa ni sehemu zilizoathiriwa vibaya zaidi.

Hivi sasa serikali ya Myanmar imeanzisha kamati ya kupambana na maafa inayoongozwa na waziri mkuu Bw. Thein Sein na vikundi 10 vya uongozi wa shughuli za kupambana na maafa. Ofisa mmoja wa Wizara ya Habari alisema serikali imetuma wanajeshi kushiriki kwenye shughuli za uokoaji na Chama cha Msalaba Mwekundu kimeanza kuwahudumia waathirika kwa kuwapa vifaa vya kimaisha.

Rangroon iliwahi kuwa mji mkuu wa Myanmar, hivi sasa ni kituo cha uchumi, mji huo umeathrika vibaya sana. Uwanja wa ndege mjini humo ambao uliwahi kufungwa, tarehe 5 umeanza kufanya kazi tena, takataka za barabarani zinasafishwa na baadhi ya sehemu zimerudisha mawasiliano ya habari, lakini huduma za umeme na maji bado hazijarudishwa.

Kimbunga hicho kilianza kuelekea kaskazini mashariki kuanzia tarehe 4 jioni na kasi ya upepo imepungua. Kwenye sehemu ya kaskazini ya Thailand mvua kubwa inaendelea kunyesha, idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Thailand imetangaza kuwa pengine kimbunga hicho kitaleta mafuriko makubwa katika sehemu za kaskazini, mashariki na ya katikati nchini Thailand.

Hali ya maafa nchini Myanmar inafuatiliwa sana na jumuyia ya kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon tarehe 5 alisema Umoja wa Mataifa utajitahidi kutoa misaada kwa Myanmar, na alisema mkurugenzi wa ofisi yake Bw. Vijay Nambiar amekutana na balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa na kujadili namna ya kuisaidia Myanmar. Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa tarehe 5 lilituma wataalam nchini Myanmar kutathmini hali ya maafa. Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa pia limetuma tani 500 za chakula kwa nchi hiyo. Licha ya hayo, idara husika za Umoja wa Mataifa zimekuwa zikiweka mpango wa kuomba jumuyia ya kimataifa itoe misaada.

Waziri ya mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi tarehe 4 alimtumia salaam za pole kwa waziri wa mambo ya nje wa Myanmar Bw. U Nyan Win. Kamati ya Umoja wa Ulaya tarehe 5 imetangaza kutoa msaada wa Euro milioni mbili kuwasaidia waathirika wa Myanmar.

Ubalozi wa Marekani nchini Myanmar pia umetoa msaada wa dharura kupitia Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa. Msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Scott Stanzel tarehe 5 alisema Marekani imekuwa ikifikiria kutoa msaada zaidi kwa nchi hiyo. Serikali ya India pia ilituma salaam za pole kwa serikali na watu wa Myanmar na kusema kwamba itatoa misaada. Wizara ya Mambo ya Nje ya Thailand imetoa msaada wa dola za Marekani elfu 50, jeshi la Thailand limetoa msaada wa dawa na chakula utakaopelekwa huko tarehe 6.