Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-07 20:36:08    
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yatoa misaada kwa Myanmar

cri
Tarehe 2 na 3 Myanmar nchi iliyopo kusini mashariki mwa Asia ilikumbwa na kimbunga cha kitropiki kilichopewa jina la "Nargis" na kusababisha hasara kubwa za mali na vifo vya watu wengi. Ili kufanya uokoaji baada ya maafa hayo yaliyotokea ghafla mashirika husika ya Umoja wa Mataifa yameanza kutoa misaada kwa juhudi. huko Geneva nchini Uswisi, kuna makao makuu ya mashirika zaidi ya kumi ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na Shirika la Afya Duniani WHO, Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF, Shirika la Wakimbizi UNHCR, Ofisi ya uratibu wa Mambo ya Kibinadamu OCHA na sekretarieti ya mkakati wa kupunguza Maafa ISDR. Tarehe 6 asubuhi kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Geneva wajumbe wa mashirika hayo walitangaza hatua zitakazochukuliwa haraka kuisaidia Myanmar.

Ofisi ya uratibu wa Mambo ya Kibinadamu OCHA ni shirika muhimu katika shughuli za uokoaji za Umoja wa Mataifa, msemaji wa ofisi hiyo Bi. Elisabeth Byrs kwenye mkutano huo alisema,

"Mara tu baada ya maafa kutokea, Umoja wa Mataifa umekuwa ukiwasiliana na serikali ya Myanmar na kujadiliana Umoja wa Mataifa unavyoweza kutoa mchango mkubwa zaidi katika shughuli za uokoaji wa maafa. Serikali ya Myanmar inaomba jumuyia ya kimataifa itoe misaada ikiwa ni pamoja na mahitaji ya haraka ya mahema, vyandarua, maji ya kunywa na chakula."

Imefahamika kwamba baada ya maafa kutokea, mashirika husika ya Umoja wa Mataifa yalifanya mjadala wa dharura na kugawa majukumu kwa kila shirika. UNICEF inawajibika kuwasaidia waathirika maji ya kunywa, huduma ya matibabu, kuwapangia malazi watoto na wanawake; WHO inawajibika kutoa huduma ya dawa na kazi ya kukinga magonjwa ya kuambukiza; UNHCR inawajibika kutoa huduma ya mahema; Shirika la Chakula na Kilimo linawajibika kupeleka chakula na kusimamia usalama wa chakula; Shirika la Mpango na Maendeleo linawajibika kusaidia ukarabati ambao unatoa kipaumbele katika kurudisha mawasiliano ya habari. Msemaji wa UNICEF Bi. Veronique Taveau alionesha wasiwasi kuhusu hali ya watoto na wanawake walioathirika. Alisema,

"ingawa kwa sasa bado ni vigumu kufahamu watoto na wanawake wangapi walioathirika, lakini inakadiriwa kuwa wanachochukua 60% ya waathirika wote, Cha kusikitisha na kutia wasiwasi ni kwamba mpaka sasa idadi ya watu waliokufa inaendelea kuongezeka."

Msemaji wa WHO Bi. Fadela Chaib alisema, hivi sasa cha muhimu ni kuzuia mpuliko wa magonjwa ya kuambukiza. Alisema,

"Kwa kawaida ugonjwa wa kuharisha hutokea baada ya maafa kutokea, ugonjwa huo unasababishwa na maji machafu, kwa hiyo suala la maji ya kunywa lazima lipewe uzito. Zaidi ya hayo, baadhi ya sehemu zilizoathirika ni maeneo yanayoshamiri malaria, kinga ya ugonjwa huo ni kuwapatia waathirika vyandarua. Hivi sasa kikundi cha wataalamu kipo huko kushughulika  kinga hiyo."

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, delta ya mto Irrawaddy ni sehemu iliyoathiriwa vibaya zaidi, kiasi cha hasara yake hata kinalingana na tsunami iliyotokea mwaka 2004 katika sehemu ya kusini mashariki ya Asia. Msemaji wa sekrekarieti ya mkakati wa kupunguza maafa ya Umoja wa Mataifa ISDR Bi. Leoni alisema maafa ya kimbunga hicho kwa mara nyingine tena yanawaonesha watu umuhimu wa kukamilisha mfumo wa tahadhari  ili kuzuia maafa na kupunguza vifo vya watu. Alisema,

"Mafuriko hayo makubwa yamesababisha vifo vya watu wengi, na baadhi ya wakazi hawakuwa na muda wa kukimbilia kwenye sehemu zenye salama. Nchi za Japan, Cuba na Bangladesh zimekuwa na mfumo kamili wa kutoa tahadhari ambao unaweza kupunguza vifo vya watu kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo kukamilisha mfumo huo ni kazi muhimu katika juhudi za kupunguza maafa."

Idhaa ya kiswahili 2008-05-07