Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-08 15:56:01    
Moja ya mbinu 36: Kuondoa ngazi baada ya kupanda kwenye chumba cha ghorofani

cri

Mbinu ya "kuondoa ngazi baada ya kupanda kwenye chumba cha ghorofani" ni moja ya mbinu 36 katika kitabu cha kale cha mbinu za kivita nchini China.

Jina la mbinu hiyo lilipatikana kutoka kwenye hadithi moja ya mshauri maarufu wa mambo ya kijeshi wa China ya kale Bw. Zhu Geliang. Hadithi yenyewe inaeleza hivi: Katika karne ya pili, jemadari mmoja hodari aliyeitwa Liu Biao alimpendelea zaidi mtoto wake mdogo Liu Qi na hakumpenda mtoto wake mkubwa Liu Zong, watoto hao wawili hawakuzaliwa na mama mmoja. Mama mzazi wa mtoto mkubwa Liu Zong alihofia sana mtoto wake atakuwa hatarini baada ya mtoto mdogo Liu Qi kurithi kiti cha baba yake. Mtoto mdogo Liu Qi alifikiri kuwa, ingawa baba yake alimpenda lakini kikawaida kiti cha baba yake kinarithiwa na mtoto wake mkubwa, hata angerithi kiti hicho pengine hali yake isingekuwa salama. Bw. Zhu Geliang alikuwa ni mtu mashuhuri kwa kutoa ushauri wa kivita, Liu Qi mara nyingi aliomba ushauri kutoka kwake lakini alikataa. Siku moja Liu Qi alimwalika Zhu Geliang kwenye chakula katika jumba moja lenye ghorofa. Baada ya kupanda kwenye chumba cha ghorofa, Zhu Geliang aligundua kwamba ngazi ya kupandia imeondolewa. Liu Qi akamwambia Zhu Geliang "Sasa unaweza kuniambia chochote unachotaka kusema kwani wengine hawawezi kusikia, nipe ushauri wako." Zhu Geliang alifahamu kwamba bila kutoa ushauri hawezi kushuka na kuondoka, akamweleza hadithi moja kwa kumwamsha kiakili, aondoke mahali penye matata. Liu Qi alielewa maana ya hadithi hiyo, akarudi nyumbani na kuomba baba yake ampeleke kwenye sehemu nyingine kuilinda, akaondoka kutoka kwa mama yake wa kambo na akakwepa janga.

Sababu ya Liu Qi kumwalika Zhu Geliang kula chakula kwenye chumba cha ghorofani ilikuwa ni kwa ajili ya kupata ushauri, na kuondoa ngazi ilikuwa ni kwa ajili ya kumwondolea Zhu Geliang wasiwasi. Kwenye kitabu cha mbinu 36 za kivita, mbinu hiyo inaelezwa kwamba katika mapambano dhidi ya maadui kuna haja kuwachochea na kuwavutia maadui waingie wenyewe kwenye sehemu yako uliyoiacha kwa makusudi, kisha ufunge njia yao ya kupata msaada na kuwaangamiza. Ingawa mbinu hiyo ya kuwaingiza maadui ndani ya mfuko wako uliowatayarishia ni nzuri lakini maadui si wajinga, kwa hiyo ngazi ambayo ni kama kishawishi cha kuwarubuni ni ya lazima kabla ya kutimiza lengo lako. Baada ya maadui kupanda kwenye "chumba cha ghorofani" yaani wamekwisha ingia ndani ya mfuko wako uondoe "ngazi" ili wasiweze kutoka na kisha uwaangamize.

Mbinu hiyo inaelezwa kwamba "ngazi" hiyo ina aina nyingi, kwa maadui wenye uchoyo uwavutie kwa faida kubwa; kwa maadui wenye kiburi uwavutie kwa unyonge wako; kwa maadui wenye ujasiri na wasio na busara utumie mtego wa kuficha askari wako. Kwa ufupi, "ngazi" hiyo uitumie kwa mujibu wa hali ya maadui wako. Jambo ambalo linapaswa kuelezwa hapa ni kwamba, wewe jemadari pia unaweza kutumia mbinu hiyo ya kuondoa "ngazi" kwa askari wako na kuwalazimisha wawashinde maadui bila kuwa na njia nyingine. Mfano wa kutumia mbinu hiyo ni kama ufuatao.

Mwishoni mwa karne ya tatu, jemadari Han Xin alipigana vita huku na huko kwa ajili ya mfalme wake Liu Bang. Mwaka mmoja jemadari Han Xin alipambana na jeshi la mfalme Zhao lenye askari zaidi ya laki mbili, lakini Han Xin alikuwa na askari elfu kumi kadhaa tu, kwa hiyo kama angepambana na maadui uso kwa uso angeshindwa. Baada ya kutafakari Han Xin alijipatia mbinu, kwamba alituma askari wake elfu kumi kwenye mahali penye mto mkubwa nyuma ya askari hao na kuwachokoza maadui, yeye mwenyewe aliongoza askari elfu nane kuwadanganya maadui kama kweli anataka kupambana nao uso kwa uso, na huku alituma askari elfu mbili kuwanyemelea maadui kisiri siri kupitia njia za vichakani na kujificha karibu na kambi ya maadui wakisubiri kuingia ndani ya kambi na kupandisha bendera ya Han Xin.

Alfajiri ya siku ya pili, Han Xin aliongoza askari wake kufanya mashambulizi, pande mbili zilipambana vikali lakini punde si punde askari wa Han Xin walijidai kuzidiwa na maadui wakarudi kwenye ukingo wa mto, maadui walifurahi wakatoka wote kambini kuwafukuza askari wa Han Xin. Wakati huo Han Xin aliwaambia askari wake kwamba mbele yao kuna mto mkubwa, nyuma yao ni maadui laki mbili, hakuna njia nyingine zaidi ya kupambana na maadui na kuwashinda. Askari walipoona kwamba hawana njia ya kusalimisha uhai walipambana na maadui kwa nguvu zote. Sambamba na hayo askari waliojificha karibu na kambi ya maadui waliingia kwenye kambi iliyokuwa tupu na kupandisha bendera nyingi za jeshi la Han. Maadui walipoona hayo walikimbia ovyo na mwishowe waliangamizwa wote.

Katika hadithi hiyo, kuteka kambi ni kama kuondoa ngazi bila kuwawezesha maadui kurudi tena, kwa upande mwingine kuwapanga askari wake kwenye mahali ambapo nyuma yao ni mto mkubwa, pia ni kama kuondoa ngazi yao, kwani walikuwa hawana njia nyingine ila tu kupambana na maadui kufa na kupona.

"Mbinu ya kuondoa ngazi baada ya kupanda kwenye chumba cha ghorofani" pia mara kwa mara inatumika maishani kwa lengo la kuwalazimisha wapinzani wakubali masharti na kutimiza lengo unalotaka.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-08