Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-08 16:33:30    
Mjapan Bw. Kobori Shogo anayeishi nchini China

cri

Bw. Kobori Shogo ana umri wa miaka 60, hivi sasa yeye ni naibu meneja mkuu wa kiwanda cha kutengeneza mashine nchini China, ambacho ni tawi la kampuni moja ya Japan. Aliwasalimia wasikilizaji wa Radio China Kimataifa kwa lugha ya Kichina. Akisema "Hamjambo wasikilizaji. Mimi ninaitwa Kobori Shogo, leo nimefurahi sana. Asanteni."

Nchini China wanaume wanaweza kustaafu wanapotimiza umri wa miaka 60, hata hivyo Bw. Kobori Shogo bado anaonekana ni mwenye ari kubwa. Kiwanda hicho kiko Yinchuan, mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui wa Ningxia, magharibi mwa China, ni tawi la kampuni moja ya Japan, ambayo iliwekeza vitega uchumi na kujenga kiwanda cha kutengeneza mashine nchini China miaka minane iliyopita. Wakati huo huo kampuni hiyo ya Japan ilimtuma Bw. Kobori Shogo nchini China ashughulikie uanzishwaji wa kiwanda hicho.

Bw. Kobori Shogo alieleza kuwa katika muda wa miaka minane iliyopita, kampuni kuu ya Japan imekuwa ikiendelea kuongeza uwekezaji kwenye kiwanda hicho mkoani Ningxia, na kuongeza uwekezaji katika sehemu nyingine za China. Alisema  "Kiwanda hicho kimefanyika upanuzi kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2005, 2006 na 2007. Baada ya kukamilika kwa miradi hiyo ya upanuzi, kampuni itazidi kuongeza uwekezaji. Mbali na hayo kampuni yetu imeanzisha kituo cha kuonesha teknolojia mjini Shanghai, China mwezi Januari mwaka 2008. Ninaamini kuwa uwekezaji wa namna hii utaongezeka."

Bw. Kobori Shogo alitoa maoni yake kuwa, kampuni za kimataifa kuongeza uwekezaji nchini China kunatokana na kuwa na imani kubwa na ongezeko la kudumu la uchumi wa China. Bw. Kobori Shogo alisema kitu kinachogusa sana hisia zake ni kwamba, kila mara aliposafiri kwenda China kutoka Japan, zawadi alizonunua nchini Japan zina chapa isemayo "made in China", alisema hii inaonesha nguvu kubwa ya bidhaa za China. Bw. Kobori Shogo alisema  "Ninaamini kuwa China itavutia vitega uchumi vingi zaidi kutoka nje, na walimwengu watakuwa na matarajio makubwa zaidi kwa soko la China. Katika nchi zote duniani, ni China pekee inayoweza kudumisha mwelekeo huo wa maendeleo. Naona mustakabali ni mzuri sana badala ya giza."

Katika muda wa miaka minane iliyopita alipoishi nchini China, Bw. Kobori Shogo alijionea jinsi mambo ya uchumi na jamii yalivyoendelezwa na maisha ya watu yalivyoboreshwa. Alisema alishuhudia jinsi kiwango cha maisha ya wafanyakazi wa kiwanda chake yalivyoinuka. Bw. Kobori Shogo alisema "Ninaona wafanyakazi wa kiwanda chetu wamekuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi, kwa mfano wa harusi, wafanyakazi wengi wa kiwanda chetu wana uwezo wa kununua nyumba na kuandaa sherehe za harusi. Katika miaka ya hivi karibuni, kiwanda chetu kimepata maendeleo makubwa, na vipato vya wafanyakazi wetu pia vimeongezeka kwa mfululizo."

Bw. Kobori Shogo amezoea maisha hapa nchini China. Alisema  "Hakuna tofauti kubwa kati ya maisha nchini Japan na yale ya hapa Yinchuan. Nyumbani nchini Japan niliweza kupata matunzo ya ndugu, lakini hapa nina uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzangu, ambao wananisaidia sana kama walivyofanya ndugu zangu."

Katika mahojiano na mwandishi wetu wa habari, Bw. Kobori Shogo alitaja mara kwa mara methali moja ya Kichina, yaani "unapokunywa maji usisahau waliochimba kisima", maana ya methali hiyo ni kuwataka watu wasisahau wengine wanaotoa msaada. Bw. Kobori Shogo alisema hii ni uelewa aliopata katika miaka minane iliyopita aliyoishi nchini China, juu ya maadili ya watu wa China. Alisema "Wachina wanasema 'unapokunywa maji usisahau waliochimba kisima'. Methali hiyo ilinipa kumbukumbu imara, kwani naona tabia ya watu wa China ni kama ilivyosema methali hii ya China."

Mjapan huyo Bw. Shogo alieleza kuridhika na maisha yake kwa hivi sasa. Zaidi ya hayo alimwambia mwandishi wetu wa habari matumaini yake kuwa, mawasiliano ya kirafiki kati ya China na Japan yataweza kufanyika bila matatizo mara kwa mara, na nchi hizo mbili zitaweza kusameheana visa. Alisema  "Naona suala la visa litatatuliwa vizuri wakati michezo ya Olimpiki mjini Beijing. Hadi kufikia mwaka 2006 watu wa Japan walipokuja China, walitakiwa kuomba visa, na mwaka 2007 sharti hilo lililegezwa katika baadhi ya miji ya China, kwa mfano miji ya Shanghai na Guangzhou, wajapan sasa wanaweza kuitembelea miji hiyo bila kuomba visa. Ninaamini kuwa kutokana na kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Japan, mawasiliano kati ya nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali pia yataendelea vizuri."

Idhaa ya kiswahili 2008-05-08