Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-09 16:30:12    
Vladimir Putin ashika wadhifa wa waziri mkuu wa Russia

cri

Rais Dmitry Medvedev wa Russia tarehe 8 alisaini amri ya kumteua Bw. Vladimir Putin kuwa waziri mkuu wa serikali mpya ya Russia. Hii ni mara ya pili kwa Bw. Putin kushika wadhifa huo tangu mwaka 1999.

Kutokana na kuapishwa kwa Bw. Medvedev kuwa rais na Bw. Putin kuwa waziri mkuu, siasa za Russia zimeingia kwenye kipindi kipya. Hivi sasa hali ya siasa na uchumi nchini Russia imeonesha mwelekeo unaowatia moyo watu, lakini wachambuzi wanaona serikali mpya itakayoongozwa na waziri mkuu Putin itakabiliwa na changamoto mbalimbali katika juhudi za kutimiza malengo makubwa ya maendeleo ya kimkakati ya Russia kabla ya mwaka 2020 yaliyotolewa na Bw. Putin.

Changamoto ya kwanza ni mfumuko wa bei. Katika miaka ya hivi karibuni, kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta kumesababisha kuwepo kwa kiwango cha juu cha mfumuko wa bei katika nchi mbalimbali ikiwemo Russia. Mwaka 2007 mfumuko wa bei nchini Russia ulifikia asilimia 11.9, kiwango ambacho ni juu ya asilimia 8 iliyokadiriwa na serikali. Katika miezi minne ya kwanza mwaka huu, kiwango hicho kilifikia asilimia 6.3. Kwa mujibu wa makadirio mapya yaliyofanywa na benki kuu ya Russia, wizara ya fedha na wizara ya maendeleo ya uchumi na biashara za nchi hiyo, kiwango hicho kitaweza kufikia asilimia 10 mwaka 2008. Wachambuzi wanaona hali halisi ya mfumuko wa bei huenda ni mbaya zaidi kuliko asilimia iliyotangazwa na serikali. Kutokana na uchunguzi wa maoni ya raia uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya Levada ya Russia, asilimia 62 ya watu wa Russia wanaona serikali mpya inatakiwa kutoa kipaumbele kwa kazi ya kuzuia mfumuko wa bei, na kupunguza bei za vitu.

Changamoto ya pili ni mageuzi ya sekta za huduma za jamii. Katika miaka minane iliyopita rais Putin alipokuwa madarakani, alijaribu kufanya mageuzi kadhaa katika sekta za huduma za jamii. Lakini kasi ya mageuzi hayo ilipungua dhahiri baada ya mageuzi kukumbwa na matatizo mbalimbali mwaka 2005. Hata hivyo huduma za jamii zinahusu moja kwa moja maslahi ya wananchi, matatizo ya sekta hizo yakishindwa kutatuliwa ipasavyo, yanaweza kukwamisha maendeleo endelevu ya jamii na uchumi. Baadhi ya wataalamu wanaona kuwa, Bw. Putin ni hodari katika mambo ya uchumi, lakini kutokana na taaluma yake na uzoefu wake wa kisiasa, ana udhaifu kwenye utekelezaji wa mageuzi ya sekta za huduma za jamii. Ndiyo maana suala hilo la mageuzi ya sekta za huduma za jamii ni changamoto nyingine kubwa itakayoikabili serikali ya Putin.

Changamoto ya tatu ni kubadilisha miundo ya uchumi. Katika muda mrefu Russia imekuwa inategemea kusafirisha nje raslimali ilizo nazo, hali hii inafanya uchumi wa Russia usiwe na aina mbalimbali za uchumi zinazoweza kuchangia ongezeko la uchumi, na kuifanya ikabiliwe na hatari ya kuyumba kwenye mchakato wa utandawazi wa biashara duniani. Miundo hiyo ya uchumi isiyofaa ni tatizo sugu linalokwamisha maendeleo ya uchumi wa Russia. Katika juhudi za kutatua suala hilo, Russia iliweka malengo ya kimkakati ya kuendeleza kwa pande zote uchumi wa uvumbuzi. Hata hivyo wataalamu wanasema, hivi sasa uchumi wa Russia bado unaendelezwa kwa kufuata njia ya kuuza nje nishati na mali ghafi, ni vigumu kupata njia mpya ya uvumbuzi baada ya mwaka 2010, na kama malengo hayo yanaweza kutimizwa pia inategemea utekelezaji mwafaka wa hatua mbalimbali za mageuzi katika sekta za elimu, sayansi na teknolojia pamoja na afya.

Mbali na hayo kupambana na ufisadi na kuinua ufanisi wa serikali vile vile ni masuala magumu yatakayoikabili serikali ya Putin.

Wachambuzi wanasema, katika miaka minane iliyopita Putin aliposhika madaraka ya urais, alifufua uchumi wa Russia kwa kutegemea kuuza nje mafuta, na hivi sasa waziri mkuu Putin anakabiliwa na mtihani mgumu zaidi wa kuinua kiwango cha uchumi wa Russia kwa kutegemea uchumi wa uvumbuzi.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-09