Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-12 14:52:49    
Mwimbaji maarufu wa Tibet bibi Cedai Drolma

cri

Bibi Cedai Drolma alizaliwa mwaka 1937 kwenye familia moja maskini ya wakulima watumwa. Miaka zaidi ya 50 iliyopita, Tibet ilikuwa inatekeleza mfumo wa wakulima watumwa, na asilimia zaidi ya 95 ya watibet walikuwa watumwa. Wakati huo masufii wa ngazi ya juu na makabaila wachache walikuwa wanamiliki mali zote za Tibet, na hata wakulima watumwa pia ni mali yao ya binafasi. Katika lugha ya kitibet, maana ya Cedai ni maisha mazuri na marefu, lakini kabla Tibet haijakombolewa, maisha ya bibi Cedai Drolma yalikuwa magumu, na familia yake ilifanya kazi kwa makabaila kwa kuduma maisha. Bibi Cedai Drolma alisema,

"Familia yangu ilikuwa maskini sana, hatukuwa na shamba wala nyumba, kwani mali zote zilimilikiwa na makabaila. Sisi tulikuwa wakulima watumwa, tulikuwa tunaishi maisha magumu. Tulikodi shamba la makabaila, na kuwapa mazao mengi ambapo sisi tulibakiwa na machache tu, hata hatukuweza kuhakikisha maisha ya kiwango cha chini."

Baada ya Tibet kupata ukombozi mwaka 1951, maisha ya bibi Cedai Drolma yalianza kubadilika. Kwa bahati nzuri alijiunga na Shirikisho la Wanawake Vijana la Tibet, na mara kwa mara alishiriki kwenye maonesho ya michezo ya sanaa yaliyoandaliwa na shirikisho hilo. Kutokana na uhodari wake wa uimbaji, bibi Cedai Drolma alianza kujulikana kwenye sehemu ya Tibet alipokuwa na umri wa miaka 21. Mwaka mmoja baadaye, bahati nzuri ilimfika tena. Ili kufundisha watibet wenye uwezo wa muziki, Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai kilianzisha madarasa ya makabila madogo madogo. Siku moja ya mwaka 1958, walimu wa chuo hicho walikwenda Tibet kuwaandikisha wanafunzi. Walimwona Cedai Drolma, na kumsifu sana kwa uhodari wake wa uimbaji. Akawa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai, alisema,

"Watu wengi walishiriki kwenye mtihani wa kuwaandikisha wanafunzi wa Chuo Cha Muziki cha Shanghai, mimi nilikuwa mmoja kati yao. Baada ya mtihani, walimu wa chuo hicho walikwenda kutaka kujua hali zetu. Kwenye kikundi cha maonesho ya michezo ya sanaa cha Shirikisho la Wanawake Vijana la Tibet, kulikuwa na wafanyakazi wengi wa kabila la Wahan, waliwaambia walimu hao kuwa kuna msichana mmoja aitwaye Cedai Drolma ana sauti nzuri. Walimu wa chuo cha muziki walinisikiliza nikiimba nyimbo, na walinikubali."

Kwa kutegemea sauti yake nzuri Cedai Drolma alijiunga na Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai. Lakini kwa msichana huyo aliyepata elimu halisi kwa muda wa chini ya mwaka mmoja, masomo ya chuo kikuu bila shaka yalikuwa changamoto kubwa kwake. Ingawa walimu wote walimsifu kwa sauti yake nzuri, lakini Cedai Drolma hakujua kusoma wala kuandika, na hakufahamu nadharia ya muziki, hivyo aliendelea polepole sana katika masomo yake, hata aliwahi kufikiri kuacha. Alisema,

"Baada ya kufika Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai, niligundua kuwa siwezi kufahamu lugha ya walimu na wanafunzi wengine. Mwanzoni hata nilifiriki kuacha masomo na kurudi Tibet."

Walimu wa Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai walifanya juhudi kubwa ili kumsadiai Cedai Drolma kuondoa tatizo lake, na hata walimu waliomfundisha walianza kujifunza lugha ya kitibet. Watu wote walikuwa wanamtendea Cedai Drolma kama ndugu yao. Hali hii ilimsaidia sana kuinua kiwango chake cha uimbaji. Katika kipindi hicho, Cedai Drolma aliimba wimbo wa Wakulima Watumwa Waliokombolewa Waimba Nyimbo kwenye filamu moja. Alisema,

"Wimbo huo ulitokana na filamu ya rikodi ziliyopigwa na kampuni ya Filamu ya Xinyi ya Mji wa Beijing. Filamu hiyo maarufu ni kwa ajili ya kuonesha hali halisi ya zamani na ya sasa ya Tibet, na hasa mabadiliko tangu mageuzi ya kidemokrasia yafanyike.

Baada ya hapo, bibi Cedai Drolma aliimba nyimbo nyingi za lugha ya kitibet, na kuwaachia kumbukumbu nzuri kwa sauti yake maalumu na hisia za dhati. Nyimbo zilizoimbwa naye ziitwazo "Kuimba Nyimbo Kwa Ajili ya Chama Cha Kikomunisti cha China" na "Juu ya Mlima wa Dhahabu wa Beijing" zimejulikana kote nchini China, na zimewafurahisha sana watu. Ili kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya Tibet, baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai, aliondoka mji ulioendelea wa Shanghai na kurudi mkoani Tibet. Alisema,

"Nilizaliwa na kukulia mkoani Tibet. Mimi ni mwimbaji wa kabila la Watibet, nyimbo zangu zina umaalumu wa kabila hilo. Naona ninaweza kufanya kazi vizuri zaidi nyumbani kwangu."

Baada ya kurudi mkoani Tibet, Bibi Cedai Drolam alijiunga na kikundi cha maonesho ya michezo ya sanaa cha Tibet. Katika miaka zaidi ya 40 iliyopita, alitembelea na kutoa maonesho kwenye kila pembe ya mkoa huo, na kuwatakia watu wa Tibet heri na baraka kwa nyimbo zake nzuri. Sasa bibi Cedai Drolma ana umri wa miaka zaidi ya 70, lakini sauti yake bado ni nyororo na ya kuvutia, anaendelea kueleza kwa nyimbo zake hadithi yake ya kuwa mwimbaji maarufu kutoka mkulima mtumwa kueleza maisha mazuri ya hivi sasa kwenye mkoa unaojiendesha wa Tibet.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-12