Tarehe 12 tetemeko kubwa la ardhi liliukumba mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China na kusababisha vifo vya watu wengi na hasara kubwa za mali. Chini ya uongozi wa serikali ya China, kazi za uokoaji zilianza mara moja baada ya kutokea kwa maafa hayo. Na kazi hizo zimesifiwa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa ofisi ya uratibu wa mambo ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Bi. Elisabeth Byrs alieleza kusikitishwa sana na maafa hayo makubwa yaliyoikumba China, alipotaja hali ya maelfu ya wanafunzi kunaswa kwenye vifusi vya majengo mkoani Sichuan, mama huyo mwenye umri wa makamo aliongea huku akitokwa na machozi, akisema
"Naona serikali ya China imefanya kila iwezalo na kuwapatia watu walionusurika mahitaji mbalimbali. Naamini kuwa watu wengi zaidi wataokolewa kutokana na utendaji wa kazi za uokoaji."
Baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Sichuan, serikali ya China ilichukua hatua haraka na kuhamasisha na kuratibu jamii nzima ya China ijiunge na kazi za uokoaji. Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alifika haraka kwenye eneo lililokumbwa na tetemeko hilo, akiongoza kazi za uokoaji na kuwapa pole waathirika wa maafa hayo. Hali hii ilimpa kumbukumbu kubwa mkurugenzi wa ofisi ya sekretarieti ya mkakati wa kimataifa wa kupunguza maafa ya Umoja wa Mataifa Bw. Salvano Briceno, alisema
"Serikali ya China ilichukua hatua kwa haraka kukabiliana na maafa hayo. Nilitazama vipindi vya televisheni, nikaona waokoaji walikuwa wamefika kwenye eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi chini ya muda wa saa 4 baada ya kutokea kwa tetemeko hilo. Serikali ya China ilifanya kazi nzuri ya kukabiliana na maafa, nilivutiwa na jinsi China ilivyochukua hatua kwa haraka sana."
Kutokana na hali mbaya ya hewa na barabara, kazi za uokoaji zinakabiliwa na matatizo mbalimbali. Hata hivyo msemaji wa Shirika la Afya duniani Bi. Fadela Chaib alieleza kuwa na imani kwa kazi za uokoaji, alisema
"Bila shaka! Hivi sasa China ni nchi yenye nguvu, uzoefu mkubwa wa kukabiliana na maafa, na wataalamu wengi wa sekta hiyo. Naona China ina uwezo wa kushughulikia mambo mbalimbali baada ya maafa hayo."
Hadi sasa nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa yameeleza nia ya kutoa uungaji mkono na misaada kwa China, na serikali ya China imetoa shukrani na kukaribisha misaada. Lakini kutokana na hali ngumu ya sasa kwenye eneo lililotokea tetemeko la ardhi China haijaanza kupokea misaada kutoka nje. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameeleza kuwa, yanapenda kutoa misaada wakati wowote. Bi. Elisabeth Byrs kutoka ofisi ya uratibu wa mambo ya kibinadamu alisema
"Tumesoma maelezo kwenye vyombo vya habari vya China, na kufahamishwa kuwa, katika eneo lililotokea tetemeko la ardhi kuna viwanda viwili vya kemikali vilivyoharibiwa vibaya. Tuna mpango wa kutuma kikundi cha wataalamu wa mazingira kwenda nchini China, na kutoa msaada kwa kushirikiana na idara husika za China."
Tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Sichuan limesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu 10. Je, kulikuwa na uwezekano wa kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa maafa makubwa ya namna hii? Mkurugenzi wa ofisi ya sekretarieti ya mkakati wa kimataifa wa kupunguza maafa ya Umoja wa Mataifa Bw. Salvano Briceno alijibu swali hilo, akisema
"Ni vigumu sana kutabiri tetemeko la ardhi, kwani linatokea ghafla. Hata kama China na nchi nyingine zinazotumia teknolojia za kisasa, hivi sasa zinaweza tu kutoa utabiri dakika chache tu kabla ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, lakini dakika hizo chache hazina maana kwa kutoa tahadhari."
Bw. Briceno aliongeza kuwa, hata hivyo binadamu wanaweza kupunguza madhara ya matetemeko ya ardhi katika kuimarisha uimara wa majengo.
|