Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-18 20:58:26    
Mwigizaji mashuhuri wa China Pu Cunxin

cri

Bw. Pu Cunxin ni mwigizaji wa China ambaye licha ya kuwa anajulikana sana kutokana na michezo yake ya kuigiza, pia ni mwigizaji mashuhuri katika filamu na michezo ya televisheni, kadhalika pia ni mwenezi wa ujuzi wa kinga dhidi ya UKIMWI.

Mliyosikia ni sauti yake alipokuwa anaimba shairi la kale la China.

Bw. Pu Cunxin alizaliwa mwaka 1953 katika familia ya wasanii. Mwaka mmoja kabla ya kuzaliwa, Kundi la Michezo ya Kuigiza la Beijing lilianzishwa na baba yake alikuwa mmoja wa waigizaji wa kundi hilo. Katika muda wa miaka zaidi ya 50 iliyopita, kundi hilo la ngazi ya taifa lilionesha michezo 300 hivi ya kale na ya zama hizi na ya nchini China na ya nchi za nje. Kundi hilo lina waigizaji wengi mashuhuri na limekuwa linang'ara sana katika utamaduni mjini Beijing. Hivi sasa Bw. Pu Cunxin ni naibu mkurugenzi wa kundi hilo. Kuhusu jinsi kundi hilo lilivyokuwa na athari kwake alisema,

"Athari niliyopata kutoka kwa kundi hili ni ya kisaikolojia, ya kiroho na ya kimaisha. Mimi ni mtu wa kizazi kipya, lakini nimewahi kuwaona wasanii wazee, na baba yangu alikuwa mmojawao. Athari yao kwangu ni kubwa, nataka kuwa msanii kama wao, ingawa sijawafikia lakini najitahidi."

Bw. Pu Cunxin alipokuwa mtoto karibu miaka yote aliipitisha mbele ya jukwaa. Baba yake kwa makusudi alimwingiza kwenye usanii wa michezo ya kuigiza, akimwacha aangalie michezo mbele ya jukwaa na kumfundisha utamaduni wa jadi wa China ikiwa ni pamoja na sanaa ya kuandika maandiko ya Kichina kwa brashi ya wino, kuchora picha na mazingira ya jukwaani, hata waongozaji na waigizaji wa michezo walipojadiliana kuhusu maandishi ya michezo nyumbani, baba yake alikuwa anamwita asikilize. Pu Cunxin aliwaona jinsi walivyojadiliana kwa upole na jinsi walivyozozana kwa kelele, na jinsi walivyosema maneno yaliyoandikwa kwenye maandishi na kuingia kwenye michezo. Mazingira hayo yalikuwa kama mwangaza wa jua na maji yaliyokuwa yakimlea kisanii. Kutokana na sababu fulani Bw. Pu Cunxin alipata elimu ya msingi tu, lakini anaona kuwa hakukosa kuelimishwa, alisema,

"Elimu niliyopata ikiwa ni pamoja na barua zangu kwa baba yangu ambaye alinirudishia barua yangu baada ya kupiga mstari kwenye maneno niliyokosea na sentensi yenye dosari na kuniambia 'soma mwenyewe'. Sikukosa kufundishwa na nina moyo wa kujiendeleza. Kwa kweli nilipokuwa katika umri wa kusoma nilishuhudia uhodari wa wasanii wazee, pamoja na hayo niwahi kupita wakati wangu mgumu ambao wengine hawakupata. Yote hayo ni uzoefu na fikra zangu ambazo nataka kuwafundisha waigizaji au wasanii vijana."

Bw. Pu Cunxin alipokuwa na umri wa miaka miwili aliugua polio na kupata athari ya ugonjwa huo, watoto walimcheka jinsi alivyokuwa anatembea. Pu Cunxin mwenye nia thabiti alifanya juhudi nyingi ili aweze kutembea kama kawaida, alicheza mpira wa kikapu, kuongelea na mara nyingine alishindana na wengine. Alipokuwa na umri wa miaka 16 "mapinduzi makubwa ya utamaduni" yalikuwa yakifanyika kote nchini China, kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wengine alipelekwa vijijini kufanya kazi za kilimo kwenye sehemu ya kaskazini mashariki ya China. Katika muda wa miaka minane alipokuwa vijijini, aliwahi kufanya kazi za kilimo, kuchunga farasi na mara moja moja pia alicheza michezo ya kuigiza. Mwaka 1977 alirejea mjini Beijing na kuwa mwigizaji katika kundi moja la wasanii. Kutokana na uigizaji wake mzuri alichaguliwa kuwa mwigizaji wa Kundi la Michezo ya Kuigiza la Beijing. Bw. Pu Cunxin alipokumbuka miaka hiyo alikuwa na mengi ya kusema,

"Nilikulia kwenye mazingira ya michezo ya kuigiza, mazingira hayo yaliniathiri na kutokana na athari hiyo nimekuwa mwigizaji. Nilirudi tena Beijing baada ya kuishi vijijini kwa miaka mingi mwishowe nimeweza kusimama jukwaani nikiwa mwigizaji! Hapo zamani nilikuwa natazama michezo chini ya jukwaa na sikuwahi kupanda jukwaani. Mara ya kwanza niliposimama jukwaani nilisisimka na hata sikuamini kama ningeweza kuwa mwigizaji wa kundi hilo maarufu! Baada ya kuwa mwigizaji wa kundi hilo, katika muda wa miaka 20 iliyopita nilikuwa mwigizaji mkubwa katika kundi hilo, najipongeza sana."

Bw. Pu Cunxin alikuwa mwigizaji mkubwa tokea alipokuwa na umri wa miaka 33. Mambo aliyopitia yamekuwa msingi wake imara ambao unamwezesha kuigiza kwa ufanisi watu wa aina mbalimbali wa zamani na wa leo, wa nchini na wa nchi za nje. Aliwahi kuigiza kama mshairi mkubwa wa zama za kale za China Li Bai, aliwahi kuigiza kama Cao Cao aliyekuwa mtaalamu wa mambo ya kivita na jemadari mwenye njama katika zama za kale nchini China, na aliwahi kuigiza kama shujaa wa zama za kale za Roma katika mchezo wa kuigiza wa "Jemadari Coriolanu" uliohaririwa kwa mujibu wa mchezo ulioandikwa na Shakespeare. Watu wanatarajia sana aweze kuigiza tena michezo maarufu kama "Mkahawa" uliooneshwa miaka mingi bila watazamaji kupungua na mchezo wa "Mvua ya Radi". Bw. Pu Cunxin alisema,

"Fasihi ya michezo ya kuigiza, hasa maandishi maarufu, inatuimarisha sisi waigizaji kisanii, tulipocheza mchezo wa "Mkahawa" maneno yaliyoandikwa na mwandishi Lao She yanatulevya na kila ninapoyachunguza zaidi ndipo ninapata hisia mpya zaidi, na nafasi ya namna ya kuonesha hisia ni kubwa, hata mchezo huo ukichezwa baada ya miaka kumi nafasi hiyo bado ni kubwa. Maandishi mashuhuri ya michezo ya kuigiza yanasaidia sana waigizaji kukua kisanii."

Mwaka jana ulikuwa ni mwaka wa mia moja tokea michezo ya kuigiza ianzishwe nchini China. Katika mwaka huo akiwa mwigizaji mkuu aliigiza michezo nane ambayo ilioneshwa zaidi ya mara 120. Licha ya michezo ya kuigiza, Bw. Pu Cunxin pia ni mwigizaji filamu anayependwa na watazamaji, na filamu nyingi alizoigiza zilipata tuzo. Bw. Pu Cunxin alisema,

"Usanii ulivyo ni kama mtu alivyo, kutokana na ubunifu wa kisanii watazamaji wanaweza kufahamu maadili yako."

Bw. Pu Cunxin mbali ya kuwa mwigizaji mashuhuri pia anashiriki kwenye kazi nyingi za ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kuhamasisha watu kuchangia damu, na kujikinga dhidi ya UKIMWI. Sura yake angavu katika matangazo ya ustawi wa jamii inaonekana kila mahali kwenye mabasi, vituo vya subway na kando ya barabara. Alipogusia kazi hiyo alisema,

"China imeendelea mpaka hivi leo, watu wamekuwa na uwezo na hamu ya kushiriki kwenye kazi ya ustawi wa jamii, hii ni kawaida ya maendeleo ya jamii. Ni furaha yangu kushiriki kwenye kazi hizo na napata ridhaa moyoni, hii ni aina moja ya maisha inayoleta furaha."

Mwishoni mwa mwezi Machi Bw. Pu Cunxin alikwenda Ugiriki kushiriki kwenye mbio za mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, na yeye pia ni mtu anayejitolea katika michezo ya walemavu ya Olimpiki. Shughuli zake mwaka huu zote zinahusika na michezo ya Olimpiki. Katika kipindi cha michezo ya Olimpiki ya Beijing michezo iliyo maarufu ya kuigiza itaoneshwa na kundi lake, na yeye mwenyewe ni mwingizaji mkuu katika michezo hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-15