Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-15 16:53:20    
Moja ya mbinu 36: Mtego wa Mrembo

cri

"Mtego wa Mrembo" ni moja ya mbinu 36 za kivita katika kitabu cha kale nchini China. Mbinu hiyo hutumika wakati unapokuwa katika hali mbaya vitani, kwa hiyo mbinu hiyo pia inaitwa mbinu ya mnyonge.

Kwa mujibu wa maneno, "Mtego wa Mrembo" maana yake ni kuwashawishi maadui waingie kwenye mtego wako kwa kutumia mwanamke mrembo. Wataalamu wa mambo ya vita katika zama za kale nchini China wanaona kuwa wakati unapokuwa katika hali mbaya, kuna mbinu tatu za kuwarubuni maadui. Moja ni kuwa wakati usipokuwa na njia nyingine gawa ardhi yako kwa maadui, lakini mbinu hiyo hakika inawaongezea nguvu maadui na matokeo yake hayatakuwa mazuri kwako. Mbinu nyingine ni kuwafurahisha maadui kwa fedha, vito na hariri au vitu vingine vya thamani, lakini mbinu hiyo inawaongezea mali maadui, na mbinu hiyo ikitumika kwa muda mrefu utapoteza mali nyingi na matokeo pia hayatakuwa mazuri kwako. Mbinu iliyo bora kabisa kati ya mbinu tatu ni kutumia mwanamke mrembo, kwani mbinu hiyo inaweza kuwafanya maadui wapoteze nia yao ya kupambana, kudhoofisha afya yao na kusababisha manung'uniko miongoni mwa maadui na kuwapotezea askari ushupavu wa kupambana, huku ukichukua hatua mbalimbali kujiimarisha kutoka kwenye hali ya udhaifu.

Sifa za mbinu hiyo ya kutumia mwanamke mrembo ni hatari kidogo lakini matokeo yake ni mazuri. Katika zama za kale nchini China wanawake walikuwa hawana heshima katika jamii, walikuwa ni kama vyombo tu vya kuwafurahisha wanaume katika jamii iliyotawaliwa na wanaume. Tukiangalia historia ya China na ya nchi za nje, tunaweza kuona kuwa mbinu hiyo haijawahi kushindwa, na kuna hadithi nyingi za kutumia mbinu hiyo ambazo zinastaajabisha.

Katika kipindi cha Spring na Autumn nchini China yaani tokea mwaka 770 K.K. hadi 476 K.K., katika vita mfalme wa dola la Yue aitwaye Gou Jian alishindwa kwa mfalme wa dola la Wu aitwaye Fu Chai. Mfalme Fu Chai alimwadhibu mfalme Gou Jian afanye kazi ya sulubu akiwa pamoja na mke wake ndani ya kasri lake ili kumwaibisha. Mfalme Gou Jian alinyenyakea na kujipendekeza kwa mfalme Fu Chai na mwishowe alipata uaminifu wa mfalme Fu Chai ambaye baadaye alimruhusu arudi kwenye dola lake la Yue. Baada ya kurudi kwenye dola lake mfalme Gou Jian alitumia mbinu ya "Mtego wa Mrembo" kwa mfalme Fu Chai, alichagua warembo wawili ambao hawakupatikana kirahisi, mmoja aliitwa Xi Shi, mwingine aliitwa Zheng Dan, akawatuma warembo hao kwa mfalme Fu Chai na zaidi ya hayo kila mwaka alikuwa anamzawadia mfalme Fu Chai kwa mali nyingi za vito na johari. Mfalme Fu Chai aliona kuwa kweli mfalme Gou Jian amekuwa mtiifu kwake, kwa hiyo hakuwa na wasiwasi wowote juu yake. Kila siku mfalme Fu Chai alikuwa anaburudika na warembo kwa pombe, kiasi ambacho hakutilia maanani ushauri wa mawaziri kuhusu mambo ya taifa. Baadaye mfalme Fu Chai alilishambulia dola la Qi na hata mfalme Gou Jian alimsaidia Fu Chai ili kuonesha utiifu wake kwake na kumpooza kiakili. Baada ya Gou Jian kulishinda dola la Qi, mfalme Gou Jian alikwenda kwenye dola la Wu kumpongeza mfalme Fu Chai. Fu Chai alikuwa ametumia wakati wote katika furaha ya kuburudika na warembo bila kushughulikia mambo ya utawala. Mfalme Gou Jian alifurahi sana kuona yote aliyotenda Fu Chai. Mwaka 482 K.K. dola la Wu lilikumbwa na ukame mkali, mfalme Gou Jian alitumia fursa ya Fu Chai kutokuwepo kwenye dola lake, aliwatuma askari wapanda farasi kushambulia dola la Wu kwa ghafla, na kuliangamiza dola la Wu.

Watu husema, ni vigumu kwa shujaa kushinda vishawishi vya mrembo. Lakini kwa nini shujaa mwenye ujasiri na akili anashindwa dhidi ya vishawishi vya mrembo? Shujaa kama huyo ambaye hata anashindwa kufaulu mtihani huo anastahili kuwa shujaa wa kweli? Ukweli ni kwamba "shujaa" tunayetaja hapa ni shujaa wa kweli, lakini tatizo ni kwamba mrembo anawasha hisia za shujaa na kushambulia udhaifu wake wa kimwili, kwa hiyo anashindwa kujikinga. Kwa kweli hali hiyo ina sayansi fulani. Utafiti wa Chuo Kikuu cha McMaster cha Canada umegundua kwamba wanaume wanaposhawishiwa na wanawake wanabadilika kuwa na "mtazamo mfupi". Utafiti unaonesha kuwa, wanafunzi walioshiriki kwenye utafiti huo wote wangeweza kupata pesa baada ya kuangalia picha za warembo, wanaweza kuchagua wapate dola 15 katika siku ya pili au dola 50 katika siku nyingine baadaye. Matokeo yakawa kwamba wale wanafunzi walioangalia picha za wanawake wenye sura ya kawaida walichagua kupata dola 50 baada ya muda, chaguo hilo ni la kawaida kiakili, lakini wanafunzi walioangalia picha za warembo walichagua kupata dola 15 katika siku ya pili bila ya kuweza kuvumilia kupata katika siku nyingine baadaye. Utafiti huo umethibitisha kwamba kweli wanaume wanaweza kupoteza akili na "kuchagua mrembo badala ya utawala wa taifa".

"Mtego wa Mrembo" unafaa kutumika kila mahali duniani. Katika nyanja mbalimbali kama diplomasia, ushindani wa biashara, uhusiano wa kijamii, matangazo ya biashara, na upelelezi wa habari mbinu hiyo haikosi kutumika.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-15