Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-16 16:27:55    
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za "Matofali Manne ya Dhahabu" wakutana nchini Russia

cri

Mawaziri wa mambo ya nje wa China, Russia, India na Brazil tarehe 16 watakutana katika mji wa Yekaterinburg nchini Russia. Nchi hizo nne zinasifiwa kuwa ni "nchi zenye maendeleo ya haraka ya uchumi" duniani, na kutokana na mpangilio wa herufi za Kiingereza nchi hizo pia zinaitwa nchi za "matofali manne ya dhahabu".

Jina la "Matofali Manne ya Dhahabu" lilianza kutumika mwaka 2003. Kwa mujibu wa makadirio yaliyotangazwa mwaka huo, China, Russia, India na Brazil zilisifiwa kuwa ni "nchi zenye maendeleo ya haraka ya uchumi" duniani. Septemba mwaka 2006 mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo nne walikutana mjini New York wakati mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ulipofanyika mjini humo. Kwenye mkutano wa sasa mawaziri hao watajadiliana kuhusu hali ya usalama wa nishati na namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo. Aidha, mawaziri hao pia watabadilishana maoni kuhusu masuala ya kupunguza silaha, kutoenea kwa silaha za nyuklia, mapambano dhidi ya ugaidi, uhalifu wa vikundi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Baada ya mkutano watatangaza taarifa ya pamoja ikionesha msimamo wa pamoja wa nchi hizo kuhusu uchumi na usalama duniani.

Kati ya nchi chipukizi kiuchumi duniani, nchi hizo za "matofali manne ya dhahabu" zinajitokeza zaidi. Kati ya nchi hizo, China, India na Brazil ni nchi zinazoendelea, na Russia ilikuwa ni sehemu ya nchi yenye nguvu kubwa kupita kiasi, Urusi ya zamani na hivi sasa nchi hiyo Russia imekuwa inafufuka. Kati ya nchi hizo licha ya maendeleo ya China yanayovutia duniani, uchumi wa India unaongezeka kwa wastani kati ya 6% na 7% kila mwaka katika muda wa zaidi ya kumi, na mwaka 2007 hata ulifikia 8.9%. Katika muda wa miaka saba iliyopita uchumi wa Russia pia umekuwa unakua haraka, mwezi Februari mwaka huu Rais Putin alipokumbusha maendeleo yaliyopatiakana katika kipindi alipokuwa madarakani alisema, thamani ya uzalishaji iliongezeka haraka hadi kufikia 8% na kuwa moja ya nchi kubwa saba kiuchumi duniani. Uchumi wa Brazil unakua kwa hatua imara, mwaka jana ongezeko la uchumi wake lilikuwa 5.4%, na akiba ya fedha za kigeni imeongezeka maradufu kuliko mwaka uliotangulia na kuwa karibu dola za Marekani bilioni 200. Kwa mujibu wa uwezo wa ununuzi, michango ya nchi hizo nne katika ongezeko la uchumi duniani inafikia 50%.

Kutokana na takwimu za makadirio, jumla ya thamani ya uchumi ya nchi hizo nne itakuwa zaidi ya nusu ya jumla ya thamani ya uchumi ya nchi zilizoendelea za Marekani, Ujerumani, Japan, Uingereza, Ufaransa na Italia. Hadi kufikia mwaka 2050 kati ya nchi hizo sita zilizoendelea, Marekani na Japan tu zinaweza kuendelea kuwa nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, wakati huo katika nchi hizo za "matofali manne ya dhahabu" kutakuwa na watu milioni 210 wenye kipato cha dola za Marekani elfu 15 kwa wastani wa kila mmoja kwa mwaka, na wakati huo Wajapan watakaopata kipato hicho watafikia milioni 120, Wajerumani milioni 75 na Waingereza milioni 57. Kwa makadirio, hadi kufikia mwaka 2025 China na India zitaongoza duniani katika sekta za bidhaa na huduma, Russia na Brazil zitaongoza duniani katika sekta za nishati na malighafi.

Wachambuzi wanaona kuwa kwa sababu mfumo na njia za kustawisha uchumi katika nchi hizo nne za "matofali ya dhahabu" zinaweza kukidhi mahitaji ya aina tofauti katika zama za utandawazi duniani, na kasi ya maendeleo ni kubwa dhahiri ikilinganishwa na nchi zilizoendelea, nchi hizo zimekuwa mfano bora kwa nchi zinazoendelea, kwa hiyo nchi za Magharibi zimekuwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko ya hadhi yao duniani.

Wachambuzi wanaona kuwa mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za China, Russia, India na Brazil ni jaribio la kuimarisha ushirikiano na kulinda maslahi ya pamoja. Mkutano huo hakika utasaidia sana kuimarisha ushirikiano wao na kurekebisha uhusiano kati yao na nchi za Magharibi.