Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-22 14:41:12    
Moja ya mbinu 36, Kuufanya Mti Uchanue Maua

cri

Si ajabu kuona kwamba mti unachanua maua, lakini mbinu ya "kuufanya mti uchanue maua" inamaanisha mti usiochanua maua uchanue.

Mbinu ya "kuufanya mti uchanue maua" ina maana ya kutengeneza maua bandia na kuyatundika kwenye matawi ya mti kama maua ya kweli, ili kuficha udhaifu wako na kuongeza tishio lako kwa maadui.

Tukiangalia historia ya China, mifano ya kutumia mbinu hiyo ya kuficha udhaifu na kujitukuza kwa umwamba ni mingi, mmoja ni kama ufuatao.

Katika Kipindi cha Madola Matatu ya Kifalme nchini China, jemadari Zhang Fei wa dola la Shu alikuwa na ujasiri na akili. Mwaka 208 jemadari Cao Cao wa dola la Wei aliliongoza jeshi lake kuushambulia mji wa dola la Shu, Jingzhou, uliokuwa unalindwa na jemadari Liu Bei. Kutokana na nguvu dhaifu, Liu Bei aliwaongoza askari na wakazi wa mji huo kukimbia mji huo, lakini kutokana na askari kujichanganya na wakazi kasi ya kukimbia mji ilikuwa ndogo sana. Baada ya kusikia kuwa kasi ya jeshi la Liu Bei ilikuwa ndogo, Cao Cao aliwaamuru askari wake wawafukuze kwa farasi. Kwenye sehemu iitwayo Dangyang, askari wa Cao Cao walikutana na askari wenzao waliopangwa kuwazuia askari wa Liu Bei. Liu Bei alishindwa na hata mke na mtoto wake wa kiume walipoteana. Kutokana na hali mbaya Liu Bei aliwahimiza askari wake wakimbie haraka huku akiomba jemadari mwenzake Zhang Fei amsaidie kupambana na Cao Cao. Wakati huo Zhang Fei alikuwa na askari wapanda farasi 30 hivi, ilikuwa si rahisi kwake kupambana na askari wengi wa Cao Cao. Lakini akili ya Zhang Fei haikuvurugika mbele ya hatari hiyo, aliwaamuru askari wake wapande farasi kukimbilia kwenye mtisu mmoja ambapo alikuwa na hakika kuwa askari wa Cao Cao watapita huko, wakate matawi ya miti na kuyafunga kwenye mikia ya farasi, kisha akawaamrisha askari hao wapige mbio huku na huko ndani ya msitu, wakati huo jemadari Zhang Fei alisimama kwenye daraja la mto mbele ya msitu akiwa na mkuki mkononi juu ya farasi mweusi. Punde si punde askari wa Cao Cao walifika, walipoona jemadari Zhang Fei amesimama peke yake bila hofu yoyote kwenye daraja na kuona mavumbi tele msituni, alisimamisha askari wake akihofia kuwa kuna askari walioficha ndani ya msitu, aliwaamrisha askari wake warurudi nyuma. Mara jemadari Zhang Fei alivunja daraja na kuondoka salama msitu. Huu ni mfano wa kutumia mbinu ya "kuufanya mti uchanue maua".

Hivi leo katika mambo ya biashara mbinu hiyo pia inatumika sana, mathalan kampuni ya tovuti ya Baidu inayojulikana sana nchini China. Hapo awali ilikuwa haina nguvu kiasi cha kuweza kushindana na kampuni kubwa za Sina na Sohu zenye wanamtandao wengi. Kampuni hiyo alitumia sera iliyoambatana na hali yake halisi na kushiriki kwenye ushirikiano na kampuni hizo kubwa kwa bei ya chini. Kwanza ilishirikiana na kampuni za Sina na Sohu kwa kuzisaidia kampuni hizo kutoa huduma za mtandao wa internet. Kutokana na umaarufu wa kampuni hizo kubwa, tovuti ya Baidu pole pole ilinyakua wanamtandao waliokuwa wa Sohu na Sina nchini China, baada ya muda nguvu ya Baidu ilizidi nguvu ya Sohu hatua kwa hatua, na iliharakisha hatua zake za kuingia sokoni na ikajenga mfumo wake wa kibiashara. Pamoja na hayo Sohu imeanzisha tovuti yake yenyewe na kuwahudumia moja kwa moja wanamtandao wake, matokeo yakawa kampuni hiyo imekuwa na wanamtandao wengi kuliko tovuti nyingine nchini China. Ufanisi wa Baidu unatokana na sera yake sahihi iliyoambatana na hali halisi na kushirikiana na kampuni kubwa za tovuti kwa unyenyekevu hapo awali. Kampuni hizo kubwa zilizokuwa maarufu bila kujua ziliisaidia Baidu ipate umaarufu katika matangazo yao. Huu ni mfano hai wa kutumia mbinu ya "kuufanya mti uchanue maua". Mfano huo unawasaidia watu kimawazo katika ushindani wa kibiashara unaopamba moto katika zama hizi.