Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-22 14:52:41    
Mwigizaji kijana Wang Baoqiang

cri

Miaka zaidi ya kumi iliyopita, mtoto mmoja baada ya kutazama filamu iliyooneshwa kijijini mwake alikuwa na ndoto ya kuwa mwigizaji filamu, na kweli baada ya juhudi ametimiza ndoto yake na kuwa mwigizaji mashuhuri, mwigizaji huyo anaitwa Wang Baoqiang.

Mwaka 2007 mchezo wa televisheni uitwao "Mashambulizi ya Ghafla" wenye sehemu nyingi mfululizo ulioneshwa kote nchini China. Huu ni mchezo unaoonesha maisha ya kiaskari. Katika mchezo huo, Wang Baoqiang aliigeza kama askari aitwaye Xu Sanduo, askari mpya aliyetoka kijijini. Katika mambo ya mafunzo ya kijeshi askari huyo alikuwa anashika mkia kwenye kundi lake kutokana na kuwa mgumu wa kuelewa mambo na mwenye bongo lala, askari wenzake walimlaumu na hawakuwa na njia ya kumbadilisha. Lakini yeye ni mtu myoofu, mwaminifu, na anayeshikilia kutimiza mambo anayotakiwa kutimiza. Kutokana na tabia hiyo mwishowe alichaguliwa kuwa askari hodari wa kikosi maalumu.

Katika siku za kuonesha mchezo huo, "askari punguani Xu Sanduo" pamoja na mwigizaji wa askari huyo Wang Baoqiang mara walijulikana kote nchini China.

Katika mchezo huo wa televisheni Wang Baoqiang aliigiza kama askari aitwaye Xu Sanduo, watazamaji wanamwita Xu Sanduo badala ya jina lake halisi. Bw. Wang Baoqiang alisema anapenda sana jinsi askari huyo alivyo. Alisema,

"Nimekua kwenye mazingira kama ya askari Xu Sanduo. Nimekulia katika mazingira ya kudharauliwa, kila niliposema nataka kuwa mwigizaji wa filamu wengine walinicheka na waliambia naota ndoto za mchana."

Wang Baoqiang alizaliwa mwaka 1984 katika kijiji kidogo wilayani Nanhe katika mkoa wa Hebei. Alipokuwa na umri wa miaka minane, filamu ya gongfu iitwayo "Hekalu la Shao Lin" ilioneshwa kijijini mwake. Filamu hiyo iliigizwa na mcheza filamu nyota Jet Li. Jinsi alivyoonesha uhodari wa gonfu katika mapambano ilimvutia sana, na akadhamiria kuwa mwigizaji kama Jet Li.

Moyoni mwa Wang Baoqiang hekalu la Shao Lin ni mahali patakatifu pa kujifunza gongfu, ni mahali pa kutimiza ndoto yake ya kuwa mwigizaji wa filamu ya gongfu. Aliwabembeleza na kuwang'ang'aniza wazazi wake mwishowe alikubaliwa kwenda kwenye hekalu la Shao Lin. Miaka kadhaa ilipita haraka, baada ya Wang Baoqiang kukua alifahamu kwamba kumbe maisha yake kwenye hekalu hilo yalikuwa hayana uhusiano wowote na uigizaji wa filamu.

Mwishoni mwa mwaka 1997 Wang Baoqiang alirudi nyumbani bila kuambulia kitu, kutokana na jinsi alivyokuwa na hamasa kubwa ya kutaka kuwa mwigizaji wa filamu, alikuwa mnyonge kama puto lililovuja hewa, wanakijiji wenzake walimcheka na kumdhihaki, lakini wakati huo alikuwa na wazo jingine la kuja Beijing kushiriki kwenye uigizaji wa filamu. Mtoto wa kijijini anawezaje kuja Beijing kushiriki kwenye uigizaji wa filamu? Wanakijiji waliona anaota.

Nia yake imara ya kufuatilia ndoto yake inafanana sana na hali ya askari Xu Sanduo. Katika mchezo wa "Mashambulizi ya Ghafla" mkuu wa kikundi bila kuwa makini alisema aliwahi kutaka kutengeneza barabara moja mbele ya nyumba za kikundi kilipo, askari Xu Sanduo alichukulia maneno hayo kama ni amri ya kijeshi, yeye alikuwa peke yake alikamilisha barabara hiyo bila kuwaambia wengine. Wang Baoqiang hakutaka kuacha tumaini lake, alikuja Beijing mwanzoni mwa mwaka 1999 kabla hajatimiza umri wa miaka 15.

Wang Baoqiang alikuwa peke yake na alikuwa anatangatanga katika nyanja ya uigizaji, maisha yake yalikuwa magumu sana. Kutokana na kusaidiwa na rafiki yake, siku moja alifika kwenye Kituo cha Kupigia Filamu cha Beijing na kuomba apate nafasi ya kuigiza kati ya vikundi vya uigizaji wa filamu. Alipokumbuka maisha ya kipindi hicho alisema,

"Tulikuwa watu watano, tuliishi kwenye nyumba moja ndogo ya kupanga ambayo baada ya kuweka kitanda kikubwa cha watu watano hakukuwa na nafasi nyingine, nje ya nyumba kulikuwa na mtaro wa maji machafu. Kila siku nilikuwa naamka mapema sana na kwenda kwenye kituo cha kupigia filamu kubahatika kupata nafasi ya uigizaji, kama nikipata niliweza kupata Yuan ishirini hivi, nisipopata nilirudi patupu kwenye nyumba tuliyopanga."

Wang Baoqing alitumai kuonekana kwenye filamu angalau uso tu, ili wanakijiji wenzake waweze kumwona, lakini baada ya mwaka mzima kupita hakupata nafasi hiyo, alikuwa hana budi ila kwenda kwenye sehemu ya ujenzi kufanya kazi ya kibarua ili kupata riziki. Alisema,

"Baada ya kuja Beijing maisha yangu yalikuwa kama mzururaji, nilikuwa sina kazi ya uhakika. Kazi ya kibarua naweza kuipata nyumbani kwangu, ya nini kuifanya hapa Beijing? Siku zilikuwa zinapita moja baada ya nyingine, sikujifunza lolote na sikupata pesa yoyote. Tumaini langu limekuwa linapotea siku hadi siku."

Wakati Wang Baoqiang alipokuwa pekee bila msaada wowote alipata barua kutoka kwa baba yake. Alisema,

"Baba yangu alisema yote ni makosa yake, nisimlaumu, anajua adha yangu kwenye sehemu ngeni, ananikaribisha wakati wowote nirudi nyumbani. Barua ya baba yangu ilinitia uchungu hata nisiweze kujidhibiti, barua yake ilinitia moyo nilipokuwa katika wakati mgumu kabisa, nikaamua kukaza nia nisirudi nyumbani, lazima nipate mafanikio nimfariji baba yangu."

Mwishowe Wang Baoqiang alipokuwa na umri wa miaka 16 alikuwa mwigizaji muhimu katika filamu ya "Shimo la Giza". Katika filamu hiyo Wang Baoqiang aliigiza kama mwanafumzi wa kijijini aliyefanya kazi ya kibarua mjini na kudanganywa. Wang Baoqiang aliyetoka kijijini aliigiza vizuri mhusika mwanafunzi huyo wa kijijini. Alisema,

"Nilivaa sare ya shule na kutembeatembea nikiwa na mzigo mgongoni. Mwongozaji wa upigaji wa filamu hiyo alipoona jinsi nilivyokuwa, alisema mtoto huyo wa kijijini hata akiigiza vipi atafanana tu mwanafunzi wa kijijini. Maneno hayo ya mwongozaji yalinipa moyo wa kujiamini."

Filamu ya "Shimo la Giza" ilipata tuzo katika tamasha la 53 la filamu la kimataifa la Berlin. Wang Baoqiang alipokuwa anakaribia umri wa miaka 20 alichaguliwa na mwongozaji mashuhuri wa upigaji wa filamu Feng Xiaogang kuwa mwigizaji katika filamu ya "Duniani Hakuna Mwizi".

Katika filamu hiyo ya "Duniani Hakuna Mwizi" Wang Baoqiang aliigiza kama kijana mmoja wa kijijini asiyefahamu mambo ya mjini, ndani ya garimoshi moyo wake mnyoofu uliwagusa hisia wanandoa wawili waliotaka kumwibia hapo awali kuwa walinzi wake katika mapambano dhidi ya wezi. Waigizaji katika filamu hiyo wote ni mashuhuri lakini uigizaji wake pia unavutia sana. Tokea hapo jina lake alilopewa na watazamaji "pungwani" likajukikana zaidi.

Mwaka 2007 mchezo wa televisheni wa "Mashambulizi ya Ghafla" ulioneshwa na kumfanya kijana huyo wa kijijini Wang Baoqiang ajulikane kwa kila familia. Alisema,

"Mwanzoni nilikuwa na nia tu ya kuonekana katika michezo ya televisheni na filamu ili wazazi wangu wanione, na wanakijiji wenzangu waseme, 'tizama, mtoto wenu!' Mchezo wa 'Mashambulizi ya Ghafla' ulipooneshwa wanakijiji wote waliwahi kutizama na walipofanya kazi mashambani walizungumza sana na baba yangu kwa sababu hawakuamini kama mtu waliyemwona kwenye televisheni ni mtoto wa jirani yao."

Vyombo vya habari vya nchini na nje viliandika habari nyingi kuhusu ufanisi wa Wang Baoqiang, vinaona kuwa nia thabiti ya kufuatilia lengo lake bila kurudi nyuma ilimfanya afanikiwe.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-22