Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-22 17:03:50    
Wanajeshi wafanya chini juu kuwaokoa wahanga wa tetemeko la ardhi mkoani Sichuan

cri

Tarehe 12 Mei tetemeko kubwa la ardhi lenye nguvu ya 8 kwenye kipimo cha Richter liliukumba mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China. Katika sehemu zilizoathirika vibaya kwenye maafa hayo, karibu nyumba zote zilibomoka, na wakazi wengi walifunikwa na kifusi. Wanajeshi, askari polisi na wazima moto wa China walitoa mchango mkubwa sana katika kazi ya uokoaji iliyoanza mara baada ya maafa hayo kutokea. Makala hii inaelezea jinsi walivyofanya uokoaji.

Mlizosikia ni kelele za askari polisi wakishangilia kufanikiwa kuwaokoa watu zaidi ya 20 kutoka kwenye kifusi tarehe 14 baada ya jitihada za muda wa zaidi ya saa 50. Hadi siku hiyo ya tarehe 14, watu wapatao 33,434 walinusurika na kuokolewa.

Tarehe 14 katika mji wa Beichuan, ambayo ni moja ya sehemu zilizoathirika vibaya zaidi kwenye tetemeko la ardhi, wazima moto kutoka mji wa Chongqing na sehemu nyingine mkoani Sichuan walikuwa wanaendelea kutafuta watu walionusurika kwenye kifusi cha jengo la shule ya sekondari ya Beichuan. Walipogundua kuwa, mwanafunzi mmoja wa kike alikuwa hai, uokoaji ulianza mara moja. Mzima moto mmoja alisema kwa sauti kubwa,  "Dada mdogo, usiongee sasa, uhifadhi nguvu yako na tusubiri tunakuokoa. Usiwe na wasiwasi, kamwe hatutaacha kipande cha saruji kikuangukie."

Baada ya mashine kuondoa nguzo nzito za nyumba, wazima moto walikuwa wakianza kuondoa kifusi kwa mikono yao na zana ndogo, wakihofia kuwa matumizi zaidi ya mashine yangeweza kusababisha kubomoka tena kwa sehemu ya juu na kumdhuru mtoto huyo. Muda si mrefu baadaye mwanafunzi huyo Zhu Hongmei mwenye umri wa miaka 13 aliokolewa kwa mafanikio, halafu alipelekwa mara moja kwenye zahanati ya muda iliyoko karibu ili apimwe afya.

Daktari akimaliza kumpima afya, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hali ya mwanafunzi huyo ilikuwa ni nzuri isipokuwa mguu wake wa kulia ulivunjika. Daktari alimfanyia matibabu ya lazima.

Muda wa saa 72 baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi unakubalika duniani kuwa ni kipindi mwafaka kabisa cha kufanya uokoaji. Hata hivyo baadhi ya watu walionusurika katika tetemeko hilo la ardhini mkoani Sichuan, waliokolewa baada ya muda huo wa saa 72, hata wengine waliokolewa baada ya saa 100.

Bw. Zhang Xiaoping ni mkazi wa mji wa Dujiangyan, aliokolewa baada ya kufunikwa ndani ya kifusi kwa muda wa saa 128.

Tetemeko la ardhi lilipotokea mchana wa tarehe 12, Zhang Xiaoping alikuwa nyumbani, nyumba ya ghorofa alikoishi ilibomoka na yeye akafunikwa na kifusi. Saa 3 na nusu asubuhi ya tarehe 17 alipogunduliwa na wanajeshi, alikuwa amekaa kwenye kifusi kwa saa karibu 116, lakini wakati huo bado alikuwa anaweza kupumua, isipokuwa alikuwa mdhaifu sana. Wanajeshi waliondoa kifusi kilichomfunika, huku madaktari wakisubiri karibuni.

Daktari mmoja aliyeshiriki kwenye uokoaji alisema "Tuliandaa machela, hewa ya oxygen, na zana nyingine za kutoa huduma ya kwanza pia ziko kwenye gari la wagonjwa. Hivi sasa habari nzuri ni kuwa mgonjwa huyo mwenyewe anaweza kunywa maji kiasi, sasa hivi tulimpa hewa ya oxygen. Mgonjwa huyo amekuwa akijeruhiwa kwa siku kadhaa, bado anaweza kupumua na kufikiri, kwa hiyo hakujeruhiwa vibaya sana."

Baada ya uokoaji wa saa mbili, sehemu ya juu ya mwili wa Bw. Zhang Xiaoping ilianza kuonekana, lakini miguu yake bado ilikuwa imefunikwa ndani ya kifusi. Meja jenerali Wang Qinlin wa kikosi kikuu cha wazima moto cha mji wa Chongqing, kilichoshiriki kwenye uokoaji alisema  "Hivi sasa ni kipindi muhimu cha uokoaji. Tutafanya kila tuwezalo kumwokoa hata kama kuna matumaini kiasi tu, iwapo mtu huyo bado anapumua, sisi wazima moto sote tutafanya chini juu kumwokoa."

Bw. Zhang Xiaoping aliokolewa kwa mafanikio saa 5 usiku wa tarehe 17, wakati ambapo muda wa saa 128 ulikuwa umepita baada ya tetemeko la ardhi kutokea.

Daktari wa saikolojia Feng Zhengzhi ni mmoja kati ya watu walioshiriki kwenye uokoaji. Alieleza kuwa mbali na kuwaokoa waathirika wa tetemeko la ardhi, matibabu ya kisaikolojia pia yalianza mapema, ili kuwasaidia kuondoa hofu na wasiwasi.

Daktari Feng Zhengzhi alisema  "Kwa mfano mtu mmoja alipoguduliwa alikuwa amefunikwa na kifusi kwa siku tano. Hali yake kimwili haikuwa si mbaya, yeye mwenyewe alionesha nia imara ya kuendelea kuishi. Uokoaji ulipokuwa unaendelea, nilizungumza naye. Katika mazungumzo kati yetu, nilianza kumpa matibabu ya kisaikolojia, matibabu ya namna hii yaliweza kumsaidia kuimarisha nia yake ya kuendelea kuishi, ili awe na imani kubwa, hakika waokoaji wanaweza kumwokoa kwa mafanikio."

Daktari huyo aliongeza kuwa, watu wakiokolewa, madaktari na wataalamu wa kisaikolojia wanawatibu zaidi kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisaikolojia, kwa mfano kuwasaidia waelezee hofu waliyo nayo, kuwaambia madaktari na waathirika wengine hisia zao wakati walipokumbwa na maafa hayo, kuwapa dawa, kuwatuliza ili waweze kupita kipindi hiki cha taabu.

Hivi sasa kazi ya uokoaji bado inaendelea katika sehemu zilizokumbwa na tetemeko la ardhi, ambapo wanajeshi, askari polisi na wazima moto wa China wanaendelea kuwa katika mstari wa mbele kuokoa maisha ya watu.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-22