Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-23 16:21:06    
Raia wa kigeni wakimbia Afrika Kusini kutokana na ghasia za mabavu

cri

Tokea wiki iliyopita Afrika Kusini imekumbwa na vurugu za kuwafukuza raia wa kigeni nchini humo, na hadi kufikia tarehe 22 wageni 42 walikuwa wameuawa na elfu 16 wamepoteza makazi, kwa hiyo wageni wengi wamekimbia nchi hiyo. Wachambuzi wanaona kuwa vurugu hizo zinasababishwa na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa tofauti ya mapato kati ya matajiri na watu maskini, watu maskini walio wengi kulalamikia hali mbaya ya maisha na kuona kwamba watu waliotoka nchi za nje wamenyakua ajira zao.

Hapo mwanzoni vurugu hizo zilitokea katika mtaa wa watu maskini mjini Johannesburg, wageni kadhaa waliokuwa wanafanya kazi mjini humo walipigwa, kisha vurugu hizo zikaenea kwenye mitaa mingine na kuwa kubwa kiasi kwamba mjini humo matukio ya kuwapiga wafanyakazi wengi wa kigeni yakabadilika kuwa kupora mali na kuwafukuza wageni. Makazi ya wafanyakazi hao wa kigeni yalichomwa moto na wengi walijeruhiwa. Hivi sasa vurugu hizo pengine zitaenea kote nchini.

Baada ya vurugu hizo kutokea, sekta mbalimbali pamoja na jumuyia za kimataifa zimetoa wito wa kuwataka watu wa Afrika Kusini kuwa wavumilivu na kukomesha haraka vurugu hizo za kuwafukuza wageni. Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini tarehe 20 alitoa taarifa akiwataka wawe na moyo wa Kiafrika na kufahamu kwamba kuheshimu kila Mwafrika ni sawa kujiheshimu. Rais Mbeki ameunda tume maalumu kufanya uchunguzi kuhusu vurugu hizo. Alihimiza polisi ichukue hatua za haraka kupambana na wahalifu. Na amekubali kutuma askari kwenye sehemu zenye vurugu kulinda hali ya utulivu na hasa kuwalinda wageni. Kwenye vurugu hizo polisi wamewakamata wahalifu wengi.

Kwenye vurugu hizo wahalifu wanalenga tu wale wanaotoka kutoka Zimbabwe, Msumbuji na Nigeria na Waafrika wengine wanaotafuta ajira nchini humo, lakini wageni wengine kutoka Ulaya na Asia wako salama. Sababu ya kuwafukuza wageni inatokana na kwamba watu wa nchi jirani wamenyakua nafasi za ajira.

Afrika Kusini ambayo ni nchi inayoendelea haraka kiuchumi barani Afrika, kila mwaka inawavutia watu wengi wa nchi jirani na nchi nyingine za Afrika wanaokwenda kutafuta ajira, na kati yao wengi ni wahamiaji haramu. Kutokana na kuwa katika miaka ya hivi karibuni hali ya uchumi wa Zimbabwe inazidi kuwa mbaya, watu wengi wa nchi hiyo wanakwenda huko kufanya kazi za vibarua au kufanya biashara ndogo ndogo, kwa mujibu wa takwimu hivi sasa Wazimbabwe nchini Afrika Kusini wamefikia milioni moja.

Katika historia ya Afrika Kusini kutokana na sera ya ubaguzi wa rangi wazawa wa Afrika Kusini hawakusoma sana, kwa hiyo hawawezi kushindana na watu wa Zimbabwe na Msumbuji wenye elimu zaidi, na watu kutoka nchi hizo hawadai mishahara mikubwa. Imefahamika kwamba kiasi cha watu wa Afrika Kusini wasio na ajira kimefikia 40%. Katika muda wa miaka miwili iliyopita kasi ya maendeleo ya uchumi nchini Afrika Kusini imepungua, na makampuni mengi yalipunguza ajira kutokana na upungufu wa umeme.

Katibu mkuu wa chama tawala cha Afrika Kusini Bw. Kgalema Motlanthe alisema, watu wanaoishi katika mitaa maskini wamejaa hasira na ni wepesi kufanya matukio ya mabavu. Alisema kuboresha mazingira yao ya kimaisha na kuwainulia maisha yao na kuwapatia nafasi za kusoma ili kuwaongezea uwezo wa kujitafutia maisha ni msingi wa kutatua vurugu kama hizo.