Tarehe 27 serikali ya Afrika Kusini ilifanya mkutano wa dharura ulioshirikisha idara 11 husika kuchunguza chanzo cha ghasia za kuwafukuza wahamiaji na kujadili kazi zinazotakiwa kufanyika. Mkutano huo unaona kuwa kutilia maanani na kuboresha hali ya maisha ya wakazi maskini wa sehemu zilizo karibu na miji mikubwa ni msingi wa kutatua ghasia hizo.
Tarehe 11 kwenye mtaa wa wakazi maskini mjini Johannesburg kulitokea ghasia za kuwafukuza wahamiaji. Wazawa wa Afrika Kusini walioshika fimbo na mashoka waliwapiga na kuwafukuza wahamiaji waliotoka nchi jirani za Zimbabwe, Musumbiji na Malawi wakidai kuwa watu hao wamenyakua nafasi zao za ajira na kuleta matukio mengi ya uhalifu. Hatimaye ghasia hizo zikaenea hadi kwenye miji ya pwani ya Durban na Cape Town, na matukio ya mabavu yalitokea katika mikoa saba kati ya mikoa tisa. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 56 na watu elfu 35 kupoteza makazi.
Kwa sababu ya ghasi hizo wahamiaji maelfu kwa maelfu ya wahamiaji waliotoka nchi jirani walikimbia Afrika Kusini na kukusanyika kwenye mpaka, na ikatokea hali mbaya ya ubinadamu kutokana na kukosa makazi, chakula na maji. Hivi sasa wakimbizi zaidi ya elfu 30 wanaishi kwenye mahema yaliyosaidiwa na jumuyia za kimataifa za utoaji wa msaada wa kibinadamu, na wengine wanakaa kwenye vituo vya polisi na makanisani. Kwa mujibu wa maelezo ya ofisa wa Chama cha Msalama Mwekundu cha Afrika Kusini, tatizo lililopo sasa ni kuwa idara zisizo za kiserikali za Afrika Kusini ni vigumu kuwasiliana na serikali za nchi zenye wakimbizi hao, na kazi ya kuthibitisha uraia wa wahamiaji hao wakati kwenye forodha inakwenda pole pole.
Serikali za nchi zenye wahamiaji wengi nchini Afrika Kusini zilitoa taarifa ya kuwakaribisha wananchi wao kurudi nyumbani, lakini kati yao wengi ni wahamiaji haramu nchini Afrika Kusini na hawana paspoti, ndio maana kazi ya kuthibitisha uraia wao inakwenda pole pole.
Kutokana na wageni wengi kuondoka nchini Afrika Kusini, ghasiza za mabavu dhidi yao imeanza kutulia. Mkutano wa serikali ya Afrika Kusini ulioshirikisha idara husika unaona kuwa serikali ya Afrika Kusini ilizembea kuchukua hatua na kutuliza jamii kwa kuongeza nguvu za polisi baada ya ghasia za mabavu kutokea kwa wiki moja. Wachambuzi wa taasisi ya utafiti wa uhusiano wa kikabila nchini Afrika Kusini wanaona kuwa ingawa Rais Thabo Mbeki tarehe 25 alisema akitaka wananchi wake watambue umuhimu wa umoja wa Afrika na kusema kwamba ghasia za mabavu za kuwafukuza wageni zinaharibu heshima ya Afrika Kusini, lakini yote hayo yamechelewa sana.
Kuhusu sababu za kutokea kwa ghasia hizo kubwa za kuwafukuza wageni, mkutano huo unaona kuwa ongezeko la uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka huu lilipungua na kufikia 2.1%, lakini mwaka jana ongezeko hilo lilikuwa ni 5.3%, upungufu huo umesababisha shinikizo kubwa la ajira. Mkutano huo unaona kuwa kutilia maanani kuboresha hali ya maisha ya watu kwenye sehemu za watu maskini zilizo karibu na miji mikubwa ni msingi wa kutatua tatizo lenyewe, na serikali inapaswa kuimarisha ujenzi wa miundombinu kwenye sehemu hizo na kutenga fedha nyingi zaidi kwa mambo ya elimu ya vijana wanaoishi kwenye sehemu hizo, kuwapa ufuatiliaji zaidi wa jamii na kuongeza nafasi nyingi zaidi za ajira, aidha kupambana vikali na uhalifu wa mabavu wa aina mbalimbali.
|