Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-30 18:59:14    
Italia yaisifu China kwa juhudi za kupambana na maafa ya tetemeko la ardhi

cri

Baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea tarehe 12 huko Wenchuan mkoani Sichuan, China, nchi nyingi marafiki zilitoa misaada kwa China, ikiwemo Italia. Vifaa na dawa za misaada zilizotolewa na Italia hivi sasa zimewakilishwa kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa, hospitali za muda na madaktari wanaojitolea pia walianza kazi za uokoaji mara baada ya kufika huko. Kutokana na kujionea hali ya huko, wamesifu sana jinsi serikali ya China na wananchi wake wanavyopambana na maafa ya tetemeko la ardhi kwa juhudi kubwa. Mkurugenzi wa idara ya uokoaji ya Italia Bw. Di Agostino Miozzo alipozungumza na waandishi wetu wa habari alisema:

"Kutokana na habari nilizopata kutoka kwa wenzangu na watu wetu waliopo kwenye sehemu ya maafa, nimeona kuwa serikali ya China imetumia nguvu nyingi kwenye sehemu iliyiokumbwa na maafa. Kazi ya uokoaji ni ngumu sana kutokana na hali mbaya ya kijiografia kwenye sehemu hizo, hata hivyo katika siku kadhaa tu serikali ya China ilituma watu wanaojitolea, askari na wahandisi wapatao laki kadhaa kwenda huko. Hii imeonesha kuwa serikali ya China ina uwezo mkubwa wa uongozi, na serikali hiyo inawajibika kihalisi kwa wananchi wake. Zaidi ya hayo, waziri mkuu wa China alikwenda kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa na kuamua mara moja kuhamasisha nguvu zote za kitaifa kushiriki kwenye kazi za uokoaji. Hii inaonesha kwamba serikali ya China ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na mambo ya dharura."

Bw. Luigi D' Angelo ni kiongozi wa kikundi cha waokoaji wa Italia, kazi yake ni kuratibu na kugawa vifaa vya misaada vinavyotolewa nchini China kutoka nchi za Ulaya. Alisema:

"Ushirikiano kati yetu na wizara ya mambo ya uraia ya China ni mzuri, shughuli zilipangwa vizuri na serikali za mitaa, na kwenye viwanja vya ndege hakuna vifaa vilivyokwama. Malori huwa yanakuwa tayari kabla ya vifaa vya nchi fulani kufika kwenye uwanja wa ndege na kusafirisjwa mara moja kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa, shughuli zote zinakwenda kama ilivyopangwa. Kutokana na ushirikiano mzuri kazi yetu inafanyika bila tatizo."

Bw. Grossi Favio na Bw. Vaccari Paolo ni wataalamu wa uokoaji baada ya maafa. Tarehe 18 walifika kwenye sehemu za maafa wakiwa pamoja na mizigo ya vifaa vya uokoaji. Bw. Grossi Fabio alisema, mshikamano mkubwa wa wananchi wa China unamshangaza sana. Alisema:

"Mshikamano mkubwa wa wananchi wa China umenishangaza sana. Watu wengi na waokoaji wamekuwa kama mashine kubwa inayofanya kazi kwa kushirikiana kila sehemu katika shughuli za uokoaji, na huduma za kikazi zinakwenda bila vurugu. Kazi za kimataifa za uokoaji huwa zinacheleweshwa kutokana na uzembe wa uongozi. Lakini idara za elimu kwenye sehemu za maafa nchini China zilitaka mahema yawe tayari mara tu baada ya sisi kufika, na kweli mahema yakawa tayari baada ya muda wa saa chache, na siku ya pili watoto waliweza kuanza kusoma ndani ya mahema." Bw. Vaccari Paolo alisema,

"Kinachonishangaza zaidi kwamba simu za mkononi ziliweza kutumika muda mfupi baada ya tetemeko la ardhi kutokea, hii imeleta hali nzuri ya kupashana habari za hali kuhusu maafa na kuwatuliza watu walioathirika, na pia imetupa urahisi wa kuwasiliana na idara yetu husika nchini Italia."

Bw. Di Agostino Miozzo mara nyingi alishiriki kwenye shughuli za kimataifa za uokoaji, ana uzoefu mkubwa kuhusu tetemeko la ardhi. Alisema:

"Nikiwa mtaalamu naona kuwa tetemeko la ardhi nchini China huenda litaleta maafa mengine, serikali inapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi ili kuepusha vifo vya watu kutokana na baridi baada ya mwezi Juni na magonjwa ya kuambukiza. Naamini serikali ya China itafanikiwa kabisa."