Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-03 14:54:08    
Mji wa Shouguang unaosifiwa kuwa kijiji cha uzalishaji wa mboga nchini China

cri

Mboga ni chakula kinachohitajika katika maisha ya kila siku. Tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, uzalishaji wa mboga umekuwa unapata maendeleo makubwa nchini China. Mwaka jana uzalishaji wa mboga ulizidi tani milioni 580, na uuzaji wa mboga katika nchi za nje ulichukua nafasi ya kwanza duniani.

Mji wa Shouguang uko katikati ya Peninsula ya Shandong, na una maliasili nyingi za kimaumbil na hali rahisi ya mawasiliano. Miaka 20 iliyopita, mkuu wa kijiji cha Sanyuanzhu cha mji huo Bw. Wang Leyi alivumbua mabanda ya kupanda mboga katika majira ya baridi, ambayo yalibadilisha historia ya watu wanaoishi kaskazini mwa China kuweza kula mboga za kabichi ya kichina na figili tu. Mji huo pia unasifiwa kuwa ni kijiji cha uzalishaji wa mboga nchini China. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa uuzaji wa nje wa mboga za mji huo, baadhi ya watu wamekuwa wanauita mji huo kuwa ni kikapu cha mboga duniani.

Lakini katika miaka kadhaa iliyopita, mboga zilizozalishwa mjini Shouguang hazikuuzwa vizuri kwenye masoko ya kimataifa. mkuu wa kampuni ya maendeleo ya kilimo cha kisasa ya Shijisanyuan cha mji huo Bw. Yin Yong alisema,

"Tulianza kuuza mboga nje mwaka 2000, ambapo tuliuza nyanya nchini Russia. Tunaweza kuzalisha nyanya kwa mwaka mzima kwenye mabanda ya mboga. Lakini tulishughulikia uuzaji wa mazao ya aina moja tu, hivyo tuliathiriwa zaidi na mabadiliko kwenye soko la kimataifa. Kwa mara ya kwanza mazao yetu hayakufikia vigezo vyao. Wana vigezo vikali kuhusu muda wa kuhifadhi na sura ya mboga. Tena wanakagua masalio ya dawa za kikemikali kwenye mboga. Kama mazao yetu hayafikii vigezo vyao, wanaataa kununua."

Mwaka 2002, mboga zilizozalishwa mkoani Shandong zilikataliwa nchini Japan mara kwa mara, na makampuni yanayozalisha mboga yalikabiliwa na shinikizo kubwa. Mtafiti wa idara ya mboga ya Taasisi ya sayansi ya kilimo ya mkoa wa Shandong Bw. Lang Fengqing alieleza kuwa, uuzaji wa mazao katika nchi za nje ulikabiliwa na matatizo kutokana na kuwa sifa ya mazao haifikii vigezo vya nchi zinazonunua mazao hayo, na nchi hizo kudhibiti uingizaji wa mazao kutoka nchi za nje. Alisema,

"Kwa mfano kama mahitaji ya mboga fulani kwenye soko la kimataifa ni madogo, nchi zinazonunua mazao zitaongeza vigezo vya kukagua mazao, ili kudhibiti uuzaji wa mboga kwenye soko la kimataifa, ambavyo vitaathiri wafanyabiashara wa mazao ya kilimo na wakulima wanaopanda mboga."

Kutokana na ushindani mkali kwenye soko la kimataifa, ili kupunguza shinikizo kubwa la makampuni yanayouzwa mboga katika nchi za nje, ni lazima makampuni hayo yachukue hatua kuinua sifa ya mboga. Mji wa Shouguang umefanya juhudi kuendeleza uzalishaji wa mazao unaofikia vigezo.

Ili kuwafanya wakulima wasizingatie kiasi cha uzalishaji tu na wasitumie ovyo dawa za kikemikali na dawa za kuua wadudu ambazo zinaweza kusababisha kupungua kwa sifa ya mboga, mji wa Shouguang ulitoa mwito wa kuendeleza kilimo cha uzalishaji mkubwa, sifa nzuri na ufanisi mkubwa. Na kuendeleza uzalishaji wa mazao unaofikia vigezo. Mtaalamu wa taasisi ya sayansi ya kilimo ya mkoa wa Shandong Bw. Jia Xi alieleza kuwa taasisi hiyo inafanya juhudi kutafiti uzalishaji unaofikia vigezo, alisema,

"Kwanza tunachagua aina za mboga na njia ya upandaji inayofaa uuzaji wa mazao katika nchi za nje, ili kuhakikisha mazao yanakuwa na sifa nzuri na kufikia vigezo vya kuuzwa nje. Kwa upande mwingine, tunafanya ukaguzi ukiwemo ukaguzi wa mabaki ya dawa za kuua wadudu na dawa za kikemikali. Hii pia ni kazi muhimu. Tunafanya uvumbizi wa kisayansi na teknolojia, ili kuzuia uzalishaji wa mboga zenye matatizo, na halafu tunafanya upimaji wa sifa. Tumetuma wataalamu kuongoza uzalishaji kwenye vituo vya uzalishaji wa mboga."

Kutokana na uungaji mkono wa kisera wa serikali na uelekezaji wa wataalamu, makampuni mengi yanayouza mboga katika nchi za nje na wakulima wanaopanda mboga mjini humo wananufaika moja kwa moja. Mwaka 2006 mji huo uliandikisha chapa ya "mboga za Shouguang", ambayo inamaanisha kuwa mboga zinazozalishwa huko zimefisiwa na watu kutokana na kuwa na sifa nzuri. Mji huo pia uliwekeza yuan milioni 12 kuanzisha kituo cha upimaji. Mboga zikipitishwa kwenye upimaji wa kituo hicho zitaweza kuuzwa katika nchi za nje bila ya kukaguliwa. Upimaji wa kituo hicho umekubaliwa na nchi zaidi ya 50 duniani, ambao unamaanisha kuwa chapa ya "mboga za Shouguang" inakubaliwa na nchi nyingi duniani. Mkuu wa kampuni ya maendeleo ya kilimo cha kisasa cha Shijisanyuan cha mji huo Bw. Yin Yong alisema,

"Hivi sasa mustakabali wa maendeleo ya masoko ni mzuri. Tuna kituo cha uzalishaji wa mimea ya mboga. Baada ya kuingia kwenye soko la kimataifa, mapato yameongezeka, ambayo yamewahimiza wakulima waendelee kufanya uzalishaji unaofikia vigezo."

Bw. Wang Leyi ambaye alianzisha mabadiliko ya uzalishaji wa mboga na anawaongoza wakulima wafanye juhudi kushughulikia uzalishaji huo. Pia alitoa mwito akiyataka makampuni ya uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini China yaendelee kukuza uzalishaji unaofikia vigezo, na kupima vizuri sifa ya mazao, alisema,

"Vyakula ni muhimu kwa maisha ya watu, na usalama wa vyakula ni muhimu sana. Ni lazima tuwe na moyo wa kuanzisha chapa maarufu, kufanya uzalishaji wa kuaminika, na kulinda sifa ya chapa maarufu ya mazao ya kilimo ya China. Tunawahudumia watu kwa mazao yenye sifa nzuri, kuendeleza uzalishaji wa mazao yanayofikia vigezo, kuimarisha udhibiti wa sifa kwenye uzalishaji, na kukamilisha utaratibu wa usimamizi wa usalama wa mazao, ili kutoa mazao ya kilimo yaliyo salama na yenye sifa nzuri.