Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-03 16:12:20    
Mkutano mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo FAO wafanyika

cri

Mkutano wa siku tatu wa viongozi wakuu kuhusu usalama wa chakula duniani unaoandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo duniani FAO unafanyika kuanzia tarehe 3 huko Rome. Wajumbe wa ngazi ya juu kutoka nchi na jumuiya za kimataifa zaidi ya 150 wanahudhuria mkutano huo. Ajenda kuu ya mkutano huo ni usalama wa chakula kutokana na changamoto za kupanda haraka kwa bei ya chakula, mabadiliko ya hali ya hewa na utengenezaji wa nishati kwa kutumia nafaka.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo, hivi sasa watu zaidi ya milioni 860 duniani wanakumbwa na tatizo la njaa, kwa hiyo kuondoa njaa ni moja ya malengo yanayotakiwa kufanyiwa juhudi za muda mrefu. Hivi sasa usalama wa chakula unakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na kupanda haraka kwa bei ya chakula. Katibu mkuu wa mkutano huo ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Bw. Alexander Muller alipozungumza na waandishi wa habari alisema,

"Kilimo kinakabiliwa na changamoto kubwa ambazo hazijawahi kutokea hapo kabla, bei ya chakula imefikia kiwango cha juu kabisa katika muda wa miaka 30 uliopita. Kutokana na hali ya miezi kadhaa iliyopita, tunajua kwamba wakazi wa mijini wanafanya maandamano kwa sababu ya kushindwa kumudu bei ya chakula, ghasia za kimabavu zilitokea mitaani na nchi kadhaa zilitokumbwa na vurugu za kijamii."

Bei kubwa ya chakula imewaletea watu shinikizo kubwa, uzalishaji wa nishati kwa kutumia nafaka umeleta mapambano kati ya magari na njaa, na utengenezaji wa nishati kwa kutumia nafaka unachukuliwa kuwa ni sababu kubwa ya kupanda kwa bei ya chakula. Wataalamu wengi akiwemo Bw. Alexander Muller wanaona kuwa uzalishaji wa nishati kwa kutumia nafaka haufai kuathiri usalama wa chakula na maendeleo endelevu duniani. Alisema,

"Kwa upande mmoja mahitaji ya chakula yanaongezeka na kwa upande mwingine mahitaji ya nishati yanaongezeka. Kilimo kinaweza kuzalisha nishati, lakini pia uwekezaji unatakiwa kufanyika kwa ajili ya kuzalisha nishati. Kwa hiyo kama njia yetu ni sahihi, uzalishaji wa nishati kwa kutumia nafaka unaweza kuwa ufumbuzi wa tatizo la nishati, maana nishati ya aina hiyo inatakiwa ifuate njia endelevu na isiathiri usalama wa chakula."

Kila nchi ina sera yake kuhusu namna ya kuendeleza nishati inayotengenezwa kwa nafaka na hakuna msimamo wa namna mmoja. Ili nchi hizo ziweze kufikia msimamo wa namna moja Bw. Muller alisema,

"Ni matumaini yangu kuwa pande mbalimbali zinaweza kuafikiana na kuwa na msimamo mmoja kuwa utengenezaji wa nishati kwa nafaka usiathiri usalama wa chakula. Tukiwa na msimamo huo tutaweza kupiga hatua ya kuwanufaisha watu maskini kutokana na uzalishaji huo wa nishati."

Wajumbe 2,500 wanahudhuria mkutano huo, ambao ni pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon na viongozi wakuu wa nchi zaidi ya 40. Watu wana matumaini kuwa mkutano huo utaweza kufikia msimamo wa namna mmoja kuhusu maendeleo endelevu ya kilimo. Bw. Muller alisema,

"Nafurahi kuona kwamba viongozi wengi wakuu wanahudhuria mkutano huo kwa nia ya kutafuta ufumbuzi na kuchukua hatua halisi. Ni matumaini yangu kwamba mkutano huo utatoa taarifa ya pamoja na kutoa ahadi kuhusu uwekezaji kwenye kilimo na kuchukua hatua za haraka, ni lazima tuunganishe hatua za muda mfupi na za muda mrefu, na hatua hizo zinategemea kutekelezwa na jumuiya ya kimataifa kwa pamoja."

Idhaa ya kiswahili 2008-06-03