Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-03 16:34:00    
Maskani ya kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama ?2?

cri

Katika kipindi hiki cha mashindano ya chemsha bongo ya mwaka huu kuhusu ujuzi wa vivutio vya utalii mkoani Guangxi, China, leo tunawaletea makala ya pili kuhusu Maskani ya kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama, kima hao wanaishi kwenye sehemu za milima mikubwa mjini Chongzuo mkoani Guangxi.

Kabla ya kuanza kusoma makala hii ya kwanza, tunatoa maswali mawili: 1. Mbali na mkoa wa Guangxi, China, kuna sehemu nyingine duniani ambazo pia zina kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama? 2. Hivi sasa bado kuna kima wangapi wenye vichwa vyeupe? Tafadhali sikilizeni kwa makini ili muweze kupata majibu kutoka kwenye makala tunayowasomea.

Kwenye sehemu za milima mikubwa na bonde mjini Chongzuo mkoani Guangxi, wanaishi kima watundu wanaopendeza, kima hao wana vichwa ambavyo manyoya meupe yanasimama juu yake, vichwa vyao ni kama vimevaa kofia ndogo nyeupe zenye ncha, na sehemu ya shingo na mabega za kima hao pia zina rangi nyeupe, na mikia yao mirefu pia ina rangi nyeupe. Kima wa aina hiyo walianza kuishi kwenye sehemu hiyo zaidi ya miaka milioni 2.5 iliyopita, na mimea na wanyama waliokuwepo wakati huo pamoja na kima wa aina hiyo, wengi wametoweka. Hivi sasa kuna kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama zaidi ya 700 tu, tena kima hao wanaishi kwenye sehemu ya Chongzuo tu, kima hao ni adimu zaidi kuliko panda wanaojulikana duniani.

Asubuhi ya siku moja, waandishi wetu wa habari walifika kwenye hifadhi ya mazingira ya asili ya kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama huko Chongzuo mkoani Guangxi. Eneo la hifadhi hiyo ni kilomita 24 za mraba, ambapo kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama ambao ni kundi kubwa zaidi la kima wa aina hiyo duniani. Waandishi wetu wa habari waliona kuwa, kwenye miamba mikali, kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama wapatao 6 au 7 walikuwa wanakula majani na matunda ya miti, na walichezacheza kama watundu, miamba mikali kwao ni kama sehemu ya tambarare waliruka na kutembea bila shida. Mkazi wa kijijini Xiao Wang alisema:

"Kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama ni marafiki wa wanakijiji wa huko, kwani watu wote wanajua, kima kama hao ni adimu sana duniani, wanaishi kwenye sehemu yetu tu, hivyo ni wenye thamani kubwa, sisi sote tunawalinda".

Xiao Wang ni m-miao, waandishi wetu wa habari walipokwenda nyumbani kwake kwanza walizuiliwa mlangoni, walitakiwa kunywa kwanza pombe ya kuingia mlangoni, desturi hii ya kabila la wamiao ambayo huonekana wakati watu wa kabila hilo wanapofanya sherehe ya kufunga ndoa, wenyeji wanapowakaribisha wageni, huweka pombe mbele ya mlango wa nyumba, wageni wakinywa pombe ndiyo wameonesha urafiki kwa wenyeji, ambapo wenyeji na wageni huimba nyimbo za kutoa pongezi na kutoa shukrani, hali ya furaha ilijaa huko. Hivi sasa kila wageni wanapofika nyumbani kwa watu wa kabila la wamiao, wenyeji huwapa pombe kuwakaribisha. Nyumbani kwa Xiao Wang, aliwaelezea waandishi wetu wa habari hadithi kuhusu kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama. Alisema:

"Zamani sana sehemu hiyo ilikuwa ni yenye hali ya umaskini sana, wanakijiji walikuwa wanakumbwa na njaa mara kwa mara. Siku moja mzee mmoja alifariki dunia, wanakijiji ambao vichwa vyao vilifungwa kwa kitambaa cha rangi nyeupe na kufunga mkanda wa rangi nyeupe viunoni walimzika mzee huyo kwenye mlima. Baada ya mazishi, watoto waligundua matunda mengi mlimani waliyala kwa furaha, halafu walichezacheza mlimani. Wazazi wao waliona watoto wao walicheza kwa furaha, wakakubali wabaki mlimani. Siku za baadaye, kijiji hicho kilianza kuwa na utajiri siku hadi siku, wazazi hao waliwakumbuka watoto wao na kutaka watoto hao warudi nyumbani, lakini watoto hao waliwaambia kuwa, walitaka kubaki mlimani, kwani nyumbani kwao kijijini hakuna chakula kingi. Hivyo watoto hao wakaishi mlimani, siku nenda siku rudi, watoto hao walikuwa wazima na wakafunga ndoa, wakazaa watoto, lakini sura za watoto wao zilibadilika, vitambaa vyeupe vilivyowahi kufungwa vichwani mwao vimebadilika kuwa manyoa meupe, na mkanda wa rangi nyeupe uliofungwa viunoni mwao ukabadilika kuwa ni mikia mirefu myeupe".

Profesa wa Chuo Kikuu cha Beijing Bw. Pan Wenshi anayefanya utafiti na uhifadhi wa kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama amekaa kwenye sehemu ya Chongzuo zaidi ya miaka 10 iliyopita, aliwaambia waandishi wetu wa habari kuwa, mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, kwenye sehemu ya Chongzuo, walikuwepo kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama zaidi ya 2000. Lakini idadi ya kima wa aina hiyo ilipungua kwa kiasi kikubwa, ilipofika mwaka 1996, kima wa aina hiyo wamebaki zaidi ya 90 tu. Profesa Pan alisema, shughuli za binadamu zinazoongezeka kama vile kuchoma majani na miti mlimani ili kuendeleza kazi ya kilimo kumeshambulia eneo wanaloishi wanyama pori, na wahalifu fulani waliwawinda kiharamu wanyama hao, hivyo idadi ya kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama imepungua kwa kiasi kikubwa. Profesa Pan alisema:

"Kama tunaweza kuzuia kabisa uwindaji haramu, na kufufua mazingira ya asili ya eneo wanaloishi wanyama, naamini kuwa kima wa aina hiyo wataongezeka. Wanyama wengi ambao wako hatarini kutoweka kama watapata muda wa kutosha na nafasi za kutosha kwenye mazingira ya asili, hakika wataongezeka".

Profesa Pan alisema kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama wanafuata kwa makini kanuni zao za maisha, kila asubuhi na jioni wanakula chakula na kuchezacheza mlimani, wanapumzika adhuhuri mlimani, na usiku wanarudi mapangoni mwao kulala. Alisema kama binadamu wanaweza kuwasaidia kima hao kuishi katika mazingira ya asili waliyoishi hapo awali hakika watazaliana na kuishi vizuri kwenye sehemu hiyo. Serikali ya Chongzuo ilifanya kazi nyingi ili kufufua mazingira ya eneo wanaloishi kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama. Bw. Wei Xin wa idara ya utalii ya Chongzuo alisema:

"Ili kulinda mazingira ya viumbe ya sehemu hiyo, serikali ya Chongzuo imesaidia kila familia kujenga shimo moja la kutumia gesi ya kinyesi, kuwasaidia wakazi kupata ujuzi wa kujenga shimo na kutumia gesi ya kinyesi. Hivi sasa wakazi wengi wa sehemu hiyo wanatumia gesi ya kinyesi kuwasha taa na kupika chakula. Serikali pia inawaelekeza wakulima kupanda mazao ya biashara ili kupata mapato bila kuathiri mazingira ya viumbe".

Tokea miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya Chongzuo imepiga marufuku vitendo vya kuchoma majani mlimani kwa ajili ya kulima mazao, kueneza ufundi wa kujenga shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi ili kuitumia, kupunguza hali ya kukata miti ili kupata kuni za kupikia chakula, na kuwahamasisha wakulima kupanda miwa, mahindi na mpunga ili kuongeza kipato, hivyo maisha ya wakulima yameboreshwa, hali hii imeepusha binadamu na kima wenye thamani kunyang'anyana nafasi kwenye mazingira, hivyo mazingira ya asili yanaboreshwa siku hadi siku, ambapo hali asili ya eneo wanaloishi kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama inafufuliwa vizuri siku hadi siku, idadi ya kima wa aina hiyo inaongezeka na kufikia zaidi ya 700. Hivi sasa wanakijiji wa huko wanalinda kwa hiari mazingira ya viumbe na kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama. Mwanakijiji Bw. Zhao alisema:

"Hivi sasa sisi sote hatuendi mlimani kukata miti kwa ajili ya kupata kuni, tunapaswa kuhifadhi vizuri maliasili ya viumbe ili kuwapatia mazingira mazuri ya kuishi kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama".

Tokea kuanzishwa kwa hifadhi ya mazingira ya asili ya kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama mwaka 2002 kwenye sehemu ya Chongzuo, shughuli za utalii za sehemu hiyo pia zimeanzishwa. Labda wasikilizaji wetu wanaweza kuwa na wasiwasi, kuendeleza shughuli za utalii kama kutaweza kuharibu mazingira ya asili wanayoishi kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama? Kwani mazingira hayo yamefufuliwa si muda mrefu uliopita. Profesa Pan alituambia, kuendeleza shughuli za utalii kwenye mazingira ya asili, kunaweza kuleta nafasi mpya za ajira kwa wakulima wa sehemu hiyo, na kuboresha maisha ya wakazi wa huko siku hadi siku, ili kupanua zaidi eneo la hifadhi ya mazingira ya asili, na kuviwezesha viumbe vya huko viongezeke kuwa vya aina nyingi zaidi. Profesa Pan alisema:

"Kuendeleza shughuli za utalii kwenye sehemu hiyo, si kama tu tunaweza kuwalinda kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama, bali pia tunaweza kuwawezesha wakazi wa sehemu hiyo waboreshe maisha yao siku hadi siku. Kuendeleza shughuli za utalii kwenye sehemu ya kulinda mazingira ya asili, kunaweza kuwafanya watu wa vizazi vya baadaye waishi maisha mazuri zaidi kuliko ya sasa".

Profesa Pan alidhihirisha kuwa, kuendeleza shughuli za utalii ni lazima kuweka malengo wazi na kuwashirikisha watu kwa mpango mwafaka, na haifai kuendeleza shughuli za utalii kupita kiasi, ili kulinda mazingira ya asili na kupata maendeleo endelevu bila kusita.

Kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama wanaopendeza ni marafiki wa binadamu. Kwenye sehemu ya Chongzuo mkoani Guangxi, wakulima wa huko wanaishi pamoja na kima hao wenye thamani kubwa katika mazingira yenye hali ya mapatano.

Sasa tunarudia maswali mawili ya leo: 1. Mbali na mkoa wa Guangxi, China, kuna sehemu nyingine duniani ambazo pia zina kima wenye vichwa vyenye manyoya meupe yaliyosimama? 2. Hivi sasa bado kuna kima wangapi wenye vichwa vyeupe?

Idhaa ya kiswahili 2008-06-03