Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-04 18:29:13    
Jumuiya ya kimataifa yajadili usalama wa chakula duniani

cri

Mkutano wa viongozi kuhusu usalama wa chakula duniani ulianza kufanyika tarehe 3 kwenye makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo FAO huko Rome. Kutokana na kupanda kwa juu kwa bei ya chakula, mkutano huo umekuwa unafuatiliwa sana. Ajenda ya mkutano huo ni "changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na matumizi ya nafaka katika kutengeneza nishati". Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon kwenye mkutano huo alitoa hotuba muhimu na kutoa onyo la tahadhari kutokana na hali mbaya aliyojionea. Alisema, ".

"Hivi karibuni, huko Liberia nilijionea kwamba hapo kabla watu walinunua mchele kwa mifuko, lakini sasa wananunua kwa vikombe. Nchini Cote d'Ivoire viongozi waliniambia kwamba wana wasiwasi mkubwa wa kutokea tena kwa vurugu za kijamii baada ya migogoro ya kimabavu kumalizika hivi karibuni na kuufanya ukarabati unaofanyika sasa uwe bure. Tuna wasiwasi kwamba hali hiyo itatokea tena nchini Afghanistan, Haiti na Liberia, nchi ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zinapata maendeleo kutokana na misaada ya Umoja wa Mataifa."

Kwa mujibu wa takwimu za FAO, tokea mwaka 2006 bei ya chakula duniani ilipoanza kupanda, hadi kufikia mwaka 2007 imepanda kwa 24%, na katika miezi mitatu ya mwanzo mwaka huu bei ya chakula imepanda kwa 53% ikilinganishwa na ile ya mwaka jana wakati kama huu. Kutokana na ongezeko la idadi ya watu, mahitaji ya chakula pia yanaongezeka. Mkurugenzi mkuu wa FAO Jacques Diouf alisema,

"Hivi sasa idadi ya watu duniani imefikia bilioni sita, hadi kufikia mwaka 2050 idadi hiyo itaongezeka na kuwa bilioni tisa. Ili kukidhi idadi kubwa hiyo ya watu tunalazimika kuongeza mazao tuliyo nayo sasa kwa mara mbili."

Kutokana na hali hiyo, kuhakikisha usalama wa chakula limekuwa ni suala linalofuatiliwa sana. Watu wanaohudhuria mkutano huo wanaona kuwa chanzo cha kupanda kwa bei ya chakula ni pamoja na upungufu wa akiba duniani, nchi zinazozalisha nafaka kwa wingi zimepungukiwa mavuno, na pia inatokana na uhamisho wa mitaji kwenye biashara kubwa ya kilimo kutokana na thamani ya dola za Marekani kushuka na kupanda kwa bei ya mafuta. Katika hotuba zao, baadhi ya wajumbe wa nchi na jumuiya walisema, maendeleo ya haraka ya nchi zinazoinuka kama China na India yamesababisha ongezeko la mahitaji ya mazao na kusababisha kupanda kwa bei ya chakula. Kuhusu suala hilo, mjumbe wa serikali ya India ambaye pia ni waziri wa kilimo wa nchi hiyo Bw. Sharad Pawar alisema,

"Mheshimiwa mwenyekiti, tumesikia mengi kuhusu usemi ambao maendeleo ya uchumi yamesababisha kupanda kwa bei ya chakula. Lakini takwimu za FAO zimeonesha wazi kwamba bei kubwa ya chakula haisababishwi na maendeleo ya uchumi wa nchi hizo. Ukweli wa mambo umethibitisha kwamba mahitaji makubwa ya mahindi na mbegu za rapa kwa ajili ya kutengeneza dizeli na alcohol na bei ya juu ya mafuta ndio chanzo cha kupanda kwa bei ya chakula".

Mjumbe wa China ambaye pia ni waziri wa kilimo Bw. Sun Zhengcai alisema,

" 'Usalama wa chakula kwa kila mtu' ni msingi wa haki za binadamu, kupata chakula bora ni matumaini na haki ya watu wa nchi zinazoendelea na pia ni ishara muhimu ya maendeleo ya dunia. Kuzibebesha lawama nchi zinazoendelea au sera fulani za nchi fulani kuhusu suala la ongezeko la mahitaji ya chakula na kupanda kwa bei sio halali, na wala sio msimamo wa kujenga."

Bw. Sun Zhengcai alitoa mapendekezo matano ya kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa na kuhakikisha usalama wa chakula duniani.