Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-05 15:18:35    
Mpiga piano maarufu wa China Li Jian

cri

Bw. Li Jian alizaliwa miaka 43 iliyopita katika familia ya wanamuziki mjini Shanghai China, yeye ni pandikizi la mtu mwenye mikono mikubwa na nguvu. Ingawa si mtu hodari kwa kuongea, lakini anapozungumzia muziki wa piano maneno yake hayaishi. Mama yake Yu Li ni mpiga fidla mashuhuri nchini China, muziki alioupiga unaoitwa "Mapenzi kati ya Liang Shanbo na Zhu Yingtai" hadi sasa bado ni muziki aliopiga vizuri kabisa kuliko wengine walioupiga. Bw. Li Jian alipokuwa na umri wa miaka sita, mama yake alianza kumfundisha kupiga fidla, lakini yeye alipenda zaidi kujifunza upigaji piano. Alisema, .

"Sababu ya kutaka kujifunza kupiga piano ilikuwa ni ujanja wa kukimbia uchovu wa kupiga fidla kwa kusimama. Kwa sababu mama yangu ni mpiga fidla, ni kawaida kwa yeye kutaka nijifunze upigaji fidla, lakini nilipojifunza kupiga ala hiyo nilisikia uchovu kutokana na kusimama saa mbili, lakini kupiga piano kwa kukaa ni starehe. Mwanzoni sikuwa na hamu ya kujifunza kupiga piano mpaka nilipotimiza umri wa miaka 12."

Bw. Li Jian alisema, alipokuwa na umri wa miaka 10 alipata ugonjwa mkubwa na nusura apoteze maisha yake. Baada ya kupona alianza kupenda muziki na hasa muziki wa piano. Tokea hapo alikuwa anajituma kujifunza kupiga piano, kila siku alipiga piano kwa zaidi ya saa 12, ufundi wake ulikuwa unaongezeka haraka.

Mwaka 1981 alipokuwa na umri wa miaka 16 alijipatia umaarufu kutokana na kupata tuzo kubwa kwenye mashindano ya kimataifa ya muziki wa piano huko Paris Ufaransa. Wakati huo alikuwa mwanamuziki mdogo kabisa aliyepata tuzo hiyo kati ya washiriki wengi. Kutokana na tuzo hiyo alipata udhamini wa masomo uliotolewa na serikali ya Ufaransa katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Pierre Sancan mjini Paris.

Bw. Li Jian baada ya kuwa mtu maarufu, mara kwa mara alikuwa anafanya maonesho ya muziki huku na huko duniani. Mwaka 1987 akiwa pamoja na kundi la muziki la Aiyue la China alikwenda Marekani kufanya maonesho ya muziki. Kutokana na uhodari wake aliwavutia sana wasikilizaji wa Marekani na popote alipoonekana alikaribishwa sana na wasikilizaji. Kuanzia hapo kila mwaka Li Jian alikuwa anafanya maonesho yake Marekani, nchi za Ulaya na nchi za Mashariki ya Mbali, muziki aliopiga ni pamoja na muziki wa piano pekee na muziki wa piano uliosaidiwa na bendi ya okestra.

Kujifunza upigaji piano na kufanya maonesho katika nchi za Magharibi kulimpatia nafasi ya kuona na kujifunza mengi.

Bw. Li Jian anapenda sana muziki wa kale wa Magharibi, kila alipopiga muziki wa kale alikuwa anaonesha vya kutosha hisia alizopata kutoka kwenye muziki wenyewe, anaona kuwa muziki wa kale wa Magharibi unategemea mpigaji anavyouelewa muziki wenyewe, kwa hiyo ingawa ni muziki mmoja, lakini unapigwa kwa namna tofauti na wanamuziki wengine, kwa sababu kila mpigaji ana ufahamu wake kuhusu muziki anaoupiga. Alisema,

"Hapo awali muziki ulianza kutokea kanisani ambao ulikuwa ni kwa ajili ya kusifu mambo nje ya dunia. Eneo la muziki wa kale ni kubwa kama bahari, ukizama ndani ya bahari hiyo hutaki kutoka, na katika bahari hiyo kuna muziki wa aina nyingi. Ninachotaka kusema ni kwamba muziki wa kale ni muziki pekee usiotumia kikuzasauti na umeme, haidhuru kama hamna umeme wakati muziki wa kale unapopigwa."

Muziki anaopiga Li Jian unagisa sana hisia za wasikilizaji, kwa mfano, simfoni ya nne ya Beethoven na muziki wa piano wa nne unaosaidiwa na bendi ya okestra. Muziki huo unatofautiana na muziki mwingine nane wa simfoni, kwani zinaonesha zaidi hisia za upole, hamasa za ujana na ukakamavu imara. Muziki anaoupiga huonesha zaidi hisia za upole za Beethoven ambazo hupuuzwa na wasanii wengine, ili kuwaachia wasikilizaji wahisi na waelewe wenyewe. Bw. Li Jian anaona kuwa wapiga piano wanapaswa kuonesha vilivyo hisia za watunzi muziki, na wala sio kuonesha hisia zao wenyewe. Alisema,

"Mtindo binafsi wa wanamuziki haufai kuoneshwa, lakini kuna wanamuziki wengi wanapopiga muziki wanajitahidi kuonesha mtindo wao wenyewe badala ya mtindo wa watunzi wa muziki. Mtindo wa wanamuziki hakika utaoneshwa wakati wanapoonesha mtindo wa watunzi wa muziki."

Katika muda wa miaka kadhaa iliyopita, Bw. Li Jian alifanya maonesho mengi huku na huko duniani. Hadi sasa amechapisha CD 13. Ingawa Bw. Li Jian ni mwanamuziki mashuhuri duniani lakini anaishi maisha ya kawaida kabisa, anaona kuwa wanamuziki wanapaswa wawe watulivu na wenye juhudi katika shughuli za muziki, kwa hiyo anapinga shughuli zote za maingiliano ya kijamii na kujifungia nyumbani akijizamisha katika dunia yake ya muziki. Alisema,

"Napenda kuburudika na kompyuta na kutengeneza vitu ninavyopenda kama taa za mezani na vitu vingine. Taa nyingi ninazotumia nyumbani kwangu nilizitengeneza mwenyewe kwa kutumia karatasi za kutupwa. Na vile vile napenda mashindano ya mpira wa miguu na kuendesha pikipiki kupita huku na huko barabarani."

Idhaa ya kiswahili 2008-06-05