Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-06 15:44:40    
Ushirkiano wa elimu kati ya China na Afrika

cri

Mwandishi wetu wa habari hivi karibuni alikutana na mkenya Bi. Maria Dwamba anayesomea shahada ya udaktari kwenye chuo kikuu cha kilimo cha Nanjing. Bi. Maria Dwamba pia ni mwanafunzi aliyetumwa na chuo kikuu cha Egerton cha Kenya kwa ajili ya mawasiliano kati ya chuo kikuu cha Egerton na chuo kikuu cha kilimo cha Nanjing. Bi. Maria Dwamba alisema,

"Sasa ninachukua kozi ya sayansi ya vyakula na miradi, hasa ninafanya utafiti wa ngano. Taaluma hiyo ni muhimu sana, kama tutashika ujuzi, tutaweza kuhimiza maendeleo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini Kenya."

Chuo kikuu cha Egerton ni chuo kikuu cha kwanza nchini Kenya kilichoshiriki kwenye miradi ya ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya China na Kenya. Tangu mwaka 2000 chuo kikuu cha kilimo cha Nanjing na chuo kikuu cha Egerton vilianzisha uhusiano wa ushirikiano, na kuanza kutumiana walimu ili kufanya mawasiliano. Ushirikiano kati ya vyuo vikuu viwili ni moja wapo ya miradi ya ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika. Tangu mwaka 2000 baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lilipoanzishwa, ushirikiano na mawasiliano kati ya China na Afrika katika sekta ya elimu ziliimarishwa siku hadi siku, ambazo zimekuwa ni sehemu muhimu ya ushirikiano kati ya China na Afrika.

Kwa kweli, miaka ya 50 ya karne iliyopita, China na Afrika zimeanza kufanya ushirikiano katika sekta ya elimu. Wakati ule Jamhuri ya watu wa China iliyoanzishwa muda mfupi uliopita, ilianza kuwapokea wanafunzi kutoka nchi za Afrika. Katika miaka kadhaa nchini China iliwapokea wanafunzi mia kadhaa kutoka nchi za Afrika zikiwemo Misri, Kenya na Uganda. Mwishoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita China ilianza kutekeleza mpango wa mradi wa utafiti wa elimu ya vyuo vikuu. Kutokana na mpango huo, China ilitoa zana za ufundishaji na utafiti wa kisayansi kwa vyuo vikuu barani Afrika, kutuma walimu kwenye vyuo vikuu vya Afrika, na kuwasaidia walimu wa Afrika kufanya utafiti wa sayansi. Mkurugenzi wa ofisi ya ushirikiano na mawasiliano ya kimataifa ya wizara ya elimu ya China Bw. Xue Yanqing alijulisha kuwa zamani utoaji misaada kwa Afrika ilikuwa ujenzi wa miundo mbinu na msaada wa fedha. Alisema,

"Zamani China ilitoa misaada kwa nchi za nje katika ujenzi wa miundo mbinu, kwa mfano wa kuzisaidia kujenga majengo, barabara, hata kutoa fedha moja kwa moja. Lakini kuanzia karne ya 21, maendeleo ya Afrika yanahitaji watu wengi wenye ujuzi."

Baada ya kuingia kwenye karne mpya, ili kukabiliana na mabadiliko ya hali mpya na maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika, China ilifanya mageuzi kuhusu kazi ya utoaji misaada kwa Afrika, na kutoa elimu na mafunzo kwa waafrika kumekuwa njia muhimu ya ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika. China iliwachagua vijana wa nchi za Afrika wanaoshughulikia mambo ya utafti wa sayansi waje nchini China kushiriki kwenye utafiti wa ngazi ya juu, vilevile ilitenga fedha kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa watu wenye ujuzi wa sekta mbalimbali barani Afrika. Njia hizo za utoaji msaada zimepata mafanikio makubwa tangu ulipotekelezwa. Hivi sasa ushirikiano kati ya China na Afrika umepata maendeleo makubwa katika sekta za kilimo, vyombo vya habari, miradi ya upashanaji wa habari, matibabu na afya.

Kwenye mkutano wa sita wa kazi ya kutoa misaada ya elimu na kuzisaidia nchi zinazoendelea kuwaandaa watu wenye ujuzi, uliofanyika hivi karibuni mjini Nanjing, naibu waziri wa elimu wa China Bw. Zhang Xinsheng alijulisha mafanikio yaliyopatikana katika ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika katika miaka kadhaa iliyopita. Akisema,

"Tokea mwaka 2000 wizara ya elimu ya China ilitenga fedha na kuandaa semina 54 kwenye vyuo vikuu vinavyobeba majukumu ya kutoa misaada kwa nchi za nje. Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2007 China ilipokea wanafunzi 19,948 kutoka nchi za Afrika. Kati ya wanafunzi hao wa Afrika, kuna wanafunzi 12,156 waliopewa udhamini wa masomo na serikali ya China."

Udhamini wa masomo aliotaja Bw. Zhang ni udhamini maalumu wa masomo ulioanzishwa na serikali ya China na vyuo vikuu mbalimbali kwa ajili ya kutoa misaada ya kifedha kwa wanafunzi wa Afrika. Hivi sasa China inaongeza zaidi idadi ya wanafunzi wanaopewa udhamini wa masomo, ili kuwavuta vijana wengi zaidi vya nchi za Afrika kusoma nchini China. Bw. Zhang Xinsheng alisema,

"Mwaka 2007 wanafunzi 2,733 wa Afrika walipewa udhamini wa masomo nchini China, idadi hiyo ilichukua asilimia 26.9 ya ile ya jumla ya wanafunzi wote wa nchi za nje waliopewa udhamini wa masomo. Mwaka 2009 tutaongeza idadi ya wanafunzi wa Afrika watakaopewa udhamini wa masomo nchini China kufikia elfu nne."

Licha ya kutoa udhamini wa masomo nchini China kwa wanafunzi wa nchi za Afrika, wizara ya elimu ya China na vyuo vikuu husika pia vinatafuta mfumo wa kutuma walimu barani Afrika, na kuanzisha vituo vya misaada ya elimu barani Afrika.

Wasikilizaji wapendwa mliosikia maelezo kuhusu ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika. Katika kipindi kijacho tutaendelea kuwaleteni maelezo kuhusu maendeleo mapya ya ushirikiano huo. Kwa herini.

Idhaa ya kiswahili 2008-06-06