Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-10 15:55:34    
Waziri mkuu wa Iraq asema ziara yake nchini Iran imefanikiwa

cri

Waziri mkuu wa Iraq Bw Nouri Al-Maliki tarehe 9 alimaliza ziara yake nchini Iran, na kabla ya kuondoka mjini Teheran alisema ziara yake imepata mafanikio makubwa?na ana matumaini kuwa mafanikio hayo yatasukuma mbele maendeleo ya urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Bw. Nouri Al-Maliki alifika mjini Teheran Tarehe 7 na kuanza ziara yake nchini Iran. Hii ni mara ya pili kwa waziri mkuu huyo kufanya ziara nchini Iran katika mwaka mmoja, na hii inaonesha kwamba Iraq inazingatia sana uhusiano kati yake na Iran. Alipokuwa ziarani huko Iran Bw Nouri Al-Maliki kwa nyakati tofauti alifanya mazungumzo na kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, rais Mahmoud Ahmadinejad na spika wa bunge Bw Ali Larijani, mazungumzo yao yalihusu masuala ya usalama, nishati na ushirikiano wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi.

Lengo la ziara ya Bw Nouri Al-Maliki ni kuielezea Iran "Makubaliano kuhusu Hadhi ya Jeshi la Marekani Nchini Iraq" ambayo yanazungumzwa sasa. Hivi karibuni "Makubaliano kuhusu Hadhi ya Jeshi la Marekani Nchini Iraq" yaliyotolewa na Marekani yamesababisha wasiwasi mkubwa na upinzani mkali wa Iran. Ayatollah Khamenei alipokutana na Nouri Al-Maliki alisema tatizo kubwa linaloikabili Iraq kwa sasa ni kuwepo kwa majeshi ya nchi za nje zinanazoongozwa na Marekani nchini humo, hiki ni kikwazo kikuu kwa Iraq kutimiza umoja wa kitaifa. Lakini jibu la Bw. Maliki liliondoa wasiwasi wa Iran.

Kwanza, kwa niaba ya serikali ya Iraq Bw. Maliki alisema Iraq inazingatia usalama nchini Iraq, pia inazingati sana usalama wa Iran. Iraq haitaruhusu ardhi yake itumiwe kwa kuidhuru Iran. Bw. Maliki pia alisisitiza kuwa "Makubaliano kuhusu Hadhi ya Jeshi la Marekani nchini Iraq" kati ya Iraq na Marekani hayataidhuru Iran hata kidogo.

Pili, Iraq na Iran zimesaini waraka wa kumbukumbu ya maelewamo kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili. Tarehe 8 Mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo mbili walionesha matumaini ya kuimarisha ushirikiano huo kati ya nchi zao wakiona kuwa ushirikiano wa kijeshi utaleta amani na utulivu kwenye kanda yao, kisha pande mbili zilisaini waraka huo katika siku ya pili. Waraka huo unasema Iran na Iraq zitafanya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kijeshi ili kuhimiza amani na utulivu katika kanda yao.

Tatu, licha ya kutuliza moyo wa Iran Bw. Maliki pia amepata uungaji mkono kutoka Iran kuhusu usalama na ukarabati wa Iraq.

Kwenye mazungumzo na rais Ahmadinejad, Bw. Maliki alisema Iraq na Iran zinapaswa kusukuma mbele ushirikiano wa pande mbili katika fani mbalimbali, hii inasaidia sana Iraq kupata maendeleo na utulivu. Alisisitiza kuwa utulivu wa Iraq unasaidia sana kulinda usalama wa kikanda na hata dunia nzima. Bw. Ahmadinejad alisema nchi jirani za Iraq, nchi washirika na hata Umoja wa Mataifa, zote zinapaswa kuisaidia Iraq kurudisha utulivu na amani, na nchi jirani za Iraq zinapaswa kutoa mchango mkubwa zaidi. Spika wa bunge la Iran Bw. Ali Larijani alipokutana na Bw. Maliki alisema, utulivu na usalama wa Iraq unalingana na maslahi ya nchi zote kwenye kanda hiyo ikiwemo Iran. Ili kuikarabati Iraq, hali ya amani na utulivu ni ya lazima, na Iran inapenda kutoa mchango muhimu katika ukarabati huo.

Vyombo vya habari vinaona kuwa ziara ya Bw Al Maliki imefikia lengo alilotaka, yaani kufafanua kuhusu "Makubaliano kuhusu Hadhi ya Jeshi la Marekani Nchini Iraq", kutuliza moyo wa Iran, na huku amepata uungaji mkono kutoka Iran kuhusu usalama na ukarabati wa Iraq.