Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-10 18:21:32    
Sehemu ya mpakani inayopendeza na yenye miujiza mkoani Guangxi, China

cri

Mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang wa Guangxi uko kwenye sehemu ya mpaka wa kusini magharibi mwa China, mkoa huo unapakana na nchi ya Vietnam?mkoa huo ni moja kati ya sehemu muhimu ya mipakani nchini China. Leo tunawaongoza kutembelea sehemu ya mpaka nchini China na kuhisi mvuto wa mandhari nzuri ya mazingira ya asili na vivutio vya utalii na utamaduni kwenye mkoa wa Guangxi.

Kwanza tunatoa maswali mawili, mnatakiwa kusikiliza kwa makini makala tutakayosoma ili muweze kuyajibu. 1. Kinanda cha kale cha kabila la wazhuang kinaitwaje? 2. Maporomoko ya maji ya Detian yako kwenye sehemu ya mpaka kati ya China na nchi gani?

Kama tukifunga safari kuelekea magharibi kutoka Nanning, mji mkuu wa Mkoa wa Guangxi, baada ya saa moja na nusu tutafika kwenye Wilaya ya Ningming ya Mji wa Chongzuo inayopakana na nchi ya Vietnam. Katika Wilaya ya Ningming, mabaki ya michoro ya kale kwenye miamba yaliyoko kando ya Mto Zuojiang ni maarufu zaidi. Michoro hiyo ya kale iko kwenye Miamba mirefu kando ya mto, uchunguzi uliofanyika umethibitisha kuwa michoro hiyo imekuwa na historia ya zaidi ya miaka elfu 2, ambayo ilichorwa na mababu wa watu wa kabila la wazhuang.

Tukipanda meli kutembelea Mto Zuojiang, tunaweza kuangalia michoro hiyo ya kale kwenye miamba. Michoro hiyo inaonekana kuwa ya rangi nyekundu, michoro mingi ni ya binadamu, pia kuwa wanyama, vyombo au alama kadha wa kadha za maumbo, michoro yenyewe ni mikubwa na yenye urefu wa zaidi ya mita 200, na kimo cha mita 40. Na binadamu wote kwenye michoro hiyo ni wanaocheza dansi, ama wananyanyua mikono miwili juu, ama wanachuchumaa, ambao walionesha hali ya zama za asili yenye miujiza. Wataalamu walitafsiri kuwa, michoro hiyo ilionesha hali ya watu walivyovuna mazao, au waliofanya matambiko. Lakini katika zama za kale, mababu wa kabila la wazhuang walikuwa wanawezaje kuchora michoro kwenye miamba mirefu namna hii? Je, walitumia rangi ya namna gani ambayo haichuji baada ya maelefu ya miaka kupita? Maswali kama hayo yanatakiwa kuendelea kufanyiwa utafiti na wataalamu.

Watalii wakitembelea kwenye Mto Zuojiang, huwa wanaweza kusikia sauti ya nyimbo zinazoimbwa na wasichana wa kabila la wazhuang wa sehemu hiyo. Wasichana hao wenye sauti nyororo, kila mmoja anashika kinanda kimoja kinachoitwa Tianqin, ambacho ni kinanda maalum cha muziki cha kabila la wazhuang kilichokuwepo zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Zamani waganga wa kienyeji walitegemea vinanda vya Tianqing kueleza masimulizi ya kuonesha shughuli mbalimbali za uganga wao, na kuwasaidia watu kuondokana na maafa na kuwaombea baraka na fanaka. Hivi sasa wazhuang wanapiga vinanda vya Tianqing kuimba nyimbo za kienyeji.

Mliosikia ni wimbo uitwao " Mkoa wa Guangxi unaopendeza" walioimba wasichana wa kabila la wazhuang huku wakipiga vinanda vya Tianqing.

Baada ya kuangalia michoro yenye miujiza kwenye miamba na kusikiliza wimbo walioimba wasichana wa kabila la wazhuang, tulipanda gari kuelekea tena magharibi, baada ya saa moja hivi tulifika kwenye mji mdogo waw Pingxiang ulioko kwenye sehemu ya mpakani. Mlango wa Urafiki kwenye sehemu hiyo ya mpaka kati ya China na Vietnam ni sehemu muhimu yenye vivutio vya utalii. Nchini China kuna "milango tisa maarufu kwenye sehemu ya mpaka", kama vile Mlango wa Shanhaiguan mkoani Hebei, Mlango wa Jiayuguan mkoani Gansu, na Mlango wa Juyongguang kwenye kitongoji cha Beijing. Lakini milango hiyo haichukuliwi tena kuwa ni milango ya sehemu ya mpakani, bali ni sehemu zenye vivutio zilizofunguliwa kwa watalii. Lakini Mlango wa Urafiki kwenye sehemu ya mpaka kati ya China na Vietnam bado ni mlango wa sehemu ya mpaka, bado ni sehemu muhimu ya mawasiliano kati ya wakazi wa sehemu ya China na wakazi wa sehemu ya Vietnam.

Mwandishi wetu wa habari alikutana na marafiki wengi wa Vietnam waliorudi nyumbani kupitia Mlango wa Urafiki, baadhi yao walifanya kazi nchini China, na wengine walisoma nchini China, ambapo walikuwa wanarudi nyumbani kwa ajili ya likizo. Mfanyakazi wa upande wa China Bibi Li Haixia aliyekuwa anaambatana na marafiki hao wa Vietnam kupita Mlango wa Urafiki alimwambia mwandishi wetu habari akisema:

"Wavietnam hao wanapanda basi la kampuni yetu kurudi Vietnam. Hivi sasa wavietnam wengi wamekuja kusoma au kufanya kazi katika sehemu mbalimbali nchini China. Wamekodisha basi la kampuni yetu, hivyo sisi tunaambatana nao kufanyiwa utaratibu wa kupita forodhani".

Kwenye kando mbili za Mlango wa Urafiki kuna milima mirefu, sehemu hiyo ilikuwa sehemu iliyokuwa ikigombewa sana na makundi ya kijeshi. Mwishoni mwa karne ya 19, jeshi la China lilipambana na jeshi la Ufaransa lililoivamia China na kulirudisha nyuma kutoka kwenye sehemu hiyo. Hivi sasa watalii wanaweza kutembelea sehemu hiyo ya Mlango wa Urafiki wenye mabaki ya vituo vya mizinga, wakikumbushwa kuwa, maisha yao ya amani hayakupatikana kirahisi.

Tukipanda basi kuelekea kwenye sehemu ya kaskazini ya Mlango wa Urafiki wa Pingxiang, baada ya saa mbili utafika kwenye Wilaya ya Daxin iliyoko kwenye sehemu ya mpaka kati ya China na Vietnam. Kwenye wilaya hiyo kuna sehemu mbili zenye vivutio zinazowavutia watalii, moja ni Shamba la Mingshi, nyingine ni Maporomoko makubwa ya Detian. Shamba la Mingshi linaonesha mandhari nzuri ya vijiji vya mkoani Guangxi, watalii wanaweza kupanda mashua ndogo ya mianzi kutembelea sehemu ya shamba hilo, wataona kuwa kando mbili za mto kuna mashamba ya mimea, mapangaboi ya maji, msitu wa mianzi na milima mirefu yenye miti mingi, ambapo watajisikia raha starehe. Mtalii kutoka Taiwan Bibi Luo Caiqing alimwambia mwandishi wetu habari kuwa hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutembelea mkoani Guangxi akisema:

"Sehemu hii ina mandhari nzuri sana, na milima ya hapa hata sisi hatujawahi kuiona".

Katika sehemu ya Shamba la Mingshi, milima inayoegemeana inatambaa bila ukomo na kuwavutia watu macho. Kabla ya kuondoka kutoka kwenye shamba hilo, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, chini ya milima na mto, mkulima mmoja alikuwa akilima shamba kwa ng'ombe, kwenye kijiji kilichoko mbele yake, familia moja moja zilipika chakula na moshi wa jikoni ulikuwa unafuka kuelekea angani. Mandhari ya mashamba ilimfanya mwandishi wetu wa habari ajione kama yuko kwenye dunia iliyosimuliwa kwenye hekaya.

Maporomoko ya Detian ni maporomoko makubwa yanayovuka mpaka kati ya China na Vietnam kwenye sehemu ya juu ya Mto Guichunhe. Chanzo cha Mto Guichunhe kiko nchini China, mto huo unatiririka na kuingia nchi ya Vietnam kutoka Mkoa wa Guangxi, China, halafu unatiririka na kurudi mkoani Guangxi. Maporomoko hayo yana upana wa mita 100 na urefu wake ni mita 80, hayo ni maporomoko makubwa kabisa barani Asia, na ni maporomoko makubwa ya pili yanayovuka mpaka wa nchi mbili. Wakati wa majira ya siku za joto, maji ya mto ni mengi zaidi, maporomoko hayo yanaweza kuporomoka kwa ngazi tatu kutoka juu hadi kubwagwa chini, kweli yana mvuto mkubwa sana, ukubwa wa maporomoko hayo unawashangaza watu, hata kutoka kwa mbali watu wanaweza kusikia ngurumo ya maji yanayotiririka.

Tukisimama kwenye kando ya maporomoko, tutaona kuwa sehemu ya kando nyingine ya Mto Guichunhe ni ya nchi ya Vietnam, na katikati ni mnara mmoja ya mipaka kati ya China na Vietnam. Ni kama hali ilivyo ya Shamba la Mingshi, kwenye kando mbili za Mto Guichunhe pia kuna wakulima wengi ambao wameishi huko kizazi hadi kizazi katika miaka mingi iliyopita. Wakulima hao wanategemea kazi ya kulima mashamba ya ngazi kwenye milima, au kuvua samaki kwenye mto kwa ajili ya kumudu maisha. Watalii wanaotembelea sehemu hiyo, wanaweza kuona kuwa, kwenye sehemu hiyo, kule mbali kuna maporomoko makubwa yanayoporomoka kwa kasi, lakini karibu nao wakulima wanalima kwenye mashamba yaliyoko kando ya Mto Guichunhe ambao maji yake yanatiririka kwa utulivu, ambapo mandhari nzuri ya huko yanaonekana ni nzuri ambayo kama inaweza kuonekana tu peponi. Mtalii kutoka Taibei kisiwani Taiwan Bibi Lin Yongzhen alisema:

"Tunaona kuwa sehemu hiyo yenye mandhari nzuri ya milima na mto inatuvutia sana. Maporomoko makubwa ni kivutio kweli, kama tukija wakati wa msimu ambao mvua inanyesha zaidi, hakika maporomoko hayo makubwa yatawavutia zaidi watalii".

Bibi Lin Yongzhen alisifu sana Shamba la Mingshi na Maporomoko ya Detian, alisema kutembelea sehemu hiyo yenye vivutio kama hivyo, kweli tumekaa katika sehemu ya utulivu sana, kama tunajiburudisha nje ya dunia. Vivutio hivyo viko kwenye sehemu ya mpakani vinatufanya tuone kama kuna hali ya miujiza zaidi. Bibi Lin Yongzhen pia aliwafamisha watu kwamba, kama wanataka kutembelea sehemu hiyo, wakienda wanapaswa kuhifadhi kila kitu cha sehemu hiyo, kabisa wasifanye uharibifu wowote, ili mazingira ya asili yenye mandhari nzuri yawaburudishe watu wote.

Wasikilizaji wapendwa, sasa tunatoa maswali mawili ya leo: 1. Kinanda cha kale cha kabila la wazhuang kinaitwaje? 2. Maporomoko ya maji ya Detian yako kwenye sehemu ya mpaka kati ya China na nchi gani?