Mshauri mwandamizi anayeshughulikia masuala ya Iraq katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani tarehe 10 huko Baghdad alisisitiza kuwa, Marekani na Iraq zitafikia makubaliano ya usalama mwishoni mwa Julai. Hivi sasa mazungumzo hayo kuhusu makubaliano yaliyoanzishwa mwezi Februari yanaendelea faraghani, masuala kuhusu hadhi ya jeshi la Marekani nchini Iraq na mamlaka ya Iraq yanafuatiliwa zaidi na pande mbalimbali.
Mazungumzo kuhusu makubaliano ya usalama kati ya Marekani na Iraq yanafanyika kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais George Bush na waziri mkuu wa Iraq Bw. Nouri al-Maliki mwezi Novemba mwaka jana, taarifa imesema "Marekani inaunga mkono Iraq kulinda mfumo wake wa demokrasia na kupinga tishio kutoka nchini na nje ya Iraq". Mazungumzo hayo yanahusu nyaraka mbili, moja ni kuhusu hadhi ya jeshi la Marekani nchini Iraq, nyingine ni msingi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili. Pande mbili zina matumaini kuwa zinaweza kufikia makubaliano kati yao kabla ya mwezi Julai mwaka huu.
Vyombo vya habari vinaona kuwa serikali ya Marekani inajaribu kujipatia ukaliaji wa kijeshi wa muda mrefu nchini Iraq na kuendelea kuwa na haki ya kuchukua hatua za kijeshi bila ya idhini ya serikali ya Iraq.
Baada ya kudokezwa kwa habari kuhusu mazungumzo hayo, watu wa kundi la Moqtada al-Sadr walifanya maandamano ya kupinga Marekani na kuchoma moto bendera ya Marekani wakipinga makubaliano hayo ya usalama. Mwenyekiti wa Kamati ya Waislamu Bw. Abdul-Aziz Hakim alisema, kutokana na kudhuru mamlaka ya Iraq, nguvu ya uzalendo ya Iraq inakataa vifungu vilivyotolewa na Marekani kwenye makubaliano ya usalama.
Kutokana na shinikizo kubwa, serikali ya Bw. Maliki ilisisitiza msimamo wa Iraq, kwamba bila idhini ya serikali ya Iraq, jeshi la Marekani haliruhusiwi kuondoka kutoka kwenye vituo vyao vya muda vya kijeshi, hatua yoyote ya kijeshi ni lazima iidhinishwe na serikali ya Iraq, matumizi ya fedha ya jeshi la Marekani nchini Iraq lazima zisimamiwe na benki kuu ya Iraq, hatua ya kumkamata Mwiraq yeyote lazima ikubaliwe na serikali ya Iraq, kinga ya askari wa jeshi la Marekani nchini Iraq inaheshimika tu wakati wa operesheni ya kijeshi na ni lazima ipate idhini ya serikali ya Iraq.
Ingawa pande mbili zina tofauti kubwa, lakini Marekani inailazimisha serikali ya Iraq isaini makubaliano hayo mwishoni mwa Julai kwa kuitishia kudhibiti akiba ya Iraq ya dola za kimarekani milioni mia kadhaa kwenye benki ya New York. Lakini vyombo vya habari vya Mashariki ya Kati vinaona kuwa makubaliano hayo kati ya nchi hizo mbili yanakabiliwa na matatizo mengi.
Kwanza, wagombea urais wa vyama viwili vya Marekani wana misimamo tofauti kuhusu masuala ya Iraq, ambayo itaathiri mwelekeo wa sera za Marekani kuhusu masuala ya Iraq, hatua za serikali ya George Bush zitaathiriwa na mambo ya kisiasa.
Pili, Marekani inajaribu kupitia mazungumzo ya faragha kukiuka sheria na kuingilia mamlaka ya Iraq kwa kisingizio cha "kuunga mkono Jamhuri ya Iraq kulinda mfumo wa demokrasia". Kitendo hicho kimesababisha upinzani mkali kutoka kwa makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Iraq na kuleta utatanishi zaidi wa kisiasa katika mchakato wa ukarabati wa Iraq.
Nchi jirani za Iraq hasa Iran zinafuatilia sana ukaliaji wa jeshi la Marekani nchini Iraq. Spika wa bunge la Iran Bw. Ali Rarijani amewataka watu wa Iraq wapinge makubaliano hayo, akisema, njia pekee ya kutimiza hali ya usalama nchini Iraq ni wakaliaji wa nchi za nje kuondoka nchini humo, makubaliano ya usalama kati ya Marekani na Iraq ni changamoto kwa serikali ya Iraq na wananchi wake.
Kutokana na sababu hizo ni vigumu kusainiwa kwa makubaliano ya usalama kati ya Marekani na Iraq, na hata yakisainiwa pia ni vigumu kwa pande mbalimbali kuyakubali.
|