Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-12 16:29:42    
Mfanyakazi wa kusafisha barabara apewa sifa kwa kuchapa kazi

cri

Saa 10 alfajiri wakati watu wengi kabisa wanakuwa bado wamelala, Bw. Xu Hui anakuwa ameanza kazi ya kufagia barabara, yeye ni mfanyakazi wa idara ya usafi mjini Ningbo, mashariki mwa China.

Bw. Xu Hui mwenye umri wa miaka 41 alihama kutoka maskani yake iliyoko mkoani Anhui na kuhamia mji wa Ningbo, mkoani Zhejiang China, na kuanza kufanya kazi ya kusafisha barabara.  Alisema "Maskani yangu iko Wuhu, mkoani Anhui, mke wangu alitangulia kuhamia mji Ningbo. Kazi hiyo ya kusafisha barabara ni kazi ngumu, lakini ni kazi yenye kipato cha uhakika. Kwa hiyo niliamua kuja Ningbo na ninakuwa nikifanya kazi hiyo hadi sasa."

Tangu siku ya kwanza alipoanza kufanya kazi hiyo, Bw. Xu Hui alikaza nia kuwa, "ni lazima kuchapa kazi hata kama kazi hiyo ni kufagia barabara."

Kazi ngumu aliyopewa Bw. Xu Hui ni kusafisha barabara kwenye eneo moja lenye maduka mengi na msongamano wa watu, pia kuna soko la chakula. Kila asubuhi Xu Hui anafagia barabara hizo kwanza, halafu anaanza kutembea kwenye barabara hizo ili kuondoa takataka mara moja. Anafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kiasi kwamba anaweza kumaliza kusafisha barabara hizo zenye urefu wa mita 700 hivi ndani ya dakika 12. Zaidi ya hayo Bw. Xu Hui anajitolea kuwaelimisha wapita njia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, kuwaonesha mapipa ya takataka, kuwakumbusha wenye maduka wasitupe takataka ovyo ovyo na kuweka mapipa ya muda karibu na maduka hayo.

Siku nenda siku rudi, wenye maduka wengi kabisa walipokea ushauri wa Bw. Xu Hui, na waliacha tabia mbaya ya kutupa takataka ovyo. Hivi sasa barabara hizo zinajulikana kwa usafi wake, na Bw. Xu Hui amekuwa maarufu miongoni mwa wakazi wa mji wa Ningbo kutokana na uchapaji wake kazi. Mwaka 2004 Bw. Xu Hui alipewa sifa ya mfanyakazi hodari, ambayo ilitolewa kwa watu waliotoka nje ya mji wa Ningbo.

Mkurugenzi wa Idara ya utunzaji wa mazingira ya mji wa Ningbo Bi. Zhang Jufei alimsifu Bw. Xu Hui, alisema "Yeye anachapa kazi kwa bidii na kwa uchangamfu mkubwa, hajali maslahi yake binafsi. Kwa hiyo mwaka 2004 nilipendekeza ashiriki kugombea sifa hiyo ya mfanyakazi hodari."

Mfanyakazi mwenzake Bw. Li pia alitoa maoni yake kuhusu Bw. Xu Hui, alisema  "Tulifahamiana kabla hatujaondoka kutoka maskani yetu, sisi tulitoka sehemu moja na hivi sasa tunafanya kazi pamoja. Yeye ni mtu makini kazini, pia anapenda kuwasaidia wengine, anatoa mfano mzuri wa kuigwa kwa wafanyakazi wenzetu kutokana na moyo wake wa kuchapa kazi."

Siku moja Xu Hui alipokuwa kazini, alikutana na mzee mmoja aliyeonekana kuwa na wasiwasi mkubwa. Mzee huyo Bibi Tu Chuanxin mwenye umri wa miaka 70 alikuwa amepoteza kadi ya kununulia maziwa. Bw. Xu Hui alimsaidia kutafuta kadi hiyo kwenye mkokoteni wa takataka kwa kutumia mikono, hata alipekua kutoka kwenye takataka za ardhini na kufanikiwa kupata kadi ya mzee huyo. Bibi Tu Chuanxin aliguswa sana hisia zake na tukio hilo, alisema  "Naona yeye anafanya kazi kwa makini, anatoa mchango mkubwa ingawa kazi anayofanya ni ya kawaida tu, na si rahisi kupata mafanikio makubwa kama aliyopata. Nilishuhudia akitafuta kadi hiyo ndani ya mkokoteni wa takataka kwa kutumia mikono yake, niliona yeye ni mtu mwema na mchangamfu, namshukuru sana."

Bw. Xu Hui alipata tuzo na sifa mbalimbali kutokana na uchapaji kazi, pia aliteuliwa kuwa mkimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Zaidi ya tuzo na sifa hizo, suala moja ambalo limekuwa likimsumbua liliondolewa hivi karibuni. Katika muda mrefu uliopita China ilikuwa inafuata utaratibu wa makini wa usajili wa nyumba. Utaratibu huo ulisaidia katika kutoa takwimu sahihi za nguvukazi na kulinda usalama wa jamii, hata hivyo ulikwamisha uhamiaji wa watu. Kutokana na kutekelezwa kwa utaratibu huo makini, wafanyakazi waliohamia kutoka sehemu nyingine mfano wa Bw. Xu Hui walishindwa kupata huduma sawa na wenyeji, huduma hizo ni pamoja na huduma za matibabu na huduma nyingine za kijamii.

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya China katika ngazi mbalimbali imekuwa ikilegeza utaratibu huo hatua kwa hatua. Kwa mfano mji wa Ningbo anakoishi Bw. Xu Hui, serikali ilitoa sera mpya ya kuwapa uhifadhi wa jamii wafanyakazi waliohamia kutoka sehemu nyingine. Kwa mujibu wa sera hiyo, wahamiaji hao ni kama wenyeji, ambao wanaweza kunufaika na bima za aina tano wanapojeruhiwa kazini, kupata magonjwa makubwa, kustaafu, kukosa ajira na wanapojifungua. Na wafanyakazi wapatao milioni 2.85 waliohamia kwenye mji wa Ningbo kutoka sehemu nyingine wote wanalindwa na mfumo wa bima za jamii.

Zaidi ya hayo serikali ya mji wa Ningbo hivi karibuni iliamua kuwavutia wafanyakazi hodari kutoka sehemu nyingine waishi mjini Ningbo na kuwapa hati za ukazi kwa kudumu mjini humo.

Bw. Xu Hui alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, anafurahia maisha ya hivi sasa. Alisema  "Mwanzoni nilipofika Ningbo, nilifurahia utulivu wa ajira hiyo na jinsi serikali ya huko ilivyowatilia maanani wafanyakazi waliohamia kutoka sehemu nyingine, kwa hiyo niliona ni lazima nitekeleze wajibu wangu kazini, sikuwahi kufikiria kupata sifa au tuzo, hata kupata kadi ya ukazi wa kudumu hapa mjini, hii ni kama ndoto kwetu."

Idhaa ya kiswahili 2008-06-12