Tarehe 12 Umoja wa Nchi za Kiarabu na Umoja wa Afrika ulizitaka Eritrea na Djibouti zitatue mgogoro wa mpakani kwa njia ya mazungumzo. Wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu tarehe 12 walifanya mkutano wa dharura, azimio lililopitishwa kwenye mkutano huo lilizitaka Eritrea na Djibouti ziondoe majeshi yao kutoka mpakani. Azimio hilo linasisitiza kwamba mamlaka, umoja na ukamilifu wa ardhi wa Djibouti lazima viheshimiwe, kwani kulinda maslahi ya taifa ni haki ya Djibouti na limemtaka katibu mkuu na Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Nchi za Kiarabu aendelee kufanya juhudi kutatua mgogoro huo. Azimio hilo lilimwagiza katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu na serikali ya Djibouti wawasiliane kwa lengo la kupunguza mgogoro huo na kuzuia migongano mpakani. Katika siku hiyo hiyo Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika pia ilifanya mkutano na kuonesha kuwa na wasiwasi kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizo mbili, na kuzitaka pande mbili ziwe na uvumilivu ili kuzuia mgogoro huo usiwe mkali zaidi.
Djibouti na Eritrea ziliwahi kukumbwa na mgogoro wa mpakani mara mbili. Mwaka 1996 Djibouti iliishutumu Eritrea kwa kuishambulia kwa kutumia mizinga, na mgogoro wa kugombea ardhi ukatokea. Mwaka 1998 baada ya mgogoro wa mpaka kati ya Eritrea na Ethiopia kutokea, Eritrea iliishutumu Djibouti kwa kuiunga mkono Ethiopia na kuitaka Djibouti ijiondoe kutoka kamati ya Umoja wa Afrika ya kusuluhisha mgogoro kati ya Eritrea na Ethiopia, kisha nchi hizo mbili zilisimamisha uhusiano wa kibalozi mpaka mwaka 2000.
Mgogoro wa sasa kati ya Eritrea na Djibouti ulitokea katika pembe ya Afrika kaskazini mwa Djibouti. Sehemu hiyo ni muhimu sana kwa sababu ya kuwa karibu na mlango wa bahari, meli zote za nchi za nje na meli za mafuta za nchi za Kiarabu zinapita kwenye mlango huo. Tarehe 12 kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kilitangaza kuwa ofisa mmoja wa Djibouti alithibitisha kuwa tarehe 10 jeshi la Eritrea liliingia kwenye ardhi ya Djibouti na kusababisha vifo vya askari 9 na wengine 60 kujeruhiwa. Kabla ya hapo nchi hizo mbili zilikuwa na mgogoro wa mpaka kwa miezi kadhaa. Ingawa Djibouti na Eritrea ni nchi ndogo barani Afrika, lakini kutokana umuhimu wa mahali zilipo, na zimeongeza hali ya vurugu barani humo na kusababisha uhusiano kati ya nchi nne zilizopo kwenye pembe hiyo, Somalia, Ethiopia, Eritrea na Djibouti kuwa na utatanishi zaidi, mgogoro huo unafuatiliwa zaidi na vyombo vya habari.
Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti tarehe 12 alionya kuwa nchi yake italinda ardhi yake kwa njia yoyote ile. Baada ya mkutano wa dharura mwakilishi wa Djibouti katika Umoja wa Nchi za Kiarabu alisisitiza kuwa Djibouti ina nguvu za kutosha kulinda ukamilifu wa ardhi yake, na jeshi la Djibouti limedhibiti sehemu kubwa iliyonyakuliwa na yenye mahandaki yaliyochimbwa na jeshi la Eritrea, Djibouti itarudisha ardhi yake yote kutoka mikononi mwa jeshi la Eritrea. Alishutumu kwamba Eritrea inajaribu kuharibu utulivu wa Djibouti na hata Afrika nzima, lakini huku alisema anatumai mgogoro huo utatatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu anayeshughulia mambo ya siasa Bw. Ahmad Bin Hali tarehe 12 baada ya mkutano wa dharura wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Nchi za Kiarabu itaimarisha mawasiliano na Kamati ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika, ana matumaini kwamba mgogoro kati ya nchi hizo mbili utatatuliwa kwa njia ya amani.
Idhaa ya kiswahili 2008-06-13
|