Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-16 14:56:55    
Xinyang yenye mandhari nzuri ya milima na mito

cri

Mji wa Xinyang mkoani Henan uko kwenye sehemu ya kati ya China, watu wanasema sehemu hiyo ni kaskazini mwa nchi ya kusini, na ni kusini mwa nchi ya kaskazini, Xinyang ni mahali penye mandhari nzuri ya milima na mito, pamoja na hali ya hewa nzuri, huko kuna hekalu la kale lililojengwa zaidi ya miaka 1,000 iliyopita linaloitwa "Hekalu la Lingshan" pamoja na mahali pazuri kwa kukwepa joto panapoitwa "Mlima wa Jogoo", tena kuna chai ya "Xinyang Maojian" ambayo ni moja kati ya aina kumi maarufu za chai nchini China.

Mji wa Xinyang uko kwenye sehemu ya mpakani kati ya hali ya hewa ya kusini na ya kaskazini, hivyo hewa ya sehemu hiyo ni yenye unyevunyevu, na miti na majani mengi yanasitawi kwenye sehemu hiyo. Kwenye umbali wa zaidi ya kilomita 40 kusini magharibi mwa mji wa wilaya ya Luoshan ya mji wa Xinyang, kuna "Hekalu la Lingshan" lililojengwa zaidi ya miaka 1,000 iliyopita. Ndani ya hekalu hilo kuna kisima kimoja, na maji ya kisima hicho ni matamu sana, hivyo watu wanakiita kisima hicho kuwa ni "Kisima Kitakatifu". Inasemekana kuwa maji hayo ya chemchemi yanatoka chini ya tandiko analokaa budha kwenye ukumbi wa nyuma wa hekalu. Tena ndani ya hekalu hilo kuna mvinje mmoja unaoitwa "Daozaibo", ambao hali yake ni tofauti na miti mingine, ambayo sehemu ya chini ya mti ni nyembamba, na sehemu yake ya juu ni nene, mvinje huo ulipandikizwa zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, lakini bado umestawi sana. Mandhari ya sehemu ya "Hekalu la Lingshan" inavutia watu sana kutokana na maji safi ya ziwani, anga la buluu na milima yenye miti ya kupendeza, ambapo watalii hawataki kuondoka. Mtalii kutoka Beijing, Bi. An Lihong ni mmoja kati ya watalii hao, alisema,

"Kweli ninaona sehemu ya mandhari ya hekalu la Lingshan ni kama watu walivyosema, ni 'kaskazini mwa nchi ya kusini', na ni 'kusini mwa nchi ya kaskazini', mandhari yake ya kimaumbile ni nzuri sana, tena mazingira yake yamehifadhiwa vizuri pia. Kwenye njia tuliyopita wakati wa kupanda mlimani, tuliona samaki wadogo wakiogelea kwenye kimfereji kilichoko kwenye kando ya njia, pia tuliwaona kaa wadogo, na maji ya kimfereji hicho ni masafi sana. Vijana wenzetu walitaka kuvua nguo na kuogelea kwenye kimfereji kile. Ni kweli kuwa binadamu na maumbile tumeungana pamoja barabara."

Hekalu la Lingshan ni la kipekee kwenye dini ya kibudhaa nchini China, ambalo watawa wa kiume na wa kike wanajifunza mambo ya dini kwa pamoja na bila kunyolewa nywele. Wafalme wa kwanza wa enzi za Song na Ming wote waliwahi kufika kwenye hekalu la Lingshan, mfalme wa kwanza wa enzi ya Ming Zhu Yuanzhang aliandika maneno yeye mwenyewe kwa ajili ya ubao uliotundikwa kwenye lango la hekalu, na kulipa sifa hekalu hilo ya "hekalu la taifa". Bw. Gui Junfeng kutoka kampuni ya maendeleo ya utalii ya mandhari ya hekalu la Lingshan, alisema,

"Hekalu la Lingshan limekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1,500, na ni moja kati ya mahekalu yaliyojengwa mapema sana baada ya dini ya kibudha kuingia nchini China. Jianning, binti wa mfalme Xuanzong wa enzi ya Tang, alikuwa mtawa katika hekalu hilo. Mfalme wa kwanza wa enzi ya Ming, Zhu Yuanzhang, alipewa msaada na watawa wa hekalu hilo, alipokuwa mtu maskini, baada ya kuwa mfalme wa nchi, alifika kwenye hekalu la Lingshan mara tatu."

Habari zinasema, tarehe 1 mwezi wa tatu kwa kalenda ya kichina ni siku ya kufanyika kwa gulio ya jadi kwenye hekalu la Lingshan, na kila ikifika wakati huo, njia za mlimani huwa na msongamano wa watu, hata idadi ya watu wanaolitembelea gulio hilo inaweza kufikia elfu kumi kadhaa kwa siku.

Wapendwa wasikilizaji, sasa hebu tuwafahamishe kuhusu mlima wa jogoo. Mlima wa jogoo uko kusini mashariki mwa mji wa Xinyang, unatazamana na hekalu la Lingshan kwa mbali, na ni moja kati ya sehemu maarufu za kukwepa joto nchini China. Mlima wa jogoo ni mzuri na wenye miti mingi ya kupendeza, mlima huo uko kwenye mwinuko wa zaidi ya mita 700, mlima huo unaonekana kuwa na umbo la kama jogoo anayewika, hivyo mlima huo unaitwa mlima wa jogoo.

Kwenye mlima jogoo, kuna mimea zaidi ya aina 1,200 inayoota na kustawi, mandhari yake tofauti katika majira manne ya mwaka yanavutia watu sana. Kila ifikapo majira ya joto, hata kama sehemu nyingine zikiwa na joto kali, lakini sehemu ya mlima jogoo bado inakuwa na baridi kidogo.

Mbali na hekalu la Lingshan na mlima wa jogoo, kwenye sehemu ya Xinyang kuna ziwa Nanwan, ambalo ukubwa wake ni mara 12 kuliko ziwa Xihu la Hangzhou. Sehemu ya utalii ya mandhari ya ziwa Nanwan iko kwenye kilomita 5 kusini magharibi mwa mji wa Xinyang, mkoani Henan, na inajulikana kwa watu wengi kutokana na kuwa na mchanganyiko wa vivutio vya milima, mito, misitu na visiwa, ziwa hilo lenye eneo la kilomita za mraba 75, linawavutia sana watu kwa ukubwa wake, ambalo lina visiwa 61 vyenye maumbo mbalimbali. Kwenye kisiwa cha ndege, wanaishi ndege wengi na milio yao inasikika kila mahali. Habari zinasema kila mwaka kuna ndege laki moja hivi wanaopita kwenye sehemu hiyo, na wanazaliana huko. Sehemu ya ziwa la Nanwan ina rasilimali nyingi za viumbe, na aina zake zinazidi 1,000, wakiwemo nyani, mamba wa Yangzi, fungo wadogo na kware wenye mkia mrefu; sehemu ya ziwa Nanwan pia ni mahali penye hewa nyingi za oxygen, na sehemu yake zaidi ya 75 ni misitu.

Mtalii Bi. Zhang Yi kutoka sehemu ya kaskazini ya China, alifanya matembezi kwenye ziwa lNanwan la Xinyang kwa kutumia siku za mapumziko ya siku ya wafanyakazi, kabla ya kufunga safari alisikia kuwa ziwa la Nanwan ni sehemu yenye mandhari nzuri ya maji, milima, ndege na visiwa, baada ya kufika huko aliona yote ni ya kweli kabisa. Alisema,

"Leo ninatembelea ziwa la Nanwan, tumefika sehemu hii kwa kupanda mashua, nimeona visiwa vingi kwenye ziwa, ninaona mandhari ya hapa ni nzuri sana, ninatarajia kuwa watu wanaopenda kutalii waje kuangalia na kujiburudisha kwa vivutio vya hapa."

Mji wa Xinyang licha ya kuwa na sehemu zenye mandhari nzuri na mabaki maarufu ya kale, pia una chai ya kijani ya "Xinyang Maojian", ambayo imekuwa maarufu nchini na katika dunia. Kutokana na kuwa na mwangaza mwingi wa jua pamoja na mvua nyingi, sehemu hiyo inafaa sana kwa uotaji wa michai. Habari zinasema chai ya Xinyang Maojian ilikuwa chai inayotumika katika jumba la mfalme. Mwaka 1915 chai hiyo ilipata tuzo ya dhahabu kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa huko Panama. Chai ya Xinyang Maojian inafanya kazi vizuri ya kujenga mwili, inaweza kuondoa mafuta yaliyoko katika damu, inaburudisha, kuondoa joto ya mwilini na kurefusha muda wa kuishi kwa binadamu.

Idhaa ya kiswahili 2008-06-16