Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-16 19:21:24    
Historia ya mazungumzo ya mkakati wa kiuchumi kati ya China na Marekani

cri

Mazungumzo ya nne ya mkakati wa kiuchumi kati ya China na Marekani yatafanyika tarehe 17 na 18 huko Annapolis, nchini Marekani, ambapo naibu waziri mkuu wa China Bw. Wang Qishan na waziri wa fedha wa Marekani Bw. Henry Paulson wataendesha mazungumzo hayo kwa pamoja.

Hayo ni mazungumzo ya ngazi ya juu zaidi miongoni mwa mazungumzo yaliyopo kati ya China na Marekani, pia ni yanatoa nafasi kwa maofisa waandamizi wa mambo ya kiuchumi wa nchi hizo mbili kubadilishana maoni. Mazungumzo hayo yalizinduliwa tarehe 20 Septemba mwaka 2006 na aliyekuwa naibu waziri mkuu wa China Bi. Wu Yi na waziri wa fedha wa Marekani Bw. Henry Paulson.  Kwenye sherehe ya uzinduzi, Bi. Wu Yi alisema "Kutokana na utandawazi wa kiuchumi unavyoimarika duniani na uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Marekani kuwa karibu siku hadi siku, tumeanzisha mazungumzo hayo ya kimkakati katika sekta ya uchumi kati ya nchi kubwa kabisa inayoendelea na nchi kubwa kabisa iliyoendelea."

Mazungumzo ya mkakati wa kiuchumi yanafanyika mara mbili kwa mwaka, na China na Marekani zinabadilishana zamu ya uenyeji wa mkutano huo. Chini ya uendeshaji wa Bi. Wu Yi na Bw. Henry Paulson, mazungumzo hayo yalifanyika kwa mara tatu. Mazungumzo ya kwanza yalifanyika tarehe 14 na 15 Desemba mwaka 2006 hapa Beijing. Masuala yaliyojadiliwa yalikuwa ni pamoja na maendeleo yenye uwiano kati ya miji na vijiji, maendeleo endelevu ya uchumi wa China, namna ya kuhimiza biashara na uwekezaji, nishati, mazingira na maendeleo endelevu. Baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo Bi. Wu Yi alisema,  "Mimi na waziri wa fedha Bw. Paulson pamoja na mawaziri kutoka ujumbe wa China na Marekani tumekubaliana kuwa, mazungumzo hayo ya kwanza yamepata mafanikio makubwa, kwani yatasaidia kukuza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani katika siku zijazo, na kukuza uhusiano na ushirikiano wa kiujenzi kati ya nchi hizo mbili."

Mazungumzo ya pili yalifanyika tarehe 22 na 23 Mei, mwaka 2007 huko Washington, mji mkuu wa Marekani. Baada ya mazungumzo hayo, Bw. Paulson alisema  "Leo tumefikia maoni ya pamoja kuhusu mambo mengi yanayohusu ushirikiano kati ya nchi zetu mbili katika siku zijazo, yakiwemo masuala muhimu kuhusu huduma za fedha, matumizi ya nishati, mazingira na safari za ndege za abiria. Utaratibu wa mazungumzo hayo utaendelea kuwepo na sisi pia tutadumisha moyo wa kufanya ushirikiano."

Tarehe 12 na 13 Desemba mwaka 2007 mazungumzo ya tatu ya mkakati wa kiuchumi kati ya China na Marekani yalifanyika hapa Beijing. Ajenda kuu ya mazungumzo hayo yalikuwa jinsi ya kutumia ipasavyo fursa za utandawazi wa uchumi duniani na kukabiliana na changamoto za utandawazi wa uchumi duniani. Mazungumzo hayo yalifikia maoni ya pamoja kuhusu mambo 31 na kusaini makubaliano yanayohusika. Baada ya mazungumzo hayo, rais Hu Jintao wa China alikutana na waziri wa fedha wa Marekani Bw. Paulson, alimwambia mgeni wake kuwa  "Mazungumzo yaliyomalizika hivi karibuni yalipata mafanikio makubwa kwa kufikia makubaliano mengi. Natoa pongezi na shukrani kwa uhodari wa naibu waziri mkuu Bi. Wu Yi na waziri wa fedha Bw. Paulson katika kuendesha mazungumzo, na kwa jitihada kubwa zilizofanywa na idara husika za China na Marekani katika kufanikisha mazungumzo hayo."

Mazungumzo hayo ya nne yanatarajiwa kufanyika hivi karibuni, ambapo China na Marekani zitajitahidi kukuza uhusiano wa kiuchumi kati yao ili kuwanufaisha zaidi watu wa nchi hizo mbili.